Thursday, January 8, 2015

""Till I End My Song:" Tungo za Mwisho za Washairi Maarufu

Kila siku ninapokuwa chuoni St. Olaf, ambapo nafundisha, sikosi kupita katika duka la vitabu. Mbali ya vitabu vilivyomo dukani, wanaweka pia vitabu vingi kwenye meza na makabati nje ya duka. Hapo nje unaweza kuvipata vitabu kwa bei nafuu kuliko kuviagiza wewe mwenyewe sehemu nyingine.

Basi, siku moja, katika kuangalia angalia vitabu hapo nje, nilikiona kitabu ambacho rangi za jaladaa lake zilinivutia. Nilivutiwa zaidi nilipoona kimehaririwa na Harold Bloom, na kinauzwa kwa  dola 4.98, ambalo ni punguzo kubwa, kwani bei yake ya halisi ni dola 24.99. Hapo hapo niliamua kukinunua, ingawa nilikuwa na hela kidogo tu, kwani ilikuwa ni mara tu baada ya Krismasi, huku tungiingojea siku kuu ya Mwaka Mpya.

Harold Bloom ni bingwa mojawapo duniani katika masomo ya ki-Ingereza na fasihi yake, sio tu kwa upande wa uchambuzi wa maandishi bali pia upande wa nadharia ya fasihi. Ameandika au kuhariri vitabu vingi. Nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu Cha Wisconsin-Madison, 1980-86, tulisoma baadhi ya maandishi ya Harold Bloom, sambamba na maandishi ya watalaam wengine, kama vile M.H. Abrams, Jacques Derrida, Edward Said, Wayne Booth, Michael Raffartere, Terry Eagleton, na Fredrick Jameson. Ninavyo baadhi ya vitabu vya wataalam hao, na nimehudhuria mihadhara ya Edward Said, Wayne Booth, na M.H. Abrams.

Nilivyoona hiki kitabu kipya, Till I End My Song, chenye jina la Harold Bloom, sikuweza kujizuia kukinunua. Nilivyoona kitabu kimeelezwa kama "A Gathering of Last Poems" nilipata shauku ya kukiangalia zaidi, hata kabla ya kukinunua. Nilihisi kuwa ni mkusanyiko wa mashairi ya waandishi maarufu, ambayo yalikuwa ni mashairi yao ya mwisho au ya mwisho mwisho kabla hawajafariki. Hapo dukuduku na shauku vikanielemea. Nilivutiwa, kwani sikuwahi kusikia kuhusu kitabu kilichojaribu kufanya hivyo katika lugha yoyote.

Dukuduku yangu ilikuwa kubwa: je, tungo za mwisho kabisa za washairi maarufu kama Shakespeare, Christopher Marlowe, Milton, Geradd Manley Hopkins, Wallace Stevens, na Robert Lowell, zilikuwaje? Walisema nini? Walituachia usia gani? Nilikuwa nimesoma mashairi mengi ya watunzi hao, lakini sikuwahi kuwazia dhana hii ya mkusanyiko wa mashairi yao ya "lala salama," kama wasemavyo wa-Swahili.

Harold Bloom anafafanua, katika sentensi za mwanzo kabisa za utangulizi wake, maana ya "last poems," dhana iliyomwongoza katika kuandaa kitabu hiki. Nanukuu:

There are three kinds of "last poems" in this anthology. Some literally are the final poems these women and men composed. Others were intended to mark the end, though the poet survived a while longer and continued to work. A third group consists of poems that seem to me an imaginative conclusion to a poetic career. With all three kinds I have made an aesthetic judgement: everything in this volume is here because of its artistic excellence.

Kwa jinsi kitabu hiki kilivyokusanya tungo za washairi mashuhuri sana, wa tangu zamani hadi leo, ni hazina kubwa kwa yeyote anayependa kuuelewa urithi wa uandishi katika lugha ya ki-Ingereza.

No comments: