Sunday, February 27, 2011

Vitabu vya Chap Chap

Wengi wetu tunalalamika kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia au kufa miongoni mwa wa-Tanzania. Malalamiko haya yako sana katika hii blogu yangu. Kwa mfano, soma hapa.

Labda kuna haja ya kufafanua kitu tunachokilalamikia, maana wa-Tanzania hao hao inaonekana wanasoma sana vitabu ambavyo vinatungwa papo kwa papo kuhusu masuala kama vile mapenzi.

Vitabu hivi vinaandikwa haraka na kuchapishwa haraka na ndio maana naviita vitabu vya chap chap. Ni vijitabu, kwani vina kurasa chache tu.


Mwaka jana nilipokuwa Tanzania nilinunua kitabu cha aina hiyo kiitwacho "Pata Mambo, Part 5 ," kilichoandikwa na Fuad Kitogo (Dar es Salaam: Elite Business). Ingawa hiki ni kijitabu cha kurasa 40 tu, kinashughulikia masuala mengi kama inavyooneka katika picha ya jarida hapo juu.

Hivi vitabu vya chap chap si vitabu vyenye kiwango cha kuridhisha kitaaluma, bali vinawavutia na labda kuwaridhisha wasomaji wa ki-Tanzania. Katika ukurasa wa kwanza kuna maelezo haya: "Kitabu hiki ni mwendelezo wa vitabu vya Pata Mambo kuanzia namba moja vinavyopendwa kusomwa nchi nzima."

Kuwepo kwa vitabu hivi na kupendwa kwake ni changamoto kwetu sisi tunaodai kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia Tanzania. Labda uvivu tunaoulalamikia uko kwenye kusoma vitabu vikubwa vinavyotumia muda na fikra zaidi katika kuvisoma, tofauti na hivi vya chap chap ambavyo ni rahisi kuvisoma na kuvimaliza.

10 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Tatizo la kusoma halipo kwenye vitabu tu. Hata ukiangalia mzunguko wa magazeti ya udaku na yale ya habari unagundua kuwa udaku unalipa na kusomwa sana. Hii ni kutokana na kuwa na jamii ya kidaku na si makini.

Ukienda Kenya gazeti la The Daily Nation huwa na kurasa hadi 70 kwa chapisho na linauza kama njugu. Kenya hakuna gazeti hata moja la udaku zaidi ya gutter newspaper moja tu. Uganda kuna moja tu la Pepper au pili pili.

Hapa tatizo ni nini? Jibu utalipata kwenye vitu nchi hizi za Afrika Mashariki husifika kwavyo. Kenya husifika kwa ujasiriamali, Uganda elimu na Tanzania Groceries-unaweza kuongeza udaku.

Sikiliza au tazama hata luninga zetu. Ni udaku au tuseme uchafu mtupu. Hata khanga wavaazo wake na dada zetu ni udaku mtupu. Miziki hasa taarabu au mipasho ni udaku mtupu.

Nakubaliana na Kaka Mbele. Hata ukiangalia vipaumbele vya watawala wetu. Jikumbushe siku Kikwete akikabiliwa na shutuma za kuchakachua alivyohutubia taifa kwa maneno machache na kusema: 'Tumalize watu waende kujimwanga" na siyo kutafakari ujenzi wa taifa.
Sitaki niseme mengi. Tatizo la jamii yetu ni ulimbukeni na udaku. Watu hawataki kufikiri. Wanataka kuduwaa na kula maraha hata kwa kualika karaha na balaa.

Wapo matapeli wengi wametajirika haraka kwa kuandika udaku au kuigiza filamu za matusi. Kwa vile walaji wetu wanaweza na wanapenda kula uchafu, matapeli wachache wanazidi kuchuma ambapo wangepaswa kufa kwa ukata. Wenye kuandika vitabu makini hawana soko. Ndiyo maana naanza kufikiri kuandika kwa kiingereza ili kufikia watu wenye akili badala ya kiswahili kutokana na waswahili wangu kutopenda kusoma vitu vyenye kufirisha.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kumradhini. Neno la mwisho ni kufikirisha na si kufirisha. Ni makosa ya kawaida kiuandishi.

Mbele said...

Shukrani kwa changamoto hii murua. Naifahamu Kenya vya kutosha. Ni kama unavyosema. Kuongezea hapo uliposema, kuhusu magazeti kama "The Daily Nation," utaona kuwa mara kwa mara yana kurasa nyingi zinazojadili vitabu vya kufikirisha.

Ni kweli, udaku ndio elimu ya wa-Tanzania. Kitu cha kustaajabisha ni pale rais anapotoa ahadi kuwa serikali ya CCM itatengeneza ajira milioni kadhaa. Sasa kweli wa-Tanzania na elimu yao ya udaku wataweza kushindana na wa-Kenya kwenye intavyuu ya ajira?

Haishangazi kuwa wa-Kenya wanamiminika nchini na kujitwalia ajira, wakati wa-Tanzania wanangojea ahadi ya ajira milioni ngapi sijui.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kijitabu hiki kweli kimesheheni kwani inaonekana mwandishi mpaka amekosa mahali pa kuweka vidokezo hapo juu ya ganda....Kazi kweli kweli.

Ni usiku sasa na nitarudi kutoa maoni ya kina baadaye kuhusu suala hili nikiamshwa salama. Tunapolifikiria suala hili na hasa hoja zilizozushwa na Mwalimu Mhango, pengine si vibaya tukiurejelea mjadala fulani uliowahi kurindima hapa:

http://changamotoyetu.blogspot.com/2010/09/mimi-najifunza-kitu-wewe-je.html

Usiku mwema.

Christian Bwaya said...

Mhango, hoja zako zimenifunza. Hali hii inasikitisha sana. Muhimu, tuendelee kutazama uwezekano wa kuisaidia jamii yetu pale tunapoweza.

mnkadebe said...

Prof. Mbele hapo nimekuelewa.

Binafsi naona hili basi ni tatizo la kimfumo, yaani our education sector is deficient in that it doesnt demand that type of deep, analytical and higher order thinking,mwisho unabakiwa na chapisho Kama hizo. Nadhani  kamamsikosei, enzi zenu mfumo wa elimu ulikua ule wa "Cambridge" ambao ulidandia viwango vingi, na mambo mengi, kiutaaluma ya kimataifa au?

Kuhusu nchi jirani, tukumbuke kwamba upende wa magazeti ya Kenya, wao huandika kwa Kiingereza kwa hiyo soko lao ni kubwa, the quality of analysis reflects on a wider readership, sio wa Kenya asilia tu; wamo humo wasomi wengi wa mashirika na makampuni ya kimataifa yaliyo pale Nairobi.

Mwisho ni kusema tu kwamba tatizo hili la kutofikiri kwa undone sana piamlipo upend wa sera za serikali. Watanzainia hula tunapotoshwa na majibu mopes kwa matatizo magma kwa uzembe hue wa kutotafakari kinamna uliogusia (ii.e. Mikataba isiyo na manufaa kwetu).

Asante kwa kupanua na kutuelimisha kwakutumia mfano hai.

Simon Kitururu said...

Mmmmmmh!

Christian Sikapundwa said...

Profesa,ukweli ni kwamba udaku watu hupenda kusoma sana kuliko habari za kweli na za kuijenga jamii.

Kama ni gazeti utakuta nyumbani baba kanunua lakini hataki binti alisome anamficha,kumbe na binti naye analo anaogopa kulionyesha kwa wazazi wake basi mambo hapo yanapokuwa matamu kweli.

lakini pili ule mwonekano wa nje wa kitabu chochoe kuna mvutia mtu kupenda kujua nini kilichopo,wewe ni mwana Literature nadhani unanipata maana yangu.

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Wapendwa;

Japo sikurudi kwa wakati uliopangwa kama nilivyokuwa nimeahidi (binadamu!) pengine ningependa tu kwanza tujiulize ni kwa nini magazeti na vitabu vya udaku vinapendwa sana duniani kote?

John Mwaipopo said...

labda nikijipapatua naweza kuongeza kuwa hata redio karibu zote zimekuwa za udaku, bongo fleva na mambo kama hayo.

kizazi cha sasa kinashambuliwa na mambo yasiyo ya maana sana kutoka kila kona. vitabu vya shuleni ni vile maswali na majibu. siovile vya kupanua uelewa na udadisi. watoto wanasoma maswali ili waende hatua ya mbele.

vitabu vya mtaani ndio kama hivyo. vitabu vya kina ben mtobwa, mkufya, richard mabala na kama hao sio tu havisomwi tena bali bia hata watunzi wa namana hiyo hawapo tena. wapo hawa wa fasta-fasta na ukengeushaji wa maadili.

kutoka magazetini kizazi hiki kimeshambuliwa na hadidhi na hekaya za 'chumbani' na tamthiliya za america ya kusini bila ya kusahau mpira wa uingereza. wapi yanga, simba, pamba na maji maji ya songea?

luninga ndio usiombe. ni muziki na fasheni.

au ndio falsafa ya 'kijacho mjini si haramu'

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...