Thursday, February 3, 2011

Mji wa Moshi, Tanzania

Moshi ni mji maarufu kaskazini mwa Tanzania, chini ya Mlima Kilimanjaro. Siufahamu sana mji huu, ingawa nimepita hapo mara kadhaa, na hata kulala, mara mbili tatu.






Kama ilivyo katika miji mikubwa ya Tanzania, Moshi kuna hoteli nzuri za kufikia wageni. Wakati moja nililala katika hoteli hii hapa kushoto.









Moshi ni maarufu kwa usafi. Wa-Tanzania wanajua kuwa uongozi wa Moshi una sheria kali kuhusu usafi. Hapo kushoto nipo kituo cha mabasi, pasafi kama vile pamepigwa deki. Nilikuwa safarini baina ya Arusha na Dar es Salaam. Nimechoka, shaghalabaghala; msafiri kafiri na kitabu changu cha Under Kilimanjaro.

Tangu mara yangu ya kwanza kuingia mjini Moshi, nilivutiwa na msikiti unaoonekana kushoto, ambao uko pembeni mwa kituo cha mabasi.







Wakati mmoja nilikuwa Moshi na wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, niliowaleta nchini kuwafundisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway alivyosafiri nchini mwetu akaandika juu yake. Niliwapeleka hadi Chuo cha Mweka, kinachoonekana kushoto. Kiko nje kidogo ya mji.

Ninapokuwa katika mji wowote napenda kujua maktaba ilipo. Hapo kushoto ni maktaba ya mkoa. Niliingia ndani, nikaona ilivyo nadhifu. Ina majarida na vitabu kiasi cha kuridhisha, nikifananisha na maktaba nilizoziona mikoani Tanzania. Nilivutiwa kuwaona watu wakisoma, sio watoto wa shule tu, kama ilivyo kwenye maktaba zingine.

Nilitembea kutoka Lutheran Uhuru Hostel kuelekea barabara kuu itokayo Arusha, nikaiona hoteli hii inayoonekana kushoto. Nilivutiwa na tangazo la mchemsho, ingawa sikupata kuingia ndani. Hamu ya kuingia nilikuwa nayo, kwa mategemeo ya kupata chakula cha ki-Chagga. Ni suala muhimu la kuzingatiwa siku za usoni, panapo majaliwa.

10 comments:

Simon Kitururu said...

Naudhaifu na mji huu!

Hasa kwa kuwa BABA yangu alitokea KILIMANJARO na kukuzia watoto wake wote nje ya ya MKOA ambao MOSHI ni nukta yake ,...
...na KATIKA kujaribu kutufanya tujisikie nyumbani MKOANI alijaribu sana kutufanya tuingie mji huo mara kwa mara kabla hajatupandisha HATA milimani kwa mababu na MABIBI!

Ila kwa bahati nzuri wakati miye bado mtoto nikagundua hapo mkoani kuna WACHAGA wengi ambao ni wezi kweli!:-)


Lakini WACHAGA eeh!


Mie MPARE naomba acheni wizi!

Najua kwa mamisi aka MISS TANZANIA tu wa TANZANIA mmetengeneza wengi kwahiyo wachaga labda mna genes za kutengeneza wasichana wazuri na WACHAGA wezi!:-(



Samahani Prof. Mbele !

Usijefikiria nawatukana WACHAGA.

Ila siye WAPARE na WACHAGA tuna kitu tunaita utani!


@WACHAGA MNAOMSOMA Prof MBELE:

NYIE WACHAGA acheni wizi!


Yani mmeiba mpaka STENDI YA MABASI MOSHI mmeifanya PROFESA MBELE anafikiri STENDI IMEPIGWA DEKI kumbe mbeiba mpaka makaratasi na mpaka kila kitu hapo na kwa mlivyo iba STENDI YA MOSHI ,...
....mpaka inaonekana imepigwa deki AISEE!:-)

Tukiacha utani:

HESHIMA zenu watu wa MOSHI na hata WILAYA nyingine kadhaa za KILIMANJARO ambazo naweza kuongezea hata mpaka kama ile ya SAME ,...

...kwa TZ kiusafi WA STENDI ,....

.... nawapa tano WAKUU!

Mbele said...

Loh, nimecheka kweli leo :-)

Kati ya mambo yanayonifurahisha sana Tanzania ni utani baina ya m-Pare na m-Chagga. Huwa navunjika mbavu kabisa :-)

Albert Kissima said...

Mji wa Moshi umenijengea tabia ya kutokutupa takataka hovyo (kuanzia karatasi za vocha, makopo n.k) katika mazingira popote pale niwapo. Wapo watu mahsusi waliosambazwa ktk mji huu kwa ajili ya kuwakamata wachafuzi wa mazingira. Wengi wameshaadabishwa kwa kutozwa faini. Bahati mbaya sijafuatilia na kujua ni kiasi gani watu huwa wanatozwa.

Kuna kila sababu ya watu kuadabishwa pale wanapotupa uchafu hovyo kwani kila baada ya umbali mfupi kuna sehemu maalumu ya kuhifadhi chochote kinachodhaniwa kuwa ni takataka.

@Kaka Simon, nami kupitia blog ya Prof Mbele naomba tu kuwashauri wapare waache ubahili maana wamekithiri. Mnanyimana (mnabaniana) hadi "genes" za urefu!Poo! :-)Hahahahahaha!

Simon Kitururu said...

@Albert Einstein Paul: Unataka kusema wewe MCHAGA hujawahi kustukia bonge la toto la KIPARE halafu lina pesaaaa mpaka likaamsha genes zako za wizi?

Na si unajua WAHAGA wanawake tu ndio wenye mchango chanya TANZANIA?:-)

Simon Kitururu said...

@WACHAGA: Samahani sentensi yangu hapo juu kwa mchaga ALBERT EINSTEI Paul iliyosomeka : ``Na si unajua WAHAGA wanawake tu ndio wenye mchango chanya TANZANIA?´´

Neno WAHAGA lisomeke . ``WACHAGA´´.


Na nawahurumia tu nyie WACHAGA kwakuwa hata nyie mnajua hakuna mchaga awezaye kushinda kesi akimshtaki MPARE.:-)

Albert Kissima said...

Duh! :-)

Fadhy Mtanga said...

mimi pia naupenda sana mji wa Moshi...usafi wake unavutia sana. pia naipenda hali ya hewa...nikiwa Moshi hujisikia fahari sana kila niuonapo mlima Kilimanjaro, fahari ya Afrika.

Christian Bwaya said...

Moshi pazuri. Tatizo ni athari za mabadiliko ya tabia nchi. Siku hizi joto karibia Dar! Zamani ilikuwa nadra kuiona barafu ya mlima mrefu kuliko yote Afrika. Lakini siku hizi, mambo yamebadilika. Vile vipara ya barafu karibia kila siku vinapungua shauri ya joto kali. Si muda mrefu fahari ya mlima huu itaanza kufifia.

Moshi watu wanasoma. Wauza magazeti(ambao wengi ni Wa-Pare) wanafanya biashara nzuri (iala wao wenyewe hawayasomi!). Mzunguko wa magazeti ni mkubwa Moshi. Yapo maduka kadhaa ya vitabu na yanauza hasa. Moja wapo ni hilo jengo jeupe nyuma yako kwenye picha uliyosimama hapo stendi. Vitabu mtumba navyo vinauzwa sana tu shauri ya bei yake nafuu. Moshi kumekucha.

Usafi wanajitahidi. Ukidodosha hata vocha ya muda wa maongezi wa simu tena kwa bahati mbaya, faini Tsh 50,000 hapo hapo. Hii imesaidia kuwalazimisha wakaazi wa mji huu kuwa na adabu katika utupaji taka has aneo la stendi kuu na baadhi ya maeneo ya katikati ya mji.

Tabia hii ingelazimishwa kufika hata kwenye maeneo mengine yenye pilika kama kule kwenye soko la mbuyuni, Moshi ingekuwa safi zaidi.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Mimi nimeoa huko. Nami nitembee kifua mbele na "kujimwambafai" kwamba nimeoa toto la Kichaga kutoka Moshi - mji safi na nadhifu kuliko yote Tanzania?

Mtakatifu - umenifurahisha sana!

emuthree said...

Kweli moshi sasa wanajitahidi kwa usafi, wakati nsoma Umbwe, nikiwa kituo cha basi pale Mosho mjini, waliniibia begi likiwa na zana zangu zote za shule...sitapasau, maana ilikuwa sekunde, nageuza kichwa kuangalia basi linavoingia kituoni, nageuka begi hakuna.
Watu wapo, na wala hawashughuliki na najua kabisa walimuonna huyo mwizi, lakini..kimiyaaaa!
sijui alipata faida gani.
hizo ni moja ya kumbukumbu zangu za moshi, nina muda mrefu sijafika huko!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...