Jambo la msingi ninalopangia ni kuendelea kufanya bidii katika kazi ambayo naamini Mungu mwenyewe alinipangia, kazi ya ualimu. Kazi hii inajumlisha mambo kadhaa hasa kujielimisha na kuwa tayari muda wote kuwapa wengine yale ninayoyajua. Elimu yangu si yangu pekee, bali ni dhamana kwa manufaa ya wanadamu.
Nitaendelea kusoma vitabu na makala za kitaaluma kwa bidii. Hii ni njia muhimu ya kujielimisha, ili niweze kufundisha kwa ufanisi zaidi.
Nitaendelea kutoa ushauri kwa jumuia na taasisi yoyote au kwa watu binafsi. Hii sio tu kwa faida yao, bali kwa faida yangu, kwani kwa kufanya hivyo ninapata fursa ya kupima ni kiasi gani ninafahamu jambo fulani.
Nitaendelea kufanya utafiti na kuandika. Kuandika ni aina ya ufundishaji. Mwalimu wa kiwango cha chuo kikuu ana wajibu wa kufanya utafiti na kuandika, ili kuchangia taaluma. Nitafanya bidii zaidi katika nyanja hizi.
Jambo moja la msingi ni kuwa nitachapisha vitabu vyangu Tanzania, kwa gharama yangu, ili kuchangia elimu, ingawa ninajua kuwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu kwa ujumla ni hafifu sana.
Nashukuru kuwa mwaka jana nimeweza kusoma vitabu vilivyoelezea vizuri masuala muhimu ya maisha na mafanikio. Jambo moja ambalo limesisitizwa katika vitabu hivyo ni kuwa kama mtu huna mafanikio maishani, kosa ni lako mwenyewe. Usitafute mchawi wala visingizio. Jirekebishe wewe mwenyewe.
Jambo jingine ni kuwa usipoteze muda wako na watu ambao kazi yao ni kujaribu kukusema vibaya au kukukatisha tamaa. Hao ni watu wasio na maana katika maendeleo yako. Usiyumbishwe na watu wa aina hiyo, wala usiwatilie maanani. Zingatia malengo yako. Shirikiana na watu wenye mwelekeo wa maendeleo na mafanikio.
Msingi wa yote hayo ni kumweka mbele Mwenyezi Mungu, mwezeshaji wa yote. Pia kuendelea kuwa sambamba na familia, ndugu na jamaa, na mtandao wa marafiki na wengine wote wenye mapenzi mema.
2 comments:
Maazimio yako ni elimu tosha mzee Mbele .
Ndugu Mfuko,
Shukrani kwa kupita tena hapa kwenye blogu yangu na kuweka ujumbe. Nakukumbuka vizuri, tangu tulipowasiliana hivi majuzi kuhusu kitabu.
Napenda tu kusema jitahidi kutafuta vitabu hivi na kuvisoma. Mimi vinaniletea faraja na furaha kubwa maishani, wala sihitaji hata kwenda baa kupata mbili tatu za baridi kama zamani. Vitabu vinanitosha, na papo hapo vinatajirisha akili yangu.
Kila la heri.
Post a Comment