Wednesday, December 31, 2014

Vitabu vya Kukumbukwa Nilivyosoma Mwaka 2014

Leo, siku ya mwisho ya mwaka 2014, napenda kujikumbusha vitabu nilivyosoma mwaka huu ambavyo nitavikumbuka kwa namna ya pekee. Sitavitaja vitabu tulivyovisoma darasani.

Kwanza, napenda kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kushuhudia mwaka 2014 ukiisha, huku zikiwa zimebaki saa nne tu hadi kuanza kwa mwaka 2015. Ingawa huu umekuwa mwaka mgumu kwangu kuliko miaka yote ya maisha yangu kwa sababu ya kuugua, nashukuru nimefikia hapa nilipo, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu, huduma za madaktari, wauguzi na familia yangu, na maombi ya ndugu na marafiki.

Kutokana na hali yangu hiyo, sikuweza kusoma kama ilivyo mazoea yangu. Hata hivi, kila nilipojisikia nafuu, nilishika kitabu na kusoma, hata nilipokuwa nimelazwa hospitalini. Vitabu ni moja ya vitulizo vyangu, na madaktari na wauguzi walitambua jambo hilo.

Nilipokuwa nimelazwa katika hospitali ya Abbott Northwestern, mjini Minneapolis, nilikwenda na kitabu cha mashairi ya Robert Frost kiitwacho Robert Frost: Selected Poems, ambacho binti yangu Zawadi alikuwa amenipa, kama nilivyoelezea hapa. Nilijitahidi kusoma mashairi mengi yaliyomo. Kabla ya kitabu hiki, nilikuwa nimesoma mashairi machache ya Frost wakati wa ujana wangu, na kati ya mashairi hayo, moja ambalo nimelikumbuka daima ni "The Road Not Taken."

Ninafurahi kuwa nimepata fursa ya kusoma mashairi mengi ya Frost mwaka huu 2014, ingawaje, kwa ujumla, yanahitaji tafakari sana, na kama mtu ni mvivu, hatafika mbali katika kuyasoma. Hata hilo shairi la "The Road Not Taken" linatuacha njia panda.

Kwa sababu kama hizi nilizotoa hapa juu, nitamkumbuka Robert Frost kwa namna ya pekee kama mmojawapo wa waandishi niliowasoma mwaka 2014. Nimeweza kupanua upeo wangu wa kumfahamu mshairi huyu maarufu.

Kitabu kilichonigusa kwa namna ya pekee ni The Pearl, riwaya ya John Steinbeck, ambayo niliielezea hapa. Ni riwaya inayosomeka kirahisi na inavutia kama sumaku kwa mtiririko wa matukio yake na jinsi inavyoelezea  tabia za binadamu, kama vile upendo na wivu, wema na ubaya. Ni riwaya ambayo sitaweza kuisahau.

Nimepata fursa ya kujiongezea ufahamu wa Shakespeare kwa kusoma Macbeth, tamthilia yake mojawapo ambayo sikuwa nimeisoma. Niliiongelea tamthilia hii katika blogu hii. Sina matumaini ya kusoma tamthilia zote 37 za Shakespeare. Ni nani amezisoma zote? Hii ndio hali halisi katika ulimwengu wa fasihi. Hata usome saa nyingi kila siku na kwa miaka yote ya maisha yako, utakachokuwa umefanya ni kama kuchota maji ndoo moja katika bahari inayoendelea kujaa maji. Kuna waandishi wengi maarufu, wa zamani, wa siku hizi, na wanaochipuka muda wote.

Lakini, hii isiwe sababu ya kukata tamaa, bali changamoto ya kukufanya ujitahidi kuvuna kila uwezacho katika hazina hii isiyo na mwisho. Nami, tunapoingia katika mwaka mpya, nina viporo vya vitabu ambavyo nilianza kuvisoma na napangia kuendelea navyo katika huu mwaka mpya, na papo hapo, nina shauku kubwa ya kusoma vitabu vingi zaidi, kwa kuwa afya yangu inaendelea kuimarika.

No comments: