Monday, May 23, 2016

Hatimaye, Ninatafsiri Shairi la "Kibwangai"

Hivi karibuni, nililalamika katika blogu hii kuwa nilikuwa nikijaribu kutafsiri shairi la "Kibwangai" la Haji Gora Haji, lakini nilikwama. Shairi hili lililoandikwa kwa ki-Swahili linaeleweka vizuri kabisa kwangu. Lugha niliyotaka kulitafsiri shairi, yaani ki-Ingereza, ninaifahamu vizuri sana.

Sasa tatizo lilikuwa nini? Hili ni suala moja la msingi katika shughuli na taaluma ya tafsiri. Tafsiri sio suala la ufahamu wa lugha tu, bali ufahamu wa mambo mengine pia, ikiwemo lugha ya kifasihi. Unaweza kuwa unakijua ki-Ingereza, kwa mfano, lakini hujui ki-ingereza cha fasihi. Ukitafsiri shairi kama Kibwangai, utaishia kuleta kitu ambacho hakina ladha ya sanaa.

Hiyo dhana yenyewe ya ladha ya sanaa inahitaji ufafanuzi. Lugha, iwe ni ki-Swahili, ki-Ingereza, au lugha nyingine, ina matumizi ya kawaida na matumizi ya kisanaa. Kiswahili cha kishairi kinatofautiana na ki-Swahili cha kawaida. Vivyo hivyo ki-Ingereza.

Kwa hivi, mtu unapotafsiri shairi kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, unapaswa kufahamu matumizi ya kisanaa ya lugha zote mbili. Hapo ndipo mtu unapojikuta umekwama kama nilivyokwama siku kadhaa zilizopita.

Kukwama huku hakuwafiki wale wanaotafsiri tu, bali waandishi pia. Katika nadharia ya uandishi kuna kitu ambacho kwa ki-Ingereza huitwa "writer's block," yaani mkwamo wa kiuandishi. Hii ni hali ya mwandishi kujikuta amekwama asiweze kuandika. Akili haikubali kufanya kile anachotamani mwandishi. Ernest Hemingway aliwahi kuelezea hali hiyo:

There is no rule on how to write. Sometimes it comes easily and perfectly; sometimes it's like drilling rock and then blasting it out with charges.

Kwa ki-Swahili, anasema:

Hakuna sheria za namna ya kuandika. Wakati mwingine huwa ni rahisi na kwa ukamilifu; wakati mwingine huwa ni kama kutoboa mwamba na kisha kuupasua kwa milipuko.

Nimeandika utangulizi huu mrefu kwa kuwa tangu jana jioni nimejikuta katika hali ya kuweza kulitafsiri shairi la "Kibwangai." Jana nimetafsiri beti sita. Nimebakiza tano. Hata hivi, nikishamaliza, kitakachofuata ni kuipita tafsiri nzima kwa uangalifu, neno kwa neno. Hii nayo inaweza ikawa kazi ngumu ya kuumiza, sawa na kupasua mwamba.

KIBWANGAI

1.    Kuna hadithi ya kale, kwa babu nimepokeya
       Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya
       Nilikuwa mwanakele, hayo nikazingatiya
       Leo nawadokezeya, kwa nilivyoyafahamu

2.    Nyani bada kugundua, watu wanawaviziya
       Sababu yake kwa kuwa, huila yao mimeya
       Na ndipo wakaamuwa, mwenzao kumtumiya
       Ende akawalimiye, mazao yalo muhimu

3.    Kwenye uamuzi huo, baada ya kukusudiya
       Kibwangai jama yao, wakamkata mkiya
       Unyani kwa mbinu zao, kwake ukajitokeya
       Akawa yeye si nyani, bali ni binaadamu

4.    Yalisudi watakayo, nyani wakafurahiya
       Yaliposadifu hayo, wote wakachekeleya
       Walidhani watakayo, atawakamilishiya
       Nyoyo zikategemeya, na nyuso kutabasamu

5.    Pana mmoja kasema, Kibwangai kumwambiya
       Kama tutalokutuma, weza kututimiziya
       Isiwe kurudi nyuma, ewe mwenzetu sikiya
       Wewe tumekuchaguwa, utumikiye kaumu

6.    Kibwangai akasema, hayo nimezingatiya
       Kidete nitasimama, jitijada kutumiya
       Kwa kusia na kulima, mpate jifaidiya
       Sitobadili mawazo, ilipwe yangu kaumu

7.    Kibwangai lipoona, ni mtu kakamiliya
       Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya
       Wala hakujali tena, wenzake walomwambiya
       Akahisi hawi nyani, umbo lile litadumu

8.    Kawa na tabia moja, nyani walipomwendeya
       Akajifunga mkaja, mijiwe kuwarushiya
       Hakujali zao haja, wala kuwahurumiya
       Kapiga na kukemeya, pia na kuwashutumu

9.    Nyani likawakasiri,  ghadhabu wakaingiya
       Wakafanyiza shauri, Kibwangai kumwendeya
       Kwa nguvu au hiyari, kumpa wake mkiya
       Ili awe nyani tena, asiwe binaadamu

10.  Mkia bada kumpa, mambo yakawa mabaya
       Nguo zake kazitupa, unyani kumrudiya
       Kaanza kuchupa chupa, mitini akarukiya
       Akawafata wenzake, akiwa nyani katimu

11. Wenzake wakamcheka, wote na kumzomeya
       Akakosa la kushika, kwa haya kujioneya
       Majuto yakamfika, akabakia kuliya
       Akarudia porini, iliko yake kaumu.

No comments: