Tuesday, February 26, 2013

Mhadhara Wangu Leo Umekuwa Mzuri

Mhadhara wangu leo katika chuo cha South Central umekwenda vizuri sana. Nilijua hali ingekuwa hivyo, kwani nilikuwa naongelea masuala ambayo nina uzoefu nayo kwa miaka mingi.

Niliongea na wanafunzi wakiwa mbele yangu na wengine wakiwa mji wa Mankato ila tunaonana nao kwenye skrini ya televisheni. Walimu wao walijigawa sehemu hizo mbili.

Mhadhara ulikuwa juu ya kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho maprofesa waliwaelekeza wanafunzi wakisome kabla ya mhadhara wangu.

Niliibua masuala mengi, kwa muhtasari, nikianzia na uzoefu wangu kama mshauri wa programu zinazopeleka wanafunzi na watu wengine Afrika. Nilielezea nilivyoandika kitabu hiki, na changamoto zake. Hatimaye, nilitoa nasaha kuhusu mambo ya msingi ya kukumbuka tunapokutana watu wa tamaduni mbali mbali.

Kipindi cha masuali na majibu kilifana sana. Nilifurahi kuona jinsi wanafunzi na maprofesa walivyokuwa wanakinukuu kitabu, hata kunikumbusha vipengele ambavyo sikuvikumbuka.

Mwishoni kabisa mwa muda wetu wa saa moja na nusu, wanafunzi walinipa nakala zao za kitabu changu kwa ajili ya kusaini. Huo ni utaratibu au utamaduni hapa Marekani.

Wakati wa kuagana, niliombwa nije siku nyingine. Darasa lao linaongelea mambo ya Afrika Kusini, na pendekezo ni kuwa nikajumuike nao wakati watakapokuwa wanajadili kitabu cha J.M. Coetzee kiitwacho Disgrace.

4 comments:

PBF Rungwe Pilot Project said...

Hongera sana Profesa kwa mhadhara huo mzuri wa kuelimisha wenzetu kuhusu mambo ya tamaduni

Goodman Manyanya Phiri said...

Hizi ni habari za kusisimua daima,Prof! BIG UP,MAN!

Mbele said...

Kwa kweli, mambo yalienda vizuri sana, kwa maana kwamba watu walifaidika na kufurahi kabisa, nami namshukuru Mungu kwa kunipa uwezo.

Kwa kutambua kuwa uwezo hutoka kwa Mungu, na Mungu ana malengo yake, ninapopata majukumu kama hayo huwa sichezei. Kuwajibika ipasavyo ni namna ya kumwenzi Mungu.

Shukrani za pekee ziwafikie nyinyi wadau, ambao mnanihamasisha.

Mbele said...

Kwenye Facebook, Profesa Becky Davis aliweka photo na ujumbe kuhusu mhadhara wangu. Angalia hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...