Saturday, May 14, 2016

Nimepita Tena Katika Duka la Half Price Books

Leo alasiri nilikwenda eneo la Minneapolis, mwendo wa maili 40, kwa shughuli binafsi. Ilikuwa siku nzuri, ya jua la wastani na hali ya hewa ya kupendeza. Wakati wa kurudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaamua kupitia katika duka la Half Price Books. Nilitaka hasa kuangalia kama kuna chochote juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Kufuatilia vitabu juu ya Hemingway imeshakuwa mazoea kwangu, wala siwezi kujizuia.

Ninajua kuwa sitakikuta kitabu kipya kilichoandikwa na Hemingway. Inafahamika kwamba miswada yote ya vitabu vya Ernest Hemingway imeshachapishwa. Kinachotokea ni kuwa yanachapishwa matoleo mapya ya vitabu vyake, kama vile matoleo yanayohaririwa na mjukuu wake, Sean Hemingway, ambavyo Mzee Patrick Hemingway, mtoto wa Ernest Hemingway, anaviandikia utangulizi.

Maandishi mapya kabisa ya Ernest Hemingway yanayochapishwa ni barua zake. Kuna mradi wa kukusanya barua zote za Ernest Hemingway tangu utotoni mwake. Wahariri wa mradi huu ni maprofesa Sandra Spanier na Robert W. Trogdon, ambao wamebobea katika utafiti juu ya Ernest Hemingway. Hadi sasa majuzuu matatu yamechapishwa, na kila juzuu ni mkusanyo wa barua za miaka michache. Inatarajiwa kuwa mradi huu ambao utachukua miaka mingi, utatoa majuzuu yatachapishwa 17.

Vitabu vingine vipya ambavyo vinaendelea kuchapishwa ni matokeo ya utafiti juu ya maisha na maandishi ya Ernest Hemingway. Tangu zamani, kumekuwa na watafiti wengi wanaojishughulisha na utafiti huu, na vitabu ambavyo wamechapisha na wanaendelea kuchapisha ni vingi. Si rahisi kwa mtu yeyote kufuatilia suala hili kikamilifu, lakini ninakuwa na duku duku ya kuona kuna vitabu gani vipya juu ya Hemingway katika duka la vitabu.

Nimefurahi leo kukikuta kitabu juu ya Hemingway ambacho sikuwa hata nimekisikia, The True Gen: An Intimate Portrait of Hemingway by Those Who Knew Him kilichoandikwa na Denis Brian. Katika kukipitia, niliona kuwa kitabu hiki ni taswira ya Hemingway inayotokana na kumbukumbu za watu waliomfahamu. Niliamua hapo hapo kukinunua. Baada ya kufika nyumbani, nimeanza kukisoma.  Kuna maelezo ya watu wengi, kuanzia wale waliokuwa watoto wakienda shule na mtoto Ernest Hemingway hadi waandishi, wake zake, na watu wengine.

Kama ilivyo kawaida, nilipokuwa hapo dukani Half Price Books niliwaona watu wengi humo wakizunguka zunguka kuangalia vitabu na kuvinunua. Wazazi wengi walikuwa na watoto wao. Kama kawaida, inavutia kuwaona watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa katika utamaduni wa kupenda vitabu.

Sikukaa sana humo. Baada ya kununua kitabu changu, niliona niwahi nyumbani nikaanze kukisoma.


No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...