Thursday, May 26, 2016

"The Snows of Kilimanjaro" Yatimiza Miaka 80

Mwaka huu 2016, The Snows of Kilimanjaro, hadithi maarufu ya Ernest Hemingway, inatimiza miaka 80 tangu ichapishwe kwa mara ya kwanza. Ilichapishwa katika jarida la Esquire, toleo la Agosti, 1936. Sidhani kama kuna hadithi fupi katika fasihi ya ki-Ingereza inayofahamika na ni maarufu kuzidi The Snows of Kilimanjaro.

Hemingway aliandika utangulizi mfupi wa hadithi yake, ambao unaamsha hisia zinazoendelezwa katika hadithi nzima, ikiwemo hisia ya masuali yasiyojibika:

"Kilimanjaro is a snow covered mountain 19,710 feet high, and it is said to be the biggest mountain in Africa. Its western summit is called the Masai "Ngáje Ngái," the House of God. Close to the western summit there is the dried and frozen carcass of a leopard. No one has explained what the leopard was seeking at that altitude." 

The Snows of Kilimanjaro inamhusu mtu aitwaye Harry, mzungu. Tunamwona akiwa mgonjwa kutokana na kidonda alichopata baada ya kuchomwa na mwiba porini. Kilichosababisha kidonda kufikia hali ya kutishia uhai wake ni kucheleweshwa kwa matibabu. Harry tunamwona amelala kwenye machela huku akihudumiwa na mkewe Helen, mzungu pia. Kuna pia watumishi wa-Afrika.

Mazingira inapotokea hadithi hii ni chini ya mlima Kilimanjaro. Lakini sehemu kubwa ya hadidhi ni kumbukumbu za Harry za mambo aliyofanya au kushuhudia sehemu mbali mbali za Ulaya, kama vile Paris, ikiwemo ushiriki wake katika vita. Juu ya yote, hadithi hii ni mtiririko wa fikra za Harry kuhusu uandishi. Tunamshuhudia akiwazia mengi ambayo alitaka aandike miaka iliyopita, au angependa kuwa ameandika, lakini hakuandika kwa sababu mbali mbali. Anajisikitikia kuwa sasa hataweza kuandika, kwani kifo kinamwelemea. Helen anafanya kila awezalo kumtuliza na kumpa matumaini kuwa atapona. Anamtunza na kujaribu kumzuia kujidhuru kwa ulevi. Anamweleza kuwa ndege itakuja kumwokoa.

Kwa kuwa huu ni mwaka wa kumbukumbu ya miaka 80 ya The Snows of Kilimanjaro, na kwa kuzingatia umaarufu wa Ernest Hemingway ulimwenguni, na umaarufu wa The Snows of Kilimanjaro, na kwa kuwa Mlima Kilimanjaro uko nchini mwetu, hii ilikuwa ni fursa ya kuitangaza nchi yetu. Niliwahi kuandika kidogo kuhusu jambo hili katika blogu hii. Ingekuwa wa-Tanzania tuna utamaduni wa kusoma na kuthamini vitabu, tungeichangamkia fursa ninayoelezea hapa.

Kuna mambo ambayo tungeweza kufanya. Wizara, taasisi na makampuni yanayohusika na utalii yangefurika matangazo na makala juu ya Hemingway na The Snows of Kilimanjaro. Wasomaji wa Hemingway, wanafasihi, na wengine tungekuwa tunafanya mijadala na makongamano. Vyombo vya habari, kama vile magazeti na televisheni, vingekuwa vinarusha matangazo na taarifa na mijadala hiyo. Huu ungekuwa mwaka wa kuitangaza nchi yetu na kuwavutia watalii nchini kwetu kwa namna ya pekee kabisa.

Kuna wenzetu ambao wanatumia jina na maandishi ya Hemingway kujitangaza na kuvutia watalii. Mifano ya wazi ni Cuba na mji wa Pamplona ulioko Hispania. Dunia ya leo ya ushindani mkubwa inahitaji ubunifu wa kwenda na wakati.  Dunia si ya kuichezea. Muyaka alitahadharisha hayo aliposema, "dunia mti mkavu, kiumbe siulemele" na tusijidanganye kuwa twaweza "kuudhibiti kwa ndole."

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...