Tuesday, February 12, 2013

Wanafunzi Wangu Wameipenda Tanzania

Kuanzia tarehe 3 hadi 28 Januari, nilikuwa Tanzania na wanafunzi 29 wa Chuo cha St. Olaf, kwenye kozi juu ya mwandishi maarufu Ernest Hemingway.

Niliitunga kozi hii kwa makusudi, ili kuwapa wanafunzi fursa ya kuyaelewa mambo ya mwandishi huyu ambayo hayajulikani sana au hayajulikani vizuri, hata miongoni mwa wasomi.

Tulisafiri katika maeneo kadhaa nchini Tanzania, ambamo Hemingway alipita mwaka 1933-34, tukiwa tunasoma maandishi yake kuhusu sehemu hizo. Wanafunzi walipata fursa tele ya kukutana na wa-Tanzania, kuanzia watoto wadogo hadi wazee.

Walipata fursa ya kukutana na wa-Tanzania wa dini mbali mbali. Walipata fursa ya kuona maisha ya mijini na vijiji. Walipata ufahamu mpana na wa kina kuhusu maandishi na falsafa ya Hemingway.


Kitu kimoja muhimu ni jinsi wanafunzi wote walivyopendezwa na hali waliyoiona Tanzania, hali ya ukarimu mkubwa kila walipopita. Walishangaa kuona kuwa wa-Tanzania wanajisikia raha kabisa kuwakaribisha wageni. Wamefurahi sana kupata fursa ya kuifahamu Tanzania. Wanaipenda kiasi kwamba walisononeka siku walipoondoka kurejea Marekani.

Katika picha ya juu, anaonekana mwanafunzi mmojawapo akiwa ameshika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Cultural Differences, ambacho wanafunzi walikitumia katika maandalizi ya safari yao. Katika picha ya chini tunaonekana mjini Karatu, tukiwa na mwanasheria Alex Shilla, ambaye ameshika kitabu hicho hicho, na amekuwa mdau na mpiga debe wake. Wanaonekana pia akina mama wawili ambao ni mahakimu mjini Karatu.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...