
Pichani hapa kushoto ni jamaa wawili kutoka Guatemala. Niliwapa makala yangu fupi, "Chickens in the Bus," tukaongea kuhusu tamaduni zetu, tukaona jinsi zinavyofanana. Ni kawaida kuwaona watu Guatemala wakisafiri ndani ya basi wakiwa wamebeba kuku au hata nguruwe. Kwa mujibu wa mama mmoja Mmarekani aliyefika mezani pangu na kuiona makala hiyo, Mexico nako unaweza kuwaona watu ndani ya basi wakiwa na kuku au nguruwe.
Kama picha zangu zinavyoonyesha, tamasha lilihudhuriwa na watu wa tamaduni mbali mbali. Mji wa Rochester una watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kutoka Afrika, kwa mfano, kuna wa-Somali wengi katika mji huu.
Jumuia na taasisi mbali mbali za huduma za jamii ziliwakilishwa pia.
Pichani hapa kushoto ni meza iliyowakilisha Trinidad. Nilisogea hapo, nikaongea na huyu mama. Nilimwambia kuwa ninafahamu kiasi fasihi na utamaduni wa Trinidad, tukazungumza juu ya waandishi maarufu kama V.S. Naipaul, Sam Selvon, Shiva Naipaul, na Earl Lovelace.
Tulipomwongelea mwandishi Selvon, huyu mama aliniuliza kama nimesoma riwaya yake ya The Lonely Londoners, nami nikamweleza kuwa ni riwaya mojawapo ambayo naipenda sana, nimeifundisha mara nyingi.
Lengo la tamasha, kuwaleta watu wa mataifa na tamaduni za ulimwengu pamoja kwa ajili ya kufahamiana, kuelimishana, na kufurahia maonesho mbali mbali lilifanikiwa sana. Nimeandika taarifa ya tamasha hili katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Waandaji wa tamasha, Rochester International Association, wanastahili sifa na pongezi kwa kazi yao nzuri.
No comments:
Post a Comment