Showing posts with label utalii Tanzania. Show all posts
Showing posts with label utalii Tanzania. Show all posts

Wednesday, January 11, 2017

Zawadi Kutoka Ramble Pictures Kwa Heshima Ya Hemingway

Wiki iliyopita nimepata zawadi ya picha kutoka Ramble Pictures, kampuni ya kutengeneza filamu. Kampuni hiyo ndiyo iliyotengeneza filamu ya Papa's Shadow, inayohusu maisha na safari za mwandishi maarufu Ernest Hemingway Afrika Mashariki, pamoja na maandishi yake kuhusu Afrika Mashariki. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni mazungumzo baina ya Mzee Patrick Hemingway na mimi, kuhusu masuala hayo.

Picha niliyopewa inaitangaza filamu ya Papa's Shadow. Inamwonesha Ernest Hemingway, Patrick Hemingway na mimi, Kuna pia Mlima Kilimanjaro na nchi tambarare chini ya mlima, na pia ndege ikiwa angani. Hiyo picha ya mlima na mazingira yake, pamoja na ndege, inakumshia hadithi maarufu ya Hemingway, "The Snows of Kilimanjaro."

Nimeguswa na picha hii. Ni heshima kubwa kuliko ninavyostahili kuwekwa sambamba na Ernest Hemingway na Patrick Hemingway. Ernest Hemingway alileta mapinduzi katika uandishi na alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi mwaka 1954. Patrick Hemingway ni mtu muhimu kwa watafiti wa Hemingway, akiwa ni mtoto pekee aliye bado hai wa Ernest Hemingway. Ametoa na anaendelea kutoa mchango mkubwa wa kuhariri maandishi ya Hemingway na kuyaandikia utangulizi.

Kwa upande mwingine ninafurahi kuoneshwa pamoja na Patrick Hemingway, ambaye ni mtu wa karibu kwangu. Ananifundisha mengi kuhusu Afrika Mashariki ya wakati alipoishi kule, kuhusu maisha na uandishi wa Hemingway, na kuhusu waandishi wengine, hasa wa wakati wa Hemingway.

Vile vile, Patrick Hemingway anakipenda sana kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Hata katika filamu ya Papa's Shadow, anakitaja, na kuna mahali anasoma kisehemu cha kitabu hiki kwa ki-Swahili na tafsiri yangu ya ki-Ingereza.

Filamu ya Papa's Shadow inaelezea upande wa Ernest Hemingway ambao haufahamiki vizuri, yaani jinsi alivyovutiwa na Afrika kwa maisha yake yote. Katika kufanya utafiti juu ya Hemingway na kusoma maandishi yake kwa miaka kadhaa, niligundua kuwa aliipenda Afrika tangu alipokuwa mtoto. Ndipo nikaamua kutunga kozi kuhusu mada hiyo.

Mwanafunzi mmoja katika kozi hiyo, Jimmy Gildea, alipata motisha ya kutengeneza filamu, na matokeo yake ni Papa's Shadow. Pamoja na kuelimisha juu ya uhusiano wa Hemingway na Afrika, filamu hii inaitangaza Tanzania. Nakala za filamu hii zinapatikana kwa kuwasiliana na Ramble Pictures kwa barua pepe: info@ramblepictures.com au kwa simu (952) 426-5809.

Wednesday, October 26, 2016

Miaka 80 ya "The Snows of Kilimanjaro"

Kwa mara nyingine tena, ninaandika ujumbe kuhusu kutimia kwa miaka 80 tangu hadithi ya Ernest Hemingway, 'The Snows of Kilimanjaro" ilipochapishwa kwa mara ya kwanza. Niliandika ujumbe wa aina hiyo katika blogu hii. Leo nimesoma tena ujumbe wangu, nikajiridhisha kwamba niliyosema ndiyo ninayoamini hadi sasa.

Jambo moja kubwa kabisa ni kuwa wa-Tanzania tunajipotezea fursa za wazi za kutumia hazina kama hii hadithi ya Hemingway kuitangaza nchi yetu. Niliandika katika ujumbe wangu baadhi ya mambo ambayo tungeyafanya mwaka huu wa kumbukumbu. Lakini mwaka unaelekea ukingoni, na hakuna tulichofanya. Hii ni hasara ya kukosa utamaduni wa kusoma vitabu. Tunashindwa hata kutumia fursa zilizo wazi.

Nimeona niandike ujumbe huu leo kwa sababu wiki hii, hapa katika Chuo cha St. Olaf ninapofundisha, litatokea jambo la pekee linalohusiana na Ernest Hemingway. Keshokutwa, tarehe 28, pataonyeshwa kwa mara ya kwanza filamu ya "Papa's Shadow," ambayo niliwahi kuielezea katika blogu hii.

Hiyo ni filamu iliyotokana na kozi niliyofundisha Tanzania mwaka 2013 iitwayo Hemingway in East Africa. Nilisafiri na wanafunzi 29 wa Chuo cha St. Olaf, tukazunguka maeneo kadhaa ya Tanzania kaskazini, ambamo alipita Ernest Hemingway mwaka 1933-34. Katika safari hiyo, tulikuwa tunasoma maandishi ya Hemingway kuhusu maeneo hayo na maeneo mengine ambayo alipitia mwaka 1953-54.

Maandishi hayo ni pamoja na Green Hills of Africa na Under Kilimanjaro, ambavyo ni vitabu, kadhalika hadithi fupi mbili: "The Short Happy Life of Francis Macomber" na "The Snows of Kilimanjaro." Pia aliandika makala katika magazeti na barua nyingi akielezea aliyoyaona na kufanya katika safari zake. Kwa ujumla wake, maandishi haya ya Ernest Hemingway yanaitangaza nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa namna ambayo sisi wenyewe hatujaweza kujitangaza.

Hiyo filamu ya "Papa's Shadow" inawasilisha vizuri mambo muhimu ya uhusiano wa Ernest Hemingway na Afrika Mashariki. Sehemu kubwa ya filamu hii ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway. Tunajadili kwa kina na mapana fikra za Ernest Hemingway kuhusu Afrika, uandishi, na maisha kwa ujumla.

Kwa kuwa hiyo filamu inaonyesha sehemu mbali mbali za Tanzania na maelezo kuhusu mambo yanayoifanya Tanzania kivutio kwa watalii, kama vile Mlima Kilimanjaro, na kwa kuwa filamu hii imejengeka katika maandishi ya Ernest Hemingway, mwandishi maarufu sana ulimwenguni, ni wazi kuwa filamu hii itakuwa chachu ya kuitangaza Tanzania kwa namna ya pekee. Taarifa zaidi Kuhusu "Papa's Shadow," zinapatikana kwenye tovuti ya Ramble Pictures.

Thursday, May 26, 2016

"The Snows of Kilimanjaro" Yatimiza Miaka 80

Mwaka huu 2016, The Snows of Kilimanjaro, hadithi maarufu ya Ernest Hemingway, inatimiza miaka 80 tangu ichapishwe kwa mara ya kwanza. Ilichapishwa katika jarida la Esquire, toleo la Agosti, 1936. Sidhani kama kuna hadithi fupi katika fasihi ya ki-Ingereza inayofahamika na ni maarufu kuzidi The Snows of Kilimanjaro.

Hemingway aliandika utangulizi mfupi wa hadithi yake, ambao unaamsha hisia zinazoendelezwa katika hadithi nzima, ikiwemo hisia ya masuali yasiyojibika:

"Kilimanjaro is a snow covered mountain 19,710 feet high, and it is said to be the biggest mountain in Africa. Its western summit is called the Masai "Ngáje Ngái," the House of God. Close to the western summit there is the dried and frozen carcass of a leopard. No one has explained what the leopard was seeking at that altitude." 

The Snows of Kilimanjaro inamhusu mtu aitwaye Harry, mzungu. Tunamwona akiwa mgonjwa kutokana na kidonda alichopata baada ya kuchomwa na mwiba porini. Kilichosababisha kidonda kufikia hali ya kutishia uhai wake ni kucheleweshwa kwa matibabu. Harry tunamwona amelala kwenye machela huku akihudumiwa na mkewe Helen, mzungu pia. Kuna pia watumishi wa-Afrika.

Mazingira inapotokea hadithi hii ni chini ya mlima Kilimanjaro. Lakini sehemu kubwa ya hadidhi ni kumbukumbu za Harry za mambo aliyofanya au kushuhudia sehemu mbali mbali za Ulaya, kama vile Paris, ikiwemo ushiriki wake katika vita. Juu ya yote, hadithi hii ni mtiririko wa fikra za Harry kuhusu uandishi. Tunamshuhudia akiwazia mengi ambayo alitaka aandike miaka iliyopita, au angependa kuwa ameandika, lakini hakuandika kwa sababu mbali mbali. Anajisikitikia kuwa sasa hataweza kuandika, kwani kifo kinamwelemea. Helen anafanya kila awezalo kumtuliza na kumpa matumaini kuwa atapona. Anamtunza na kujaribu kumzuia kujidhuru kwa ulevi. Anamweleza kuwa ndege itakuja kumwokoa.

Kwa kuwa huu ni mwaka wa kumbukumbu ya miaka 80 ya The Snows of Kilimanjaro, na kwa kuzingatia umaarufu wa Ernest Hemingway ulimwenguni, na umaarufu wa The Snows of Kilimanjaro, na kwa kuwa Mlima Kilimanjaro uko nchini mwetu, hii ilikuwa ni fursa ya kuitangaza nchi yetu. Niliwahi kuandika kidogo kuhusu jambo hili katika blogu hii. Ingekuwa wa-Tanzania tuna utamaduni wa kusoma na kuthamini vitabu, tungeichangamkia fursa ninayoelezea hapa.

Kuna mambo ambayo tungeweza kufanya. Wizara, taasisi na makampuni yanayohusika na utalii yangefurika matangazo na makala juu ya Hemingway na The Snows of Kilimanjaro. Wasomaji wa Hemingway, wanafasihi, na wengine tungekuwa tunafanya mijadala na makongamano. Vyombo vya habari, kama vile magazeti na televisheni, vingekuwa vinarusha matangazo na taarifa na mijadala hiyo. Huu ungekuwa mwaka wa kuitangaza nchi yetu na kuwavutia watalii nchini kwetu kwa namna ya pekee kabisa.

Kuna wenzetu ambao wanatumia jina na maandishi ya Hemingway kujitangaza na kuvutia watalii. Mifano ya wazi ni Cuba na mji wa Pamplona ulioko Hispania. Dunia ya leo ya ushindani mkubwa inahitaji ubunifu wa kwenda na wakati.  Dunia si ya kuichezea. Muyaka alitahadharisha hayo aliposema, "dunia mti mkavu, kiumbe siulemele" na tusijidanganye kuwa twaweza "kuudhibiti kwa ndole."

Thursday, September 24, 2015

"Papa's Shadow" Yapongezwa na Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa

Tarehe 20 mwezi huu nilipeleka ujumbe Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa kuhusu filamu ya Papa's Shadow. Sikuandika ujumbe mrefu, bali niliwatumia kiunganishi hiki.

Bila kuchelewa, tarehe 22 nilipata ujumbe kutoka kwao, ukiwa umeandikwa na Ndugu Noel Kabanda. Uwakilishi unaafiki kuwa Papa's Shadow ni "fursa maridhawa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni" na unasisitiza kuwa "Serikali inatambua mchango wa sanaa katika kuitangaza Tanzania katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii na utamaduni."

Kwanza, kwa kuzingatia uwingi wa majukumu yanayowakabili wawakilishi wetu katika balozi zetu, nimeona ni muhimu kusema nilivyoguswa na jinsi Uwakilishi ulivyoushughulikia ujumbe wangu.

Pili, ujumbe wa Uwakilishi unawatia moyo wahusika wa Ramble Pictures, ambao ndio watengeneaji wa Papa's Shadow. Timu nzima ya Ramble Pictures ni vijana wa ki-Marekani, na baadhi yao walikuja Tanzania mwaka 2013 kwenye kozi yangu ya Hemingway Katika Afrika Mashariki. Ni furaha kwangu, na jambo la kujivunia, kuwaeleza vijana hao kuwa Uwakilishi wa Kudumu waTanzania Umoja wa Mataifa umeipokea Papa's Shadow kwa namna hii.

Papa's Shadow si filamu ya maigizo. Ni filamu ya kuelimisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni maongezi baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa mwandishi Hemingway. Tunaongelea maisha ya Hemingway, safari zake, uandishi wake, na fikra zake kuhusu masuala mbali mbali. Tunawafungua macho walimwengu kuhusu namna Hemingway alivyoipenda Afrika na alivyokuwa mtetezi wa Afrika.

Hemingway alisafiri na kuishi Afrika Mashariki mara mbili, mwaka 1933-34 na 1953-54. Aliandika hadithi, insha, barua na maandishi mengine ambayo ni hazina kubwa. Wenzetu katika nchi zingine ambako Hemingway alipita au kuishi na akaandika habari za huko, wametumia fursa hiyo kujitangaza, na wanawavutia watalii wengi sana. Mifano ni miji kama Paris (Ufaransa), Havana (Cuba), Oak Park (Illinois, Marekani), Key West (Florida, Marekani), na Pamplona (Hispania). Hemingway anapendwa ulimwenguni kote ambako watu wana utamaduni wa kusoma vitabu. Sina shaka kuwa Papa's Shadow italeta msisimko wa aina hiyo kwa kuwaelekeza mashabiki wa Hemingway nchini kwetu.

Hamu ya kuona Tanzania inafunguka macho kuhusu fursa hii ilinihamasisha kufanya utafiti juu ya safari za Hemingway katika nchi yetu na maandishi aliyoandika. Kozi niliyotunga ilikuwa na lengo hili. Nilitaka pia kuwasaidia walimwengu kuelewa umuhimu wa Afrika katika maisha na uandishi wa Hemingway. Kwa msingi huo huo, nilishiriki kikamilifu katika kufanikisha filamu ya Papa's Shadow.

Nimeeleza hayo yote ili kuweka wazi umuhimu wa ujumbe wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa. Ni mfano wa mshikamano unaotakiwa baina yetu wanadiaspora, serikali, na wananchi wenzetu.

Wednesday, September 16, 2015

Filamu ya "Papa's Shadow:" Fursa ya Kuitangaza Tanzania

Nina furaha kuandika kuhusu filamu ambayo imeandaliwa iitwayo "Papa's Shadow," inayomhusu mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Katika filamu hiyo, ninaonekana nikiongea na Mzee Patrick Hemingway, ambaye ni mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliye hai. Ana umri wa miaka 87. Tunaongelea maisha, safari, maandishi na fikra za Hemingway, hasa kuhusu Afrika.

Sehemu nyingi hapa duniani ambako Hemingway alipita au kuishi na akaandika habari zake, zimejipatia umaarufu. na zinafaidika hasa katika utalii. Mifano ni Cuba na mji wa Pamplona nchini Hispania. Watu wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla tuna bahati hiyo, kwani Hemingway alikuja na kuishi kwetu mara mbili, mwaka 1933-34 na 1953-54, akaandika vitabu, hadithi, insha na barua kuhusu aliyoyaona.

Filamu ya "Papa's Shadow" ilitokana na kozi niliyofundisha Tanzania mwezi Januari mwaka 2013 juu ya Hemingway. Kozi ile ilimhamasisha Jimmy Gildea, mmoja wa wanafunzi wangu, kutengeneza filamu hiyo. Alianzisha kampuni, Ramble Pictures, akaanza kutegeneza hiyo filamu ya kuelimisha. Anaendelea kutengeneza filamu zingine zenye kuelimisha.

"Papa's Shadow" inaitangaza Tanzania kwa namna ya pekee. Kuna kampeni ya kuchangisha fedha za kumalizia malipo ya usajili na taratibu zingine kabla ya filamu kuonyeshwa na kusambazwa. Naleta hapa ujumbe ambao umeandikwa na binti yangu Zawadi, mmoja wa watu wanaojitolea katika Ramble Pictures, unaoelezea kampeni hiyo.

Nitapenda ujumbe huu uwafikie wa-Tanzania popote duniani, hasa wanadiaspora, ofisi za ubalozi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na wadau wengine wote. Nilitumia miaka kadhaa kusoma maandishi ya Hemingway na kuandaa kozi ambayo ni chimbuko la filamu hii. Ninapangia kuendelea kufundisha kozi hiyo. Nawe m-Tanzania mwenzangu una fursa ya kutoa mchango wako. Tushirikiane. Tutafanikiwa. Sisi tuliokuwepo wakati Tanganyika ilipopata Uhuru tunakumbuka kauli mbiu ya Mwalimu Nyerere ya kuhimiza maendeleo ya Taifa jipya: "It can be done; play your part."

=====================================================

Hello!

My name is Zawadi Mbele, and I am contacting you today to let you know about an amazing project. Ramble Pictures, a Minneapolis-based, independent film company, recently launched a 30-day "Kickstarter" campaign in order to raise funds for the distribution of our completed documentary, Papa's Shadow.

Papa's Shadow is a personal film about Ernest Hemingway in East Africa. It explores his hunting expeditions and holds key dialogues on subjects such as race, language, and the cultures that distinguish us as citizens of the world. Featuring exclusive testimony by Ernest's only living son, Patrick Hemingway, as well as Tanzanian author and Hemingway scholar, Dr. Joseph Mbele, this documentary explores the integral role of two safaris in their shaping of an author and demise of a legend. 

Over the past four years, hard work and creative energy has been poured into making this feature-length documentary. The film has already been completed, however, we cannot show or distribute the film until we finish paying for copyright licensing. Again, please visit our Kickstarter webpage to learn more about how you can play an important role in bringing this documentary to distribution. Also, with Kickstarter, we are offering exclusive rewards with every donation, such as the new Hemingway Library Edition of "Greens Hills of Africa," signed by Patrick Hemingway. 

If there is someone else from your organization you would recommend contacting, we would be grateful to have our information passed along. If you can, please take the time to explore our webpage and let me know if you have any questions at all. You can email me directly or email Elizabeth Turner at elizabeth@ramblepictures.com.

Thank you for your time, and we look forward to hearing back from you!

Sincerely,

Zawadi Mbele
email: zawadi.mbele@gmail.com

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...