Monday, December 8, 2014

Vitabu Nilivyonunua Juzi

Juzi, Jumamosi,  nilienda Minneapolis, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Afrifest Foundation, ambayo mimi ni mwenyekiti wake. Wakati wa kurudi, nilipitia Apple Valley, nikaingia katika duka la Half Price Books, ambalo nimeliongelea mara kadhaa katika blogu hii.

Ingawa ilikuwa jioni sana,  watu walikuwa wengi humo dukani: watu wazima, vijana, na watoto. Nami nilijichanganya nao, nikaangalia angalia sehemu zenye vitabu vya fasihi. Nilinunua vitabu vinne, ambavyo nitavielezea leo.

Lakini kabla ya kuelezea vitabu hivi, napenda kujikumbusha kitu kimoja kilichonigusa, wakati nimesimama katika foleni ya kulipia vitabu. Mbele yangu walikuwepo baba na mama na watoto wadogo wawili wasichana. Walikuwa wameshaweka vitabu vyao kwenye kaunta ya kulipia, huku wakiwaelezea wale watoto jinsi watakavyowasomea vitabu. Kati ya vile vitabu kwenye kaunta, niliviona viwili vikubwa vikubwa vya Harry Potter. Muda wote wale watoto walikuwa na furaha na msisimko. Kwa mara nyingine tena, nilishuhudia jinsi wenzetu wanavyowalea watoto wao katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu.

Kitabu kimojawapo nilichonunua ni Much Ado About Nothing, ambayo ni tamthilia ya Shakespeare iliyohaririwa na Barbara A. Mowat na Paul Werstine. Wasomaaji wa Shakespeare wanajua kuwa tamthilia zake zimehaririwa na wahariri mbali mbali katika hii miaka 500 tangu kufariki kwake.

Tamthilia za Shakespeare, ambazo ni 37, hupatikana pia zikiwa zimekusanywa katika kitabu kimoja kikubwa sana. Ingawa ninazo nakala za kitabu hiki--nakala mbili hapa Marekani na nyingine Tanzania--huwa napenda, mara moja moja kununua hivi vitabu vya tamthilia moja moja, kwa vile ni rahisi kubeba katika mkoba na kwenda navyo popote.

Kitabu kingine nilichonunua ni The Pickwick Papers, kilichotungwa na Charles Dickens. Wengi wetu tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu na sabini na kitu tunamkumbuka Dickens na riwaya zake, kama vile Oliver Twist na A Tale of Two Cities. Binafsi, nilimpenda sana Dickens, na nilisoma vitabu vyake kadhaa. Nimewahi kumwongelea Dickens katika blogu hii.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Hemingway on Hunting. Nimenunua toleo lililochapishwa na The Lyons Press, mwaka 2001. Kitabu hiki ni mkusanyo wa maandishi ya Ernest Hemingway yanayohusu uwindaji. Mhariri wake ni Sean Hemingway, mjukuu wa mwandishi mwenyewe. Pia kuna utangulizi mfupi ulioandikwa na Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliyebaki. Sean amekusanya maandishi kutoka katika vitabu  kama vile Green Hills of Africa, For Whom the Bell Tolls, Across the River and into the Trees, na pia makala na barua mbali mbali alizochapisha Ernest Hemingway katika magazeti.

Ingawa mengi ya maandishi hayo ninayo, niliona ni vema kuwa na kitabu hiki ambacho kinahusu hili suala la uwindaji. Ningependa kusema pia kuna kitabu cha aina hiyo hiyo, ambacho ni mkusanyo wa maandishi ya Hemingway kuhusu uvuvi, na kingine kuhusu uandishi. Hemingway, katika falsafa na nadharia zake, aliongelea uhusiano baina ya  uandishi na uwindaji.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Minaret, riwaya iliyotungwa na Leila Aboulela, ambaye alikulia Khartoum na anaishi Dubai na Aberdeen. Ni mwandishi maarufu, ambaye ameshajitwalia tuzo kadhaa kwa uandishi wake. Ingawa nimesikia habari zake kwa miaka kadhaa, sikuwahi kusoma kitabu chake hata kimoja. Leila Aboulela anajulikana kwa umahiri wake kisanaa, pia kwa jinsi anayowaelezea suala la wanawake katika u-Islam kwa mtazamo tofauti na ilivyozoeleka. Nina dukuduku ya kusoma Minaret, kwa kuanzia, na nitapenda pia kusoma riwaya zake zingine.

No comments: