Saturday, February 16, 2013

Mdau Niliyemkuta Katika Ndege

Tarehe 3 Januari, katika mazingira ya aina yake, nilimkuta mdau wa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilipanda ndege Minneapolis, kwa safari ya Amsterdam, kisha Tanzania. Baada ya kuketi kitini, akina mama waliokaa karibu yangu waliniomba iwapo inawezekana kubadilishana viti, ili rafiki yao aje akae pale nilipokaa. Nilikubali kwa roho moja, nikaenda kukaa ile sehemu nyingine.

 Baada ya kuketi tu, tulisalimiana na dada aliyekuwa amekaa kiti cha pembeni yangu. Naye, katika kuitikia, aliniangalia mara moja tu akasema, "wewe uliandika kitabu." Nilihisi alimaanisha kitabu cha Africans and Americans, kwani nyuma kuna picha yangu. Hapo alichukua kibegi chake kilichokuwa chini ya kiti, akafungua na kunitolea nakala ya kitabu hicho. Ilikuwa ni ajabu kukutana na mdau katika mazingira ya aina hiyo. Lakini hii si mara ya kwanza, kama nilivyoelezea hapa.






Mdau huyu aliniambia kuwa yuko katika ndege ile na wenzake kadhaa ambao wanaenda Kenya kwa shughuli ya kujitolea, chini ya shirika la Medical Missions Worldwide. Aliendelea kuniambia kuwa rafiki yake wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-River Falls ndiye alimwambia asome kitabu hicho. Hapo nilikumbuka kwamba miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na kikundi kutoka chuo kile ambacho kilifika chuoni kwangu kuongea nami, kama sehemu ya matayarisho ya safari ya Uganda. Tuliongelea yale niliyoandika katika kitabu hiki, nikasaini nakala zao.

Basi tuliongea sana na huyu mdau mpya katika safari yetu ya kuelekea Amsterdam, ambapo tuliachana, wao wakielekea Nairobi, nami nikielekea Arusha.

(Picha zilipigwa na John A. Williams II, mkurugenzi mtendaji wa Medical Missions World Wide)

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...