Monday, May 18, 2015

Kitabu cha Dr. John C. Sivalon, M.M.

Leo nimejipatia kitabu cha Dr. John C. Sivalon, M.M. Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985. kilichochapishwa na shirika la Kanisa Katoliki la wa-Benediktini, Ndanda. Kutokana na kutopatikana madukani hapa Marekani, nimekipata kupitia maktaba ya hapa Chuoni St. Olaf, kwa utaratibu wa uazimishanaji wa vitabu baina ya maktaba. Nimejitengenezea nakala kwa matumizi yangu, kama inavyoruhusiwa kisheria.

Hiki ni kitabu kinachojulikana Tanzania kwa kuwa kinatajwatajwa sana na viongozi wa wa-Islam wanaosema kwamba wa-Islam wamekuwa wakihujumiwa na bado wanahujumiwa na serikali ya Tanzania kwa manufaa ya kanisa na wa-Kristu.

Kutokana na madai hayo, kwa miaka yote hii nimekuwa na hamu ya kujisomea kitabu hiki. Sikuwahi kusema lolote juu yake, kwa vile sikuwa nimekisoma. Baada ya kukipata, kama saa mbili tu zilizopita, nimekipitia chote, ila bado sijakisoma kwa makini.

Hata hivi, nimeona kuwa mwandishi ameandika kitabu hiki kwa busara bila ushabiki, nikakumbuka kitabu cha Hamza Njozi, Mauaji ya Mwembechai, ambacho nacho amekiandika kwa busara bila ushabiki. Nimeangalia mtandaoni nikaona kuwa Dr. Sivalon ameandika pia kitabu kingine, God's Mission and Postmodern Culture: The Gift of Uncertainty. Hiki itakuwa rahisi kukinunua hapa Marekani.

Napenda kusema kila mmoja wetu ajisomee mwenyewe kitabu hiki cha Dr. Sivalon cha Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985, ayatafakari yaliyomo. Kwa kuzingatia kuwa bado sijakisoma kwa umakini, napenda kutoa fursa kwa yeyote ambaye amekisoma aweze kutuletea maoni yake. Nami, baada ya kukisoma ipasavyo, nitatoa maoni yangu.

9 comments:

Anonymous said...

Umefanya jambo jema sana kutafuta kitabu hicho na kujisome, binafsi sijapata nafasi ya kusoma vitabu vyote, hivyo siwezi kuzungumzia ukweli au uongo wa hoja zinazozungumziwa. Ila tu ninachoshindwa kuelewa ni kwanini malalamiko yaelekezwe kwa waumini wa wakawaida ambao hata sio walei?, Kwanini serekali imekuwa kimya sana zinapozungumzwa hizi hoja kwanye mikutano ya hadhara?.
Nadhani kuna nia nyingine iliyofichika chini ya haya malalamiko na wala sio hizi hoja.
Maana ikiwa leo nitabadili imani yangu ya dini, basi nami nitaanza kuwa malalamikaji wa kukandamizwa toka uhuru?, na pia nitaanza kuwalaiumu ndugu zangu niliozaliwa nao pamoja kwa kunikandamiza toka tupate uhuru.
Profesa kama utaweza kupata majibu ya hizi hoja katika hivyo vitabu nakutakia kila la heri.
Hongera kwa kwa kulivalia hili njuga hili swala.

Mbele said...

Ndugu Anonymous uliyeandika May 18, 2015 at 8:41, shukrani kwa ujumbe wako. Naona umeibua masuala muhimu na umeuliza masuali ya msingi.

Labda tusubiri kidogo, huenda wakajitokeza wadau wakaleta hoja, kama nilivyoomba.

Kwa upande wangu, ingawa nimesema nimekipitiapitia tu hiki kitabu, ukweli ni kuwa nimepata picha nzuri ya nini mwandishi ameandika. Nimegundua, kama nilivyosema, kwamba ameandika kwa busara, bila ushabiki. Ameonyesha utata wa masuala anayoyajadili, wala hajatoa nafasi ya tafsiri za kimkato kama zile nilizowahi kuzisikia.

Nimemhimiza kila mtu ajisomee mwenyewe, na ninapenda kukumbushia tahadhari aliyoitoa mwandishi Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria kuhusu "The Dangers of a Single Story."

PBF Rungwe Pilot Project said...

Nashukuru Profesa kwa kutupa habari hizo njema. Nitafanya kila jitihada kukipata kitabu hicho ambacho kama sitakosea amekiandika Dkt. Sivalon ambaye amenifundisha kama Mhadhiri Chuo Kikuu Cha Dar-Es-Salaam, na hivyo naelewa jinsi alivyo mahiri katika kujenga hoja na uchambuzi yakinifu kwa masuala ya kijamii kwa kutumia ndharia mbalimbali za Kisosolojia.

Mbele said...

Ndugu PBF Rungwe Pilot Project,
Shukrani kwa ujumbe wako. Nimeona kuwa ni huyu huyu unayemtaja. Nimeona kuwa alisomea shahada ya M.A. pale Chuo Kikuu Dar, wakati nilipokuwa mhadhiri katika idara ya Literature.
Pamoja na kuhitimu shahada ya uzamifu (Ph.D.) ameandika makala za kitaaluma na vitabu,na anafundisha katika chuo kikuu cha Scranton, ambacho ni cha shirika la Kikatoliki liitwalo Jesuit. Sisi wa-Katoliki, pamoja na historia ya Kanisa letu ya kuzingatia sana elimu, tuna historia ya kuwaona wa-Jesuiti kuwa ndio wakali waliobobea katika elimu kutuzidi hata sisi wengine. Ni imani tuliyo nayo, kama nilivyojionea wakati nasome seminari, na tunawaogopa ma-Jesuiti kuwa ndio wabobezi wakubwa katika elimu.
Mimi mwenyewe niliwahi kufundishwa na mabruda wa ki-Jesuiti kutoka Canada, wakati nasoma seminari (sekondari) ya Likonde. Kweli hao si mchezo.
Baada ya hiyo taarifa, ngoja nirudi kwenye mada. Nahimiza kuwa watu tuwe tunajisomea wenyewe, badala ya kutegemea kusimuliwa.
Katika siasa, kwa mfano, kama watu wangekuwa wanasoma "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na kadhalika, hawangerubuniwa na propaganda kwamba CCM ni chama cha Mapinduzi, wakati ni chama kinachohujumu Mapinduzi.
Mfano wa pili ni pale watu walivyoandamana kupinga kitabu cha Salman Rushdie cha Satanic Verses, ambacho hata hakikuwa kimeingia Tanzania, na hata kama kingekuwepo, hawangekisoma, kutokana na utamaduni wa Tanzania wa kutosoma vitabu, na hata kama wangejaribu, hawangekielewa, kutokana na kuwa kimeandikwa kwa ki-Ingereza na mtindo usio rahisi, kama nilivyoelezea katika blogu hii.
Kitabu cha Dr. Sivalon, kwa vile kimeandikwa kwa ki-Swahili, ingetakiwa kila mtu akisome mwenyewe, sio kusikiliza tu tafsiri za wengine. Na iwe hivyo kwa kila kitabu.

Yusufu Mmary said...

Prof Tunasubiri Maoni na mchango wako kuhusu hicho kitabu!

Mbele said...

Ndugu Yusuf Mmary

Shukrani kwa ujumbe wako. Mimi binafsi nilifanya juhudi kukitafuta kitabu hiki ili niwe nacho, niweze kukisoma, kila ninapohitaji. Nimekisoma kama nilivyosema, ila ninataka nikisome kwa makini zaidi. Sina haraka nacho. Ninasoma vitabu muda wote.

Ninataka kila mtu awe na tabia ya kujisomea. Utamaduni wa kununua na kusoma vitabu hauko Tanzania. Hili ni janga. Ni hatari. Kuhusu kitabu hiki cha Sivalon, watu wanasikia tu wanayoambiwa. Hii ni tabia mbaya. Ni wa-Tanzania wangapi ambao wanacho kitabu hiki, na wamekisoma?

Kwa vile umeniulizia, nitajitahidi kukipa kipaumbele kitabu hiki, nikirudie ili niandike maoni yangu. Lakini ieleweke kwamba hakuna mtu anayeweza kutoa maoni kuhusu kitabu chochote yakawa ndio maoni pekee yaliyo sahihi. Ni muhimu kila mtu ajisomee, atafakari mwenyewe, na ajijengee mtazamo wake.

Na ukweli mwingine ni kwamba, hata ukishasoma kitabu, ukajijengea mtazamo, ukisoma tena utapata fikra tofauti. Ukisoma tena na tena, utaendelea kugundua vipengele ambavyo hukuvinasa kabla. Hili ni wazo tunalofundishwa katika taaluma zinazohusika na masuala ua usomaji.

Ninarudi nilipoanzia, kwamba, pamoja na kusikiliza maoni ya wengine, sherti kila mtu ajisomee mwenyewe.

Yusufu Mmary said...

Nafurahi kwa kusisitiza watu wajenge tabia ya kujisomea lakini, tunafikiri tabia hii ya kukuta kuna jamii moja inapenda kujisomea na nyingine haipendi ni suala la bahati mbaya, au ni mipango maalumu iliyoweka na aidha jamii yenyewe au mifumo? Kwa nini kwa mfano unakuta Wtznia hawapendi kujisomea kabisa, wakati huu ambao elimu imekuwa kuliko miaka ile ambayo ninyi mlisoma!

Johnbosco Mohamed said...

NAOMBENI MWENYE PDF YA HIKI KITABU ANATUMIA KTK "johnboscomohamed@gmail.com" Please!

Azad Mtunzi said...

Mimi niliwahi kukisoma.. na sehemu tata kuliko zote ni pale Mwalimu akimwambia mtafiti(Sivalon) kuwa kamuweka Mchungaji (kwa maana wa kiprotestanti)katika idarabya elimu yaTANU si kwa sababu ya taaluma yake bali kwa sababu ya imani yake.

Sa hapo mtu aweza kujenga hoja juu ya tafsiri sahihi.... lakini ukweli uko wazi hapo... unamuweka kwa kweli imani yake ili iweje(kwamba hakuna mwanataluma hata mmoja muaminifu???)


Jambo hilo haliingii akilini.