Enzi za mababu na mabibi zetu, ilikuwa ni kawaida kwa wazee kukaa na watoto jioni na kuwasimulia hadithi. Utamaduni huu ulikuwa sehemu ya maisha. Ilikuwa ni sehemu ya elimu waliyopewa hao watoto. Hapakuwa na shule tulizo nazo leo, wala vitabu, lakini wazee walikuwa walimu bora, waliotumia mbinu mbali mbali, kama hizi hadithi, katika kuwaelimisha watoto.
Siku hizi, kutokana na kuwepo kwa vitabu, tunayo fursa ya kutumia vitabu kuendeleza elimu ya watoto. Kama hatuna uwezo wa kuwasimulia hadithi kwa mtindo wa mababu na mabibi zetu, tunayo fursa ya kuwasomea vitabu. Wenzetu katika nchi kama Marekani wanaendeleza utamaduni huu kwa kuwasomea watoto hadithi za vitabuni. Watoto wa kiMarekani wanategemea mzazi awasomee vitabu. Ni kawaida kwa mzazi kumsomea mtoto kitabu kabla hajalala.
Mashuleni na kwenye maktaba za Marekani, kuna utaratibu wa kuwa na vipindi vya kuwasomea watoto vitabu. Watu wanajitolea kwenda maktabani au mashuleni kufanya kazi hiyo, wawe ni wafanyakazi maofisini, madaktari, wanajeshi au polisi, wanasiasa au viongozi.
Kila mtu atakumbuka, kwa mfano, kwamba siku ile ya Septemba 11, 2001, ambapo mji wa New York ulishambuliwa na magaidi, Rais Bush alikuwa darasani akijumuika na watoto waliokuwa wakisoma. Rais mpya Obama, pamoja na shughuli zake nyingi, anafuata utamaduni huo, kama ilivyoandikwa hapa.
Kuwasomea watoto vitabu kunawajengea mazoea ya kusoma na kuwapanua mawazo. Ni fursa ya kujenga na kuimarisha uhusiano baina ya watoto na watu wazima. Wataalam wa elimu ya watoto wanasema kuwa kumsomea mtoto vitabu tangu anapokuwa mdogo ni njia moja ya kumjengea msingi wa mafanikio maishani.
Watanzania tuko wapi katika suala hili? Je, wazazi wanaendeleza utamaduni wa mababu na mabibi wa kuwasimulia watoto hadithi? Na kwa vile tuko katika utamaduni wa vitabu, tunavyo vitabu majumbani? Tunawasomea watoto wetu?
Watu wazima katika Tanzania wanatumia muda mwingi kwenye sehemu zinazoitwa vijiweni. Wangeweza kutumia muda huu kwenda shuleni kusaidiana na walimu kwa namna moja au nyingine, kama wanavyofanya Wamarekani, kwa kujitolea. Wakati walimu wanasahihisha daftari, kwa mfano, wazazi wangeweza kusimamia shughuli za nje ya darasa, kama vile usafi, kilimo, au ufugaji, au wangeweza kusaidia somo moja au jingine.
Kuna watu wazima wengi Tanzania ambao wamesoma vya kutosha, na wangeweza kutoa mchango mkubwa mashuleni, kwa msingi wa kujitolea. Kama wabunge, wafanyabiashara, viongozi wa mitaa, watafiti na wengine wangefanya hivyo, watoto wangefaidika, na Taifa lingepiga hatua nzuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
5 comments:
Tatizo ni pale hata watu wazima tunapoacha kusoma vitabu kwa sababu kozi imeisha na mtihani umefanyika.:-(
Inasikitisha kwamba watoto siku hizi wanakuwa wenyewe bila miongozo ya watu wazima halafu ni watu wazima walalamikao kuwa watoto wa siku hizi wameharibika.:-(
Moja ya tatizo letu tunawaachia walimu mashuleni wafanye kila kitu mtoto akirudi nyumbani mzazi yeye kila siku hana muda ila muda wa kijiweni haukosekani!Tusipo badilika tutashindwa kushindana kimataifa na tunawanyima watoto wetu dignity wanayostahili. Serikali ya Marekani imeimarisha Libraries almost katika kila kitongoji sielewi kwanini Libraries kwetu ni chache. Kwa Watanzania wanaopenda kusoma upatikanaji wa vitabu mbalimbali bado ni wa matatizo especially mikoani.Ila tusikate tamaa Article kama hii ni changamoto nzuri kutuamsha tuliolala. By the way nitapata wapi hicho kitabu cha Alfu lela ulela?nime google bila mafanikio.
Ni kweli kuwa tumefikia mahali ambapo vitabu havithaminiwi katika nchi yetu. Kuanzia miongoni mwa raia hadi kwa viongozi, utamaduni wa kuvitafuta vitabu, kuvisoma kwa ari na kuvifurahia, na kuelewa kuwa vitabu ni hazina na ufunguo wa maisha, utamaduni huo umetoweka. Hili ni janga kwa nchi yetu, na athari zake zitatukabili kwa miaka mingi, maana watoto wetu wanakulia katika mazingira haya. Watu wazima Tanzania hawana wazo la kushirikiana na watoto katika kusoma. Wanadhani hii ni kazi ya mwalimu tu. Najiuliza kama hata viongozi wetu wanavyo vitabu majumbani mwao, kwa ajili yao na watoto wao. Najiuliza kama kuna kiongozi yeyote anayesoma vitabu na kuwa mfano kwa watoto wake mwenyewe na kwa wananchi.
Kwa bahati nzuri, vitabu tulivyokuwa tunavipenda zamani kama hivi vya Alfu Lela u Lela, vimeanza kupatikana tena, baada ya baadhi ya wachapishaji wetu kuamua kuvifufua. Wachapishaji kadhaa wa Tanzania ni washiriki katika African Books Collective, ambayo husambaza vitabu vyao nje ya Afrika. Alfu lela u Lela kinapatikana hapa.
Kaka Mbele, nakupa mia kwa mia. Kwa kweli Tanzania lazima tubadilike na kuanza kujali watoto wote na shule za watoto kwa vitendo na sio maneno na kukimbilia shule binafsi za ajabu ajabu. Nakubaliana na wewe mia kwa mia na utaratibu mzima wa wazazi pia wawe wanahusika na elimu za watoto wao kwenda na kujitoa kwenye maswala mbali mbali ya shule kwa hali na mali. Haitoshi kusema tunalipa kodi kisha kukaa na kusubiri muujiza ufanyike. Wamarekeani walipa kodi sana na wanajitoa sana kwenye kazi za shule za chini "shule za msingi" ndio maana tunaona wao wanamaendelea sana katika elimu. Watanzania wenzangu sasa tuanze na sisi kuwajibika kwa elimu na kuacha kukaa vibarazani na kuagiza chupa na nyama choma.
Sio tu watu kujisomea vitabu na kuwasomea watoto, bali hata kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni yako vipi mzazi anakuwa hana muda huo
Mtoto anarudi shule na kujifanyia home work mwenyewe na pale anaposhindwa msaada wa mzazi hakuna kwa sababu mzazi yuko kijiweni, baa au atajifanya kazi nyingi ofisini na kuchelewa kurudi nyumbani
Muda mwingi malezi ya watoto yanategemea sana wafanyakazi wa ndani ndio maana siku hizi hata ile michezo tuliyocheza zamani watoto hawaijui
Post a Comment