Nimeanza kusoma As You Like It, moja ya tamthilia za Shakespeare. Ni wazi kuwa, nikizingatia kwamba leo ni tarehe 28 Desemba, hiki kitakuwa kitabu cha kumalizia mwaka.
Kama zilivyo tamthilia zingine za Shakespeare, As You Like It ni hazina kubwa ya mafundisho kuhusu mahusiano baina ya wanadamu na kuhusu maisha kwa ujumla. Tamthilia yoyote ya gwiji huyu, sawa na mashairi yake, ni hazina ya lugha ya ki-Ingereza.
Ningefurahi kama ningekuwa nimesoma angalau kitabu kimoja kwa kila wiki. Padre Lambert Doerr, OSB, mwalimu wetu wa ki-ingereza tulipokuwa tunasoma seminari ya Likonde, ambaye sasa ni abate askofu mstaafu, alitushinikiza kusoma angalau kitabu kimoja kwa wiki. Kila mmoja wetu alipewa daftari ambamo alitakiwa kuorodhesha vitabu alivyosoma, na alitegemewa kuweza kutoa maelezo mafupi kuhusu kila kitabu. Ningefurahi kama ningeweza kuendeleza jadi hii miaka yote.
Nirudi tena kwenye As You Like It. Simulizi inapoanza, tunamsikia Orlando akilalamika kuwa amedhulumiwa na kaka yake mkubwa, Oliver, kuhusu urithi. Anasema kuwa baba yao aliacha wosia kwamba Oliver amgawie yeye Orlando fungu fulani la mali yake na pia amsomeshe, lakini Oliver hakufanya hvyo. Dhuluma hii inamsononesha Orlando.
Mtindo huu wa kuanzia simulizi na mhusika akielezea masononeko tunauona pia katika tamthilia ya Shakespeare iitwayo The Merchant of Venice. Halafu katika sehemu hii ya mwanzo ya As You Like It kuna pia dhamira ya kiongozi kuporwa madaraka na ndugu yake, dhamira ambayo inajitokeza pia katika The Tempest, tamthilia nyingine ya Shakespeare. Hili suala la Shakespeare kurejea tena na tena kwenye dhamira au kipengele fulani cha sanaa yake nimeligusia kabla katika blogu hii.
Tangu mwanzoni mwa As You Like It, Shakespeare anatuweka katika hamaki ya kujua nini kitakachofuata katika mtiririko wa matukio. Vile vile, kama ilivyo kawaida yake, anatupeleka mbali katika ulimwengu wa fasihi na masimulizi na imani za zamani, kuanzia enzi za wa-Griki hadi wa-Ingereza wenyewe. Mifano ya wahusika wa masimulizi hayo ni Fortune na Robin Hood.
Sijui kama nitaweza kumaliza kusoma tamthilia hii kabla ya mwaka mpya kuanza, lakini nitajitahidi. Jambo moja linalonifanya nisome pole pole ni kuvutiwa na umahiri wa Shakespeare katika kutumia lugha kwa namna ambayo aghalabu haionekani katika ki-Ingereza cha leo.
Ni aina ya chemsha bongo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment