Sunday, February 13, 2011

Kitabu Kuhusu Mtume Muhammad

Kati ya vitabu ninavyosoma wakati huu ni Muhammad: A Biography of the Prophet, kilichoandikwa na Karen Armstrong. Ni kitabu murua kwa jinsi kinavyoelezea mazingira aliyoishi Mtume Muhammad na harakati alizopitia katika kutimiza majukumu yake kama Mtume.

Kitabu hiki kinagusa na kuelimisha sana sio tu kuhusu historia ya u-Islam, bali pia kuhusu upekee wa Mtume Muhammad, kama Karen Armstrong anavyosema:

If we could view Muhammad as we do any other important historical figure we would surely consider him to be one of the greatest geniuses the world has known
(uk.52). (Tafsiri yangu: Kama tungemtazama Muhammad kwa namna tunayowatazama watu wengine muhimu katika historia, ni wazi tungemtambua kama mmoja wa watu wenye vipaji vya ajabu kabisa ambao dunia imepata kuwafahamu).

Karen Armstrong ni maarufu kwa msimamo wake kuhusu u-Islam. Anaelezea sana historia ya zile anazoziita hisia potofu kuhusu u-Islam na zilivyoanza na kuenea. Lakini, pamoja na kutafiti na kuandika sana kuhusu u-Islam, Karen Armstrong ni mtafiti wa dini zingine pia, kama vile u-Kristu u-Juda, na u-Buddha. Ni mmoja wa watu wanaoongoza hapa duniani kwa umakini wa kuandika kuhusu dini.

Pamoja na kusoma kitabu cha Muhammad na kufuatilia maandishi mengine ya Karen Armstrong, na pamoja na kufuatilia mihadhara na mahojiano aliyotoa sehemu mbali mbali za dunia, nafuatilia pia maandishi na matamshi ya wengine kuhusu mchango wa Karen Armstrong. Nimebaini kuwa kuna malumbano kuhusu mchango wake, ambalo ni jambo la kutegemewa katika taaluma.

Kitabu cha Muhammad ni kizuri na muhimu sana. Nafurahi kukisoma, kwani kinanifungulia milango ya kuyafahamu maisha na mchango wa mtu ambaye ametoa mchango mkubwa sana duniani. Ni kitabu muhimu kwa yeyote mwenye nia ya kumwelewa Mtume Muhammad na kuuelewa u-Islam.

Karen Armstrong, ambaye alikuwa sista katika Kanisa Katoliki, ambalo ndilo dhehebu langu, anatuonyesha mfano mzuri, kwa kujibidisha katika kuzifahamu dini za wengine. Naamini kuwa iwapo sote tungefanya hivyo, kungekuwa na maelewano mazuri baina ya watu wa dini mbali mbali.

2 comments:

Simon Kitururu said...

Asante kwa dondoo Prof.!wa

Mbele said...

Shukrani Ndugu Kitururu. Ninaendelea na hii shughuli hii ya kujipunguzia umbumbumbu, taratibu, bila kusukumwa na mtu bali nafsi yangu.

Kuna mengine ambayo yanajitokeza na labda nitayaanika hapa kijiweni pangu. Ila nahisi baadhi yataleta mtafaruku, kwa sababu si kila mtu anapenda kusikia mambo tofauti na yale anayodhani ni ukweli.

Lakini sisi tunaodai tuna dini itabidi tujifunge moyo na kuupokea ukweli, kama vile tunavyokunja uso kabisa kabla ya kunywa dawa chungu :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...