Thursday, September 24, 2015

"Papa's Shadow" Yapongezwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa

Tarehe 20 mwezi huu nilipeleka ujumbe Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa kuhusu filamu ya Papa's Shadow. Sikuandika ujumbe mrefu, bali niliwatumia kiunganishi hiki.

Bila kuchelewa, tarehe 22 nilipata ujumbe kutoka kwao, ukiwa umeandikwa na Ndugu Noel Kabanda. Uwakilishi unaafiki kuwa Papa's Shadow ni "fursa maridhawa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni" na unasisitiza kuwa "Serikali inatambua mchango wa sanaa katika kuitangaza Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii na utamaduni."

Kwanza, kwa kuzingatia uwingi wa majukumu yanayowakabili wawakilishi wetu katika balozi zetu, nimeona ni muhimu kusema nilivyoguswa na jinsi Uwakilishi ulivyoushughulikia ujumbe wangu.

Pili, ujumbe wa Uwakilishi unawatia moyo wahusika wa Ramble Pictures, ambao ndio watengeneaji wa Papa's Shadow. Timu nzima ya Ramble Pictures ni vijana wa ki-Marekani, na baadhi yao walikuja Tanzania mwaka 2013 kwenye kozi yangu ya Hemingway Katika Afrika Mashariki. Ni furaha kwangu, na jambo la kujivunia, kuwaeleza vijana hao kuwa Uwakilishi wa Kudumu waTanzania Umoja wa Mataifa umeipokea Papa's Shadow kwa namna hii.

Papa's Shadow si filamu ya maigizo. Ni filamu ya kuelimisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni maongezi baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi Hemingway. Tunaongelea maisha ya Hemingway, safari zake, uandishi wake, na fikra zake kuhusu masuala mbali mbali. Tunawafungua macho walimwengu kuhusu namna Hemingway alivyoipenda Afrika na alivyokuwa mtetezi wa Afrika.

Hemingway alisafiri na kuishi Afrika Mashariki mara mbili, mwaka 1933-34 na 1953-54. Aliandika hadithi, insha, barua na maandishi mengine ambayo ni hazina kubwa. Wenzetu katika nchi zingine ambako Hemingway alipita au kuishi na akaandika habari za huko, wametumia fursa hiyo kujitangaza, na wanawavutia watalii wengi sana. Mifano ni miji kama Paris (Ufaransa), Havana (Cuba), Oak Park (Illinois, Marekani), Key West (Florida, Marekani), na Pamplona (Hispania). Hemingway anapendwa ulimwenguni kote ambako watu wana utamaduni wa kusoma vitabu. Sina shaka kuwa Papa's Shadow italeta msisimko wa aina hiyo kwa kuwaelekeza mashabiki wa Hemingway nchini kwetu.

Hamu ya kuona Tanzania inafunguka macho kuhusu fursa hii ilinihamasisha kufanya utafiti juu ya safari za Hemingway katika nchi yetu na maandishi aliyoandika. Kozi niliyotunga ilikuwa na lengo hili. Nilitaka pia kuwasaidia walimwengu kuelewa umuhimu wa Afrika katika maisha na uandishi wa Hemingway. Kwa msingi huo huo, nilishiriki kikamilifu katika kufanikisha filamu ya Papa's Shadow.

Nimeeleza hayo yote ili kuweka wazi umuhimu wa ujumbe wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa. Ni mfano wa mshikamano unaotakiwa baina yetu wanadiaspora, serikali, na wananchi wenzetu.

2 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...

Je filamu hii inapatikana wapi Dar au Nairobi? Tafadhali tujulishe.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa ulizo lako. Filamu itakuwa tayari kusambazwa baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria, hasa hatimiliki za vipengele mbali mbali. Kwa sasa kuna mchango wa fedha unafanyika ili hatimaye gharama zote zilipwe. Insha Allah, mwanzoni mwa mwaka ujao kila kitu kitakuwa kimekamilika, nami nitaweka taarifa katika blogu hii. Mimi nimeshaiangalia filamu yote. Nimeridhika nayo kabisa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...