
Moshi ni mji maarufu kaskazini mwa Tanzania, chini ya Mlima Kilimanjaro. Siufahamu sana mji huu, ingawa nimepita hapo mara kadhaa, na hata kulala, mara mbili tatu.

Kama ilivyo katika miji mikubwa ya Tanzania, Moshi kuna hoteli nzuri za kufikia wageni. Wakati moja nililala katika hoteli hii hapa kushoto.

Moshi ni maarufu kwa usafi. Wa-Tanzania wanajua kuwa uongozi wa Moshi una sheria kali kuhusu usafi. Hapo kushoto nipo kituo cha mabasi, pasafi kama vile pamepigwa deki. Nilikuwa safarini baina ya Arusha na Dar es Salaam. Nimechoka, shaghalabaghala; msafiri kafiri na kitabu changu cha
Under Kilimanjaro.

Tangu mara yangu ya kwanza kuingia mjini Moshi, nilivutiwa na msikiti unaoonekana kushoto, ambao uko pembeni mwa kituo cha mabasi.

Wakati mmoja nilikuwa Moshi na wanafunzi kutoka
Chuo cha Colorado, niliowaleta nchini kuwafundisha kuhusu mwandishi
Ernest Hemingway alivyosafiri nchini mwetu akaandika juu yake. Niliwapeleka hadi Chuo cha Mweka, kinachoonekana kushoto. Kiko nje kidogo ya mji.

Ninapokuwa katika mji wowote napenda kujua maktaba ilipo. Hapo kushoto ni maktaba ya mkoa. Niliingia ndani, nikaona ilivyo nadhifu. Ina majarida na vitabu kiasi cha kuridhisha, nikifananisha na maktaba nilizoziona mikoani Tanzania. Nilivutiwa kuwaona watu wakisoma, sio watoto wa shule tu, kama ilivyo kwenye maktaba zingine.

Nilitembea kutoka
Lutheran Uhuru Hostel kuelekea barabara kuu itokayo Arusha, nikaiona hoteli hii inayoonekana kushoto. Nilivutiwa na tangazo la mchemsho, ingawa sikupata kuingia ndani. Hamu ya kuingia nilikuwa nayo, kwa mategemeo ya kupata chakula cha ki-Chagga. Ni suala muhimu la kuzingatiwa siku za usoni, panapo majaliwa.