Thursday, December 11, 2014

Sitafundisha Mwezi Januari, 2015

Awali, kwa ratiba iliyopangwa, nilitarajiwa kufundisha mwezi Januari, kozi iitwayo "The Hero and the Trickster." Hiyo ni kozi ambayo nimefundisha karibu kila mwaka, mwezi Januari. Tuna utaratibu, katika chuo hiki cha St. Olaf kuwa na kozi za mwezi Januari ambazo zinaitwa "interim." Kozi yangu ya "Hemingway in East Africa" ambayo nilifundishia Tanzania, ilikuwa ya aina hiyo.

Pamoja na kwamba ilipangwa kwamba Januari ijayo nifundishe, hivi karibuni, viongozi wa chuo wameonelea nisifundishe bali nipumzike, ili niendelee kupona vizuri. Kwa hali yangu ilivyo, nina hakika ningeweza kufundisha, lakini uongozi wa chuo umeamua kunipa hii likizo ambayo sikuitegemea.

Ninashukuru sana. Ninaona ni mipango ya Mungu, kwani kwa miezi niliyokuwa na hali mbaya kiafya, hadi nikashidwa kufanya kazi nilizozizoea, nilikuwa katika majaribu makubwa. Kutoweza kufundisha, kufanya utafiti, kuandika au kurekebisha makala za kitaaluma ulikuwa ni mtihani mkubwa kisaikolojia.

Kwa bahati nzuri, imani ya dini, kwamba yote anayajua Mungu, na kwamba yeye ndiye mwenye uwezo wote, ilinifanya nisikate tamaa. Hata muuguzi mmoja katika hospitali ya Abbott Northwestern, kule Minneapolis, aliponiuliza inakuwaje kwamba ingawa nilikuwa nimelazwa siku nyingi, sikuonyesha dalili ya kulalamika, kusononeka au kukata tamaa, kama wagonjwa wengine wafanyavyo. Nilimjibu kwamba ninamtegemea Mungu, na sina sababu ya kulalamika, kusononeka wala kukata tamaa. Alivyokuwa ananiangalia usoni, aliona kuwa naongea kwa dhati.

Sasa, huu uamuzi wa viongozi wa chuo kwamba nisifundishe mwezi mzima ninauona kama ni neema ambayo Mungu ananishushia, baada ya kipindi kirefu cha majaribu. Nataka kumia muda ule kwa kujisomea vitabu na kuandika, mambo ambayo, sambamba na ufundishaji, yananiletea raha maishani.

Nimeona niandike ujumbe huu sio tu kwa lengo la kujiwekea kumbukumbu ya yale yanayojiri maishani mwangu, bali kujaribu kuwatia moyo wengine wanaopitia katika kipindi kigumu na majaribu maishani mwao.

2 comments:

Kadebe said...

Ugua pole Dr Membe, "mtetezi wako Kristo yu hai"!

Mbele said...
Ndugu Kadebe

Shukrani kwa ujumbe wako. Kwa kweli, pamoja na ubingwa wa madaktari na huduma bora, namtegemea Mungu. Kauli yako kuwa Kristo ndiye mtetezi ndiyo imani yangu. Ninaendelea vizuri kiafya.

Nakutakia kila la heri kwa Krismasi, Mwaka Mpya, na huko mbele ya safari.

Jina langu ni Mbele.