Mahojiano yangu na Jeff Msangi yalifanyika mwaka 2008, lakini naona yanastahili kujadiliwa hata leo na siku zijazo. Wadau wengi walichangia maoni yao ambayo unaweza kuyasoma hapa.
Mahojiano haya yamechapishwa pia katika kitabu changu cha Changamoto: Insha za Jamii.
.
-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
KWA KINA NA PROF.JOSEPH MBELE
Mbali na kuwa na utajiri wa asili wa aina yake,Tanzania ni nchi ambayo inajivunia kuwa na wasomi maarufu ambao wametapakaa kote ulimwenguni wakifundisha katika mashule na vyuo mbalimbali au kuongoza vitengo nyeti katika idara za kimataifa na zenye uzito wa ki-dunia nzima.
Mmojawapo miongoni mwa wasomi hao ni Prof.Joseph Mbele(pichani),mtanzania anayefundisha katika Chuo cha St.Olaf kilichopo Northfield jimboni Minnesotta nchini Marekani.Miongoni mwa wasomi na wafuatiliaji wa mambo mbalimbali ya kitaaluma jina la Prof.Mbele sio geni hata kidogo.Prof.Mbele ni mtunzi wa kitabu maarufu sana kiitwacho Africans and Americans:Embracing The Cultural Differences.Kitabu hicho ndicho kinachotumika zaidi hivi leo mashuleni na katika taasisi mbalimbali(zikiwemo balozi mbalimbali) wanapokuwa wanawaandaa watu wao kuja kusoma, kutembea tu,kufanya kazi au tafiti mbalimbali barani Afrika.
Kutokana na kwamba kumekuwepo na mijadala mingi sana kuhusiana na masuala yote yahusuyo mila,tamaduni,desturi,maisha ya ughaibuni nk,BC tuliamua kumtafuta Prof.Mbele ambaye ni msomi anayetambulika kimataifa na mwenye mamlaka ya kutosha kuhusiana na maeneo yaliyotajwa hapo juu ili kupata maoni na mitizamo yake.Katika mahojiano haya,Prof.Mbele anafafanua mambo mengi sana kama vile’je kuna kitu kama mila,tamaduni na desturi za kitanzania?Kwanini watu wengi hivi leo hususani vijana wanazidi kubobea kwenye tamaduni za kimarekani?Kwanini aliandika kitabu hicho kilichotajwa hapo juu? Kama wanajamii tunakubaliana kwamba tumepoteza dira na muelekeo katika tamaduni,mila na desturi zetu,nini kifanyike?Kwa majibu ya maswali hayo na mengineyo mengi,fuatana nasi katika mahojiano yafuatayo;
BC: Kumekuwepo na mijadala mbalimbali kuhusiana na suala la mila,tamaduni na desturi za mtanzania.Kuna ambao wanasema hakuna kitu kama mila,utamaduni na desturi za kitanzania ingawa wanakubali kwamba inawezekana kukawa na mila,tamaduni na desturi za makabila fulani fulani. Nini maoni yako kuhusu dhana kama hizi? Unadhani kuna mila,tamaduni na desturi zinazoweza kuitwa “za kitanzania”?
PROF.MBELE: Pamoja na tofauti zote baina ya makabila,kuna pia mambo ya msingi ambayo yamo miongoni mwetu sote. Mifano ni kama kuheshimu wazee, kupenda kuwa na watoto, kushirikiana kwenye shughuli kama mazishi na sherehe. Mambo hayo yamo miongoni mwa Waafrika kwa ujumla. Kuna mengine ambayo tunaweza kusema ni ya kiTanzania. Kwa mfano, Mtanzania ana utamaduni wa kutotilia maanani ukabila katika mahusiano na Watanzania wengine. Anazingatia utaifa kwanza. Huu ni utamaduni wa Mtanzania. Lugha ni nguzo muhimu ya utamaduni, na Mtanzania anathibitisha kuwepo kwa huu utamaduni wa kiTanzania kwa kuongea kiSwahili anapokuwa na Watanzania wa makabila mengine. Kwa kiasi kikubwa, hayo ni matokeo ya juhudi ya Mwalimu Nyerere.
BC: Vijana wengi wa hivi leo wanapenda(pengine hata kuabudu) tamaduni za kimarekani.Hii sio kwa vijana wa kitanzania peke yao bali dunia nzima.Unadhani hii inatokana na nini? Nini faida au madhara ya mapokeo haya ya tamaduni za kigeni au kimarekani?
PROF.MBELE: Hao watu wanaoiga namna hiyo wana matatizo.Tatizo moja ni kuwa wanayoiga ni yale yenye mushkeli hata huko Marekani kwenyewe. Marekani, kama sehemu yoyote duniani, ina watu wanaokiuka maadili ya jamii. Vijana wetu wanaiga mambo hayo yenye walakini, iwe ni katika mitindo, lugha, na kadhalika.
Kwa mfano,badala ya kujifunza kiIngereza sanifu, ambacho kingewawezesha kusonga mbele kielimu na kimaisha, vijana wetu wanaiga kiingereza kibovu na cha matusi ambacho wanakisikia kutoka kwa baadhi ya wanamuziki wa kiMarekani.Vijana wetu wanaiga mitindo ambayo hata huku Marekani inawabughudhi wengi. Kuna miji hapa Marekani imeshaanza kupiga marufuku aina ya mavazi wanayoiga hao vijana wetu.
Filamu nyingi za Hollywood zinawapotosha watu.Wanadhani mambo ya Hollywood ndio hali halisi ya Marekani. Hollywood kwa ujumla inapotosha ukweli wa Marekani, kama vile inavyopotosha ukweli kuhusu Arabuni, Afrika, Asia, na kwingineko.Hollywood au inatia chumvi au inadhalilisha. Hollywood inatafuta biashara, sio kuelimisha watu, na hata kama kinachouzwa ni pofotu, wao wanauza tu. Ukweli ni kuwa Wamarekani kwa
ujumla ni watu wenye heshima zao, kwa mujibu wa utamaduni wao, kama ilivyo katika nchi nyingine yoyote, na wanavaa na kutumia lugha ya kawaida na ya heshima kama vile wanavyofanya Watanzania walio wengi.
BC: Utamaduni wa “kimarekani” ambao kila kukicha unazidi kuenea dunia nzima sio jambo linalotokea kama ajali.Ni mipango madhubuti ya kiserikali ya Marekani katika kuhakikisha inaendelea kuwa “super power’ wa dunia. Je unakubaliana na dhana hii? Kama ndio,unadhani serikali za nchi kama yetu ya Tanzania ina wajibu gani katika sio tu kujaribu kukabiliana na hali hii bali pia kuhakikisha mila,tamaduni na desturi za kitanzania zinalindwa,kutunzwa na kuheshimiwa?
PROF.MBELE: Kinachoenea duniani kutoka Marekani ni utamaduni wa kibepari, ambao unageuza kila kitu kuwa bidhaa, kama alivyotueleza Karl Marx kwenye kitabu chake cha Communist Manifesto. Mabepari wanasambaza mitindo na vishawishi, ili kuwafanya watu wapende kununua bidhaa au huduma mbali mbali hata kama hazina maana katika maisha. Wao wanatafuta pesa. Wamarekani wa kawaida hawana uwezo wa kufanya hayo yote, wala hawahusiki.
Serikali ya Marekani ni mshiriki na pia wakala wa hao mabepari, na inachofanya ni kuweka mazingira ya kuuwezesha ubepari kustawi duniani kote.Serikali ya Marekani inazishinikiza nchi kama yetu ziweke mazingira muafaka ya kuuwezesha ubepari kufaidika, pamoja na kwamba wananchi walio wengi wanaathirika. Serikali ya nchi kama Tanzania ingepaswa kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala hayo, kama alivyokuwa anafanya Mwalimu Nyerere.
Lakini, leo tumekwama;viongozi wenyewe sidhani kama wana upeo unaohitajika,wala dhamira inayohitajika.Hakuna juhudi inayofanywa na serikali kuhimiza elimu kuhusu ubepari, badala yake kinachofanyika ni kuupigia debe ubepari na utamaduni wake. Hatutafika mbali, bali tutaanza kuona matatizo makubwa katika jamii yetu. Kujenga utamaduni wa kujifahamu,kujiamini, kujithamini, kujitegemea, na kujiheshimu kutatusaidia kuepuka kuwa jalala la kila kinachotoka kwa hao mabepari.
Cover la mbele la kitabu cha Prof.Mbele.
BC: Katika kitabu chako cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences( Tunashauri kila mtu akisome kitabu hiki) umeelezea kwa umakini kabisa tofauti za kimila,tamaduni na desturi kati ya waafrika na wamarekani.Nini hasa kiini cha wewe kuamua kuandika kitabu hiki? Kuna uzoefu wako binafsi wowote ule nyuma ya kitabu hiki?
PROF.MBELE: Katika kuishi na Wamarekani kwa miaka mingi, nilitambua umuhimu wa kitabu cha aina hii, ambacho kingetoa mwanga kuhusu utamaduni wao na namna unavyotofautiana na utamaduni wetu Waafrika. Lengo lilikuwa kuzuia au kupunguza mikwaruzano na kutoelewana baina ya Waafrika na Wamarekani, ambayo haikwepeki endapo hawachukui hatua za kuzifahamu tofauti zao. Mikwaruzano hii haiko baina ya Wamarekani na Waafrika tu, bali inaweza kutokea popote wanapokutana watu wa tamaduni tofauti, iwe ni katika ndoa, shuleni, kwenye biashara, diplomasia, utalii, na kadhalika.
Msukumo mkubwa wa kuandika hiki kitabu ulitoka kwa Wamarekani waliokuwa wanaenda Afrika, iwe ni kwa masomo, utafiti, kazi za kujitolea, au kwa safari tu,ambao
walikuwa wananiulizia masuali kuhusu maisha na utamaduni wa Waafrika.Lengo lao lilikuwa ni kujiandaa ili wakiwa Afrika wasipate taabu, na ili wasifanye makosa katika masuala ya mila na desturi. Pamoja na kuwaeleza ana kwa ana au kwa njia ya mawasiliano mengine, niliona niandike hiki kitabu.Nilijua kuwa Wamarekani kwa ujumla wanapenda kusoma vitabu, na hii ikawa ni njia bora ya kuwasiliana nao.
Kwa upande mwingine, nilikuwa nawawazia pia Waafrika.Wengi wanaoishi Marekani au wanashughulika na Wamarekani sehemu mbali mbali kule Afrika. Hao nao niliona watahijaji kujifunza mambo ya Wamarekani, ili iwe rahisi kuelewana nao.
Vinginevyo,nilijua kuwa watapata ugumu fulani, na hata migongano.Tatizo ni kuwa
Watanzania hawathamini vitabu kama Wamarekani wanavyothamini.Hilo limethibitishwa tena na tena.Kwa hivi, sina hakika kama lengo langu litafanikiwa kwa upande wa Watanzania.
Prof.Mbele(mwisho wa meza upande wa kulia) akiwaandaa wanafunzi wa Colorado College kwa ajili ya safari ya kimasomo Tanzania.
BC: Una mpango wowote wa kukitafsiri kitabu hiki katika lugha ya Kiswahili ili watu wengi zaidi waweze kukisoma? Kwa anayetaka kukisoma kitabu hiki hivi sasa,kinapatikana wapi au anaweza kukipata vipi?
PROF.MBELE: Itakuwa vizuri kukitafsiri kitabu hiki kwa kiSwahili na hata lugha zingine, kama vile kiSomali, kiArabu, na kiFaransa. Hapa Marekani, kuna maelfu ya waAfrika wanaotumia lugha zote hizi, na ninafahamu kuwa wanahitaji kuelewa mambo niliyoandka. Kitabu hiki kinapatikana kwenye tovuti hii http://www.lulu.com/content/105001. Ninataka kitabu hiki kipatikane Tanzania kiurahisi, kiwasaidie Watanzania wanaoshughulika na Wamarekani kwa namna yoyote. Kwa sasa, kinapatikana Dar es Salaam,simu namba 717 413 073.
BC: Ubaguzi wa rangi ni jambo ambalo hukatisha watu wengi tamaa. Kwa maoni yako nini hasa chanzo cha ubaguzi wa rangi duniani? Je wewe katika kazi zako za kila siku za ufundishaji nchini Marekani unakumbana na matatizo unayohisi ni matokeo ya moja kwa moja ya ubaguzi wa rangi? Unakabiliana nayo vipi na unatoa ushauri gani kwa watu wengine wanaokabiliwa na tatizo kama hilo?Je unadhani ubaguzi wa rangi’ ni sehemu ya utamaduni au ni tabia tu za watu?
PROF.MBELE: Sio vizuri kukata tamaa, na huenda hata wale wanaolalamikia ubaguzi nao ni wabaguzi. Kuna aina nyingi za ubaguzi, kama vile ubaguzi wa dini, jinsia,taifa, lugha, kabila, rangi, umri, uwezo wa kiuchumi, na kadhalika. Hata mahali penye watu wa rangi moja tu, ubaguzi unaweza kuwepo na kuleta matatizo makubwa, kama yale ya Rwanda mwaka 1994. Ubaguzi ni ubaguzi. Pamoja na kwamba ni muhimu kutambua ubaya uliopo katika jamii za wengine,ni muhimu pia kuona ubaya uliomo katika jamii zetu au katika nafsi zetu.
Jamii ya Tanzania, kwa mfano, ina maovu mengi. Wakati mamilioni ya watu wanaishi kwa dhiki kubwa, kuna Watanzania ambao wanafuja mali ya nchi kwa starehe na mambo yao binafsi. Na wanaiba hata hela za umma na kuzifuja. Kuna maelfu ya watoto yatima katika nchi yetu ambao wana dhiki kubwa, wakati mamilioni ya shilingi yanafujwa kila siku.
Nikirudi kwenye suala la ubaguzi wa rangi, napenda kusema kuwa,badala ya mtu kukaa na imani kuwa hutaendelea sababu ya ubaguzi wa rangi, ni bora kutambua kuwa ukiwa na elimu, maarifa na ujuzi, utahitajika, na hakuna atakayeweza kukupuuzia eti kwa sababu ya rangi yako. Dunia ya leo ni dunia ya aina yake, inategemea elimu, maarifa, na ujuzi. Makampuni na mashirika yanashindana, na yanalazimika kutafuta watu wenye ujuzi, elimu, na maarifa. Kama wewe ndio bingwa, utatafutwa wewe.Yule tajiri maarufu duniani, Bill Gates, amewekeza India, kwa sababu Wahindi wanawika kwenye fani ya kompyuta. Anawajali Wahindi kwa hilo, na wala rangi yao sio kipingamizi. Watanzania tutambue hilo. Tujifunze kutoka kwa Wahindi; tujibidishe katika elimu.
Mimi nimekuwa na msimamo huo tangu zamani. Nimelenga katika kujielimisha muda wote. Mfano mmoja wa matokeo yake ni kuwa kutokana na ujuzi wangu katika fani yangu, nilifuatwa na chuo cha St. Olaf cha Marekani nije kuwafundishia masomo fulani. Sikuomba kazi hapa. Shughuli zimeenda vizuri kwa miaka yote niliyofundisha hapa, wala sijaona usumbufu wala ubaguzi wowote. Kama ni usumbufu au kukosewa haki sehemu ya kazi, hayo yalinisibu kule Tanzania. Nimejibidisha sana pia katika utafiti wa tamaduni mbali mbali, na matokeo yake ni kuwa ninatafutwa na hao Wamarekani wanapohitaji ushauri kwenye masuala hayo.
Jambo jingine ambalo naona ni muhimu kusema ni kuwa kama kweli kuna kipingamizi kama hiki cha ubaguzi, basi tukumbuke kuwa sio lazima tuwe watu wa kuajiriwa na wengine. Kama tunao ujuzi na maarifa, tutafakari namna ya kujiajiri. Hilo wazo limenijia miaka hii ya karibuni, na niko katika kulifanyia kazi. Ujuzi na maarifa ndio msingi na ndio silaha thabiti katika mapambano ya ulimwengu wa leo.
BC: Nadhani tunakubaliana kwamba suala la udumishaji wa mila,tamaduni na desturi lina misingi yake katika malezi. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.Mporomoko wa maadili uliozikumba jamii zetu hivi leo inasemekana unatokana na malezi mabovu.Unasemaje kuhusu suala hili na unatoa ushauri gani kwa wazazi kuhusiana na suala zima la malezi?
PROF.MBELE: Ni kweli kuna mporomoko mkubwa wa maadili. Wazazi na watu wazima kwa ujumla wana wajibu wa kuwa mfano wa maadili bora. Lakini hali iliyopo katika nchi yetu, kwa mfano, hairidhishi. Mwalimu Nyerere alijitahidi sana kuongelea maadili, kuanzia kufanya kazi kwa bidii, kuwatetea wanyonge, kufuata haki, kujielimisha, kuheshimiana.
Leo hii watu wanatafuta pesa kwa namna yoyote, na maadili yamewekwa kando. Kiu ya pesa imeleta madhara ya kila aina, kama walivyoelezea akina Karl Marx. Imevuruga maadili ya dini, serikali, elimu, na kadhalika. Utapeli umeingia sehemu nyingi za maisha ya jamii.Naamini kuwa tunaweza kujirekebisha. Kwa upande wetu Tanzania, kitu kimoja tunachoweza kufanya ni kuanza kujielimisha kuhusu yale aliyokuwa anatufundisha Mwalimu Nyerere, kwani yanaendana na mazingira ya kihistoria na utamaduni wetu.
Elimu ni jambo la msingi. Kwa mfano, tungejielimisha kuhusu masuala ya afya, tungepunguza utumiaji wa pombe. Lakini Tanzania tunaona sifa kunywa pombe sana, badala ya kutambua kuwa tunahujumu akili, afya, na maisha yetu. Watoto wanakua katika mazingira ambayo hayawafundishi maadili mema. Hata kama shuleni watafundishwa, huko mitaani wanaona na kusikia mengine. Kwa mila za mababu na mabibi, watu wazima wanawajibika kuwaongoza na kuwanyoosha wadogo, lakini kwetu mambo ni kinyume. Watu wazima wanawakwaza na kuwapotosha wadogo.
Niliwahi kuhudhuria tamasha la vitabu pale Dar es Salaam. Watoto walikuwa hapo lakini watu wazima wachache sana walioonekana hapo. Watoto waliimba nyimbo, wakiwaomba wazazi wawanunulie vitabu na wawe na utaratibu wa kusoma majumbani. Lakini wazazi wenyewe hawakuwepo hapo kwenye tamasha. Ilikuwa hali ya kusikitisha. Jioni, nilipokuwa napita mitaa mbali mbali, nikirudi nyumbani, nilikuwa nawaona watu wazima kwenye baa, mtaa hadi mtaa, kama kawaida. Badala ya kujumuika na watoto kwenye tamasha la vitabu, wao walikuwa kwenye baa. Na hata viongozi hawakuwepo kwenye tamasha: wajumbe wa nyumba kumi, makatibu kata, makatibu tarafa, wabunge, na kadhalika. Hawakuwepo.Huwezi kuamini kuwa hii ndio nchi ya Mwalimu Nyerere.
Mimi kama mwalimu lazima niwaambie Watanzania kuwa hapo Wamarekani wametuzidi: wanahudhuria sana matamasha ya vitabu, na kwenye maduka ya vitabu utawakuta wakinunua vitabu. Kama nilivyosema, dunia ya leo inatawaliwa na elimu, maarifa na ujuzi, na malezi bora ya watoto lazima yazingatie hilo.
Prof.Mbele(kulia) akiongea na walimu na watoto jijini Dar-es-salaam.
BC: Hivi leo kila mtu anaongelea kuporomoka kwa maadili ya kijamii hususani miongoni mwa vijana. Kwa uzoefu na utaalamu wako, ni mila,tamaduni na desturi zipi ambazo hivi leo tumeachana nazo ambazo sio tu hatukutakiwa kamwe kuachana nazo bali tulitakiwa kuzienzi kwa udi na uvumba? Nini kinaweza fanyika hivi sasa ili kurejesha suala zima la maadilli.
PROF.MBELE: Kama nilivyogusia, ingebidi tuanze kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere, ambaye alithamini utu. Leo hii mtu anayeheshimiwa ni yule mwenye pesa. Hili ni tatizo kubwa,na dalili ya kuporomoka maadili. Jamii kwa ujumla imeingia katika hali hiyo, na vijana wanalelewa namna hiyo. Ndoto zao ni za kupata pesa nyingi, kwa njia yoyote. Lakini watu wazima ndio wameanzisha mkondo huu, na hao vijana wanafuata nyayo.
Alichojaribu kujenga Mwalimu Nyerere katika jamii yetu ni ule moyo wa kila mtu kumjali mwingine na kuangalia maslahi ya jamii, si maslahi binafsi. Na Mwalimu Nyerere alikuwa anajenga fikra zake kwenye msingi wa mila na desturi za mababu na mabibi zetu. Leo tumeachana na mwelekeo huo. Na hili ni tatizo kubwa. Naamini kuwa tukijizatiti upya na kuanza kuangalia yale aliyokuwa anafundisha Mwalimu Nyerere, tuyaingize mashuleni, sehemu za kazi, mitaani, na kila mahali, tutaweza kuanzisha mkondo ule alioutaka Mwalimu Nyerere.
BC: Dunia yetu hivi leo inakabiliwa na suala gumu la vita dhidi ya ugaidi. Unaweza kuhusisha vipi ugaidi na mila,tamaduni na desturi za binadamu au mataifa mbalimbali?
PROF.MBELE: Kitu kigumu ni kuelewa dhana ya ugaidi na kukubaliana kama wote tunaelewa hivyo hivyo. Kwa bahati mbaya, dhana hii inatafsiriwa namna mbali mbali na watu au jamii mbali mbali. Matokeo yake ni kuwa wako ambao wanasema wanapiga vita ugaidi hali kwa mtazamo wangu wao wenyewe ni magaidi. Mara nyingi nashangaa, na sijui kama kinachopigwa vita ni ugaidi au ni kitu kingine. Halafu serikali nyingi sasa zimepata fursa ya kufanya dhuluma kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Kwa maneno mengine hii inayoitwa vita dhidi ya ugaidi ina mikanganyiko ya kila aina.
BC: Mwisho una ujumbe gani kwa vijana,wanajamii,viongozi wa kiserikali,dini nk kuhusu mila,tamaduni na desturi?
PROF.MBELE: Ujumbe wangu ni kuwa Watanzania tujifunze na kuzingatia aliyotufundisha Mwalimu Nyerere: kujenga jamii yenye haki, yenye kuzingatia usawa wa binadamu, isiyo na unyonyaji na ukandamizaji, yenye kushirikiana na kuhemishimiana. Huu ndio utamaduni unaotufaa. Tuzingatie aliyotufundisha Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Alisema elimu haina mwisho, na aliongelea elimu kwa mapana na undani, kuanzia kisomo chenye manufaa, elimu ya watu wazima, na elimu mashuleni hadi vyuo vikuu.
Elimu ndio msingi wa mafanikio katika ulimwengu huu wa ushindani mkubwa. Msisimko wa elimu aliouwazia Mwalimu Nyerere umedidimia. Asilimia ya watu wasiojua kusoma na kuandika inazidi kuongezeka. Mashuleni watu wanatafuta vyeti, badala ya elimu. Watu wanatumia muda mwingi vijiweni, badala ya kujitafutia maarifa na elimu.
Tulipopata uhuru, Nyerere alieneza ujumbe maarufu: Uhuru na Kazi! Leo utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii umetetereka. Hata hao Wamarekani tunaowasema, wengi wako katika nchi yetu, kuanzia vijijini hadi mijini, wakifanya kazi za kujitolea, wakati sisi wenyewe tuko vijiweni tunapiga soga, tuko kwenye sherehe au tuko kwenye maandalizi ya sherehe.Hata hivyo, bado fursa tunayo ya kujirudi.
BC: Shukrani sana Prof.Mbele kwa mahojiano haya.Tunakutakia kila la kheri
katika kazi zako.
PROF.MBELE: Nashukuru sana kwa fursa hii ya kujieleza kwa wadau wa ukumbi huu. Nawe nakutakia kila la heri.
Prof.Mbele pia ni Mwanzilishi na Mkurugenzi wa shirika lijulikanalo kama AFRICONEXION. Unaweza kutembelea tovuti ya shirika hilo kwa kubonyeza hapa.
Je unakubaliana au unapingana na chochote alichokisema Prof Mbele?Usisite kuweka maoni yako na pia kumpelekea link ndugu,jamaa au rafiki yako ili naye apate soma ulichokisoma.Asante.
No comments:
Post a Comment