
Ninayo nakala nyingine ya Qur'an tangu mwaka 1982, ambayo ni tafsiri ya Abdullah Yusuf Ali. Hii ni kubwa kwa kuwa ina maelezo mengi. Hii mpya niliipata tarehe 28 Aprili, mwaka huu, kutoka kwa Dr. Nadia Mohamed, mzaliwa wa Misri.

Dr. Nadia Mohamed ni profesa mwenye shahada ya uzamili katika sheria za ki-Islam na shahada ya uzamifu katika elimu. Nilikuwa nimemwalika kuja kutoa mhadhara katika darasa langu la Muslim Women Writers, na baada ya kipindi ndipo alinipa Qur'an hiyo.
Tafsiri ni mtihani mkubwa, nami nimesema hivyo tena na tena katika blogu hii. Kwa kuwa hii Qur'an niliyopata karibuni ni tafsiri tofauti na ile ya Abdullah Yusuf Ali, ninategemea kufananisha hizi tafsiri mbili kutanisaidia kupata mwanga zaidi kuhusu yasemwayo katika Qur'an.
Ninasoma Qur'an sawa na ninavyosoma misahafu ya dini zingine kwa lengo la kujielimisha. Ninaamini kuwa ni muhimu kwa wanadamu kufahamiana ili tuweze kujenga maelewano miongoni mwetu. Kuzifahamu dini za wengine, tamaduni zao, na lugha zao ni njia ya kulifikia lengo hilo.
Ninapenda kusisitiza hilo, kwani nimeshakumbana na watu wanaodhani au kutegemea kwamba kwa kuwa ninasoma Qur'an, hatimaye nitasilimu. Sioni mantiki ya dhana hiyo. Je, ninaposoma msahafu wa dini ya Hindu, inamaanisha nitaacha u-Kristu niwe m-Hindu? Ninaposoma maandishi ya watu wanaozikana dini, kama vile akina Karl Marx, inamaanisha kuwa hatimaye nitaikana dini? Nimesoma fikra za Karl Marx na wapinzani wengine wa dini kwa zaidi ya miaka 40, na bado mimi ni m-Katoliki.
No comments:
Post a Comment