Sunday, January 25, 2015

Mipango ya Ziara Yangu Mankato Inaendelea

Kama nilivyoandika katika blogu hii, nitakwenda kuongea na wanafunzi wa chuo cha South Central mjini Mankato. Mipango ya ziara hii, ambayo itafanyika tarehe 24 Februari, inaendelea vizuri.

Mwenyeji wangu, mwalimu Rebecca Fjelland Davis, amenieleza kuwa shughuli ya kwanza nitakayofanya siku hiyo ni kuongea na wanafunzi katika darasa lake, kuanzia saa nne hadi saa tano na dakika hamsini asubuhi. Hao ni wanafunzi wanaojiandaa kwa safari ya kimasomo Afrika Kusini. Kama sehemu ya maandalizi hayo, wanasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na maongezi yangu nao yatahusu yale niliyoandika kitabuni.

Baada ya darasa hilo, kuanzia yapata saa sita, nitatoa mhadhara kwa wanachuo na wana jamii. Mwalimu Fjelland Davis ameniarifu kuwa duka la vitabu la hapo chuoni litakuwa limeandaa nakala za kitabu changu, kwa ajili ya kuuza. Kama ilivyo desturi hapa Marekani, nategemea kuwa baada ya mazungumzo nitasaini nakala za vitabu.

Hii sio mara yangu ya kwanza kufanya shughuli mjini Mankato. Nimewahi kwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Mankato kwa wanachuo waliokuwa wanajiandaa kwenda Afrika Kusini. Nilialikwa na Profesa Scott Fee, ambaye ni muasisi na mratibu wa mpango wa ushirikiano baina ya chuo kikuu cha Mankato na chuo kiitwacho Eden Campus cha Afrika Kusini. Nakumbuka ukumbi ulivyojaa watu siku hiyo, nami kwa kutekeleza ombi la Profesa Fee, niliwasilisha nakala yapata 40 za Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Nimewahi pia kushiriki maonesho ya Deep Valley Book Festival, na mengine yaliyofanyika katika uwanja wa maonesho ya magari, ambao jina lake nimesahau. Ningekuwa na blogu miaka ile, ningekuwa nimeandika taarifa. Siku nyingine nilialikwa Mankato na taasisi inayoshughulika na huduma kwa jamii, nikaongea na wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi mbali mbali, kama vile Somalia, Ethiopia, na Sudani. Mazungumzo hayo yaliripotiwa katika gazeti la Mankato Free Press.

Nikirudi kwenye mwaliko wa tarehe 24 Februari, napenda kusema kuwa Mwalimu Fjelland Davis na Profesa Scott Fee wanashirikiana katika mpango wa kupeleka wanafunzi Afrika Kusini. Wote wawili walihusika katika mhadhara niliotoa kwa wanafunzi wao ambao taarifa yake iliandikwa hapa na hapa.

No comments: