Showing posts with label utamaduni wa kusoma vitabu. Show all posts
Showing posts with label utamaduni wa kusoma vitabu. Show all posts

Tuesday, December 20, 2016

Zawadi ya Krismasi

Siku tatu zilizopita, jirani yangu m-Marekani, mama mwenye umri zaidi yangu, aliniomba nimsainie nakala za kitabu cha Africans and Americans Embracing Cultural Differences. Alikuwa amevinunua kwa ajili ya kuwapelekea rafiki zake, wa-Marekani wenzake, kama zawadi ya Krismasi.

Jambo hili lilitosha kunifanya niandike ujumbe katika blogu yangu, kwani linadhihirisha jadi ninayoiona hapa Marekani, kama nilivyowahi kudokeza katika blogu hii. Lakini nimehamasika kuandika baada ya kusoma makala ambayo ameichapisha Christian Bwaya katika blogu yake. Ameelezea umuhimu wa zawadi kwa watoto na mambo ya kuzingatia katika kutoa zawadi kwa watoto.

Kati ya mifano ya zawadi alizotaja ni vitabu. Ni jambo muhimu, nami kama mwalimu ninaliafiki moja kwa moja. Nimejionea jinsi watoto wanavyopenda vitabu, sio tu hapa Marekani, bali pia Tanzania. Nimeandika mara kwa mara umuhimu wa kuwasomea watoto vitabu na kuwajenga watoto katika utamaduni wa kusoma vitabu. Huwa ninafarijika ninaposoma taarifa za uhamasishaji wa suala hilo.

Tutakuwa tumepiga hatua kubwa iwapo tutajijengea utamaduni wa kuwanunulia watoto vitabu kama zawadi, kwani wanavipenda vitabu. Tutakuwa tumepiga hatua iwapo vijana wetu na watu wa kila rika watakuwa na utamaduni wa kuthamini zawadi ya vitabu.

Friday, September 30, 2016

M-Kenya Kaniandikia Kuhusu Kitabu Changu

Nimefurahi sana, tangu usiku wa kuamkia leo, kupata maoni ya msomaji wa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Msomaji huyu ni mama m-Kenya ambaye anaishi hapa Minnesota, Marekani. Aliniandikia katika Facebook ujumbe huu:

I did not tell you how precious your book is. My friend and I were reading it to our kids during a sleep over and it is amazing how your culture is similar to ours. You did well and it was very easy to understand and flow with. You are gifted Mwalimu. God bless you more. Thank you again for the great gift.

Huyu mama tulikutana tarehe 30 Aprili, mwaka huu, kwenye tamasha mjini Rochester. Alikuja kwenye meza yangu, tukasalimiana na kuongea. Alivutiwa na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, akaulizia namna ya kukipata siku nyingine, kwa kuwa hakuja na hela. Hapo hapo nilimpa nakala ya bure. Alishangaa, akashukuru sana.

Nimefurahi kuwa ameniandikia maoni yake kuhusu kitabu hicho. Ninamfananisha na wa-Tanzania kadhaa ambao, baada ya kuniomba, nimewapa nakala za bure za kitabu hiki. Nilitegemea na ningefurahi iwapo wangeniletea neno kuhusu kitabu, lakini sikuwasikia tena. Nawajibika kusema kuwa sioni kama huu ni uungwana.

Ninapowazia jambo hilo, ninapata hisia kuwa huenda hao watu hawakusoma kitabu hicho. Wazo hilo linanifikia kwa kuzingatia ukweli kwamba utamaduni wa kusoma vitabu hauonekani katika jamii ya wa-Tanzania. Hili ni jambo ambalo limelalamikiwa na linaendelea kulalamikiwa na wadau wa vitabu kama vile waandishi na wachapishaji.

Kwa upande wa wa-Kenya, nimejionea kuwa wanao utamaduni wa kupenda vitabu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Hali hiyo ninaishuhudia sio tu huku nje ya Afrika, bali pia  nchini mwao. Ushahidi moja wa wazi ni kuwa makala kuhusu vitabu si jambo geni katika magazeti ya Kenya. Kwa upade wa Tanznia, sijui ni lini niliwahi kuona gazeti la aina hiyo.

Hainifurahishi kusema mambo hayo kuhusu wa-Tanzania, lakini ninachosema ni ukweli nilivyouona. Ukweli unapaswa kusemwa, hata kama unauma. Hainishangazi kwamba hata katika soko la ajira, iwe ni Afrika Mashariki au kwingineko, wanajiamini kuliko wa-Tanzania.

Saturday, December 26, 2015

Jólabókaflóð: Mafuriko ya Vitabu Nchini Iceland

Nchi ya Iceland inaongoza ulimwenguni kwa usomaji wa vitabu, na pia kwa asilimia ya watu wanaochapisha vitabu. Hilo linatosha kuipambanua nchi ile. Lakini kuna pia jadi iitwayo Jólabókaflóð, yaani mafuriko ya vitabu, ambayo hutokea majira ya Krismasi.

Kila mwaka, kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba, pilika pilika zinazohusiana na vitabu zinapamba moto. Wachapishaji wa vitabu wanaongeza juhudi ya kutangaza vitabu, na jamii nzima huwa katika heka heka ya kununua vitabu. Mazungumzo na malumbano kuhusu vitabu hushamiri kila mahali.

Mwezi Novemba, katalogi kubwa ya vitabu iitwayo bókatíðindi inachapishwa na kugawiwa bure karibu kila nyumba. Katalogi hii huorodhesha vitabu karibu vyote vilivyochapishwa katika mwaka husika. Kadiri Krismasi inavyokaribia, shughuli ya kuzawadiana vitabu inapamba moto. Kilele huwa ni tarehe 24 Desemba, ambayo ni mkesha wa Krismasi. Watu hutumia mkesha wa Krismasi wakisoma vitabu.

Taarifa hizo sikuwa ninazifahamu, hadi leo. Sikujua kuwa utamaduni wa Iceland umefungamana na vitabu kiasi hicho. Nimejikuta ninawazia hali ilivyo nchini mwangu Tanzania. Nimekumbuka makala niliyoandika katika blogu hii nikiwazia ingekuwaje iwapo wa-Tanzania tungeanzisha utamaduni wa kupeana vitabu kama zawadi ya Idd el Fitr au Krismasi.

Je, sisi wa-Tanzania tunaweza kuthubutu kuwapelekea wa-Tanzania wenzetu vitabu kama zawadi ya sikukuu au ya sherehe kama arusi? Tafakari mwenyewe.

Saturday, December 5, 2015

Kuwalea Watoto Kupenda Vitabu

Kati ya mambo yanayonivutia sana hapa Marekani ni namna wazazi wanavyowalea watoto katika utamaduni wa kupenda kusoma vitabu. Katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba, ninawaona wazazi wakiwa na watoto. Nimewahi kuandika kuhusu suala hilo katika blogu hii. Lakini kwa kuwa hii ni mada ninayoitilia maanani sana, nimeamua kuiongelea tena.

Picha ya juu hapa kushoto ilipigwa mwaka 2008, niliposhiriki sherehe za kumbukumbu ya uhuru wa Nigeria hapa Minnesota. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Nakumbuka vizuri jinsi huyu mama m-Nigeria anayeonekana pichani alivyokuja mezani pangu na binti yake. Tulisalimiana, wakaangalia na kuvifurahia vitabu vyangu, kama inavyoonekana pichani.

Picha ya pili hapa kushoto nilipiga katika tamasha la vitabu la Deep Valley, mjini Mankato, Minnesota. Nilivutiwa na namna hao watoto walivyokuwa wanafuatana na mama yao kutoka meza hadi meza wakiangalia vitabu.

Picha ya tatu hapa kushoto nilipiga mwezi Agosti mwaka huu mjini Brooklyn Park, Minnesota, katika tamasha la Afrifest. Huyu bwana, m-Marekani Mweusi, alikuja na watoto wake kwenye meza yangu, kuangalia vitabu. Watoto hao ni wadogo sana, na sijui kama walikuwa wanajua kusoma, lakini, nilivutiwa na kitendo cha baba yao kuwaleta kuangalia vitabu.

Kwa wa-Marekani, umri wa mtoto si tatizo. Wanawasomea vitabu hata watoto wadogo sana, hasa kabla ya kulala. Watoto wanapenda kusomewa vitabu. Hapa naikumbuka video ya kusisimua inayomwonyesha mtoto mdogo akisomewa vitabu, halafu anavyoangua kilio kila anapoambiwa kuwa hadithi imeisha. Hebu iangalie.


Sunday, February 27, 2011

Vitabu vya Chap Chap

Wengi wetu tunalalamika kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia au kufa miongoni mwa wa-Tanzania. Malalamiko haya yako sana katika hii blogu yangu. Kwa mfano, soma hapa.

Labda kuna haja ya kufafanua kitu tunachokilalamikia, maana wa-Tanzania hao hao inaonekana wanasoma sana vitabu ambavyo vinatungwa papo kwa papo kuhusu masuala kama vile mapenzi.

Vitabu hivi vinaandikwa haraka na kuchapishwa haraka na ndio maana naviita vitabu vya chap chap. Ni vijitabu, kwani vina kurasa chache tu.


Mwaka jana nilipokuwa Tanzania nilinunua kitabu cha aina hiyo kiitwacho "Pata Mambo, Part 5 ," kilichoandikwa na Fuad Kitogo (Dar es Salaam: Elite Business). Ingawa hiki ni kijitabu cha kurasa 40 tu, kinashughulikia masuala mengi kama inavyooneka katika picha ya jarida hapo juu.

Hivi vitabu vya chap chap si vitabu vyenye kiwango cha kuridhisha kitaaluma, bali vinawavutia na labda kuwaridhisha wasomaji wa ki-Tanzania. Katika ukurasa wa kwanza kuna maelezo haya: "Kitabu hiki ni mwendelezo wa vitabu vya Pata Mambo kuanzia namba moja vinavyopendwa kusomwa nchi nzima."

Kuwepo kwa vitabu hivi na kupendwa kwake ni changamoto kwetu sisi tunaodai kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia Tanzania. Labda uvivu tunaoulalamikia uko kwenye kusoma vitabu vikubwa vinavyotumia muda na fikra zaidi katika kuvisoma, tofauti na hivi vya chap chap ambavyo ni rahisi kuvisoma na kuvimaliza.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...