Thursday, June 2, 2016

Tafsiri ya Ubeti wa Kwanza wa "Kibwangai"

Niliandika katika blogu hii kwamba ninatafsiri kwa ki-Ingereza shairi la Haji Gora Haji liitwalo "Kibwangai." Baada ya kukabiliana na matatizo katika kila ubeti, nimeshatafsiri beti zote kumi na moja, na leo nimeona nioneshe nilivyojaribu kutafsiri ubeti wa kwanza. Ubeti huo unasema hivi:

Kuna hadithi ya kale, kwa babu nimepokeya
Kwa manyani zama zile, mkasa ulotokeya
Nilikuwa mwanakele, hayo nikazingatiya
Leo nawadokezeya, kwa nilivyoyafahamu

Mstari wa kwanza una sehemu mbili, kama ilivyo mistari mingine yote katika ubeti huu. Niliutafsiri mstari wa kwanza namna hii: "There is an age-old story, I got from grandfather." Katika hizo sehemu mbili, sehemu ya kwanza haikunipa tatizo. Tatizo lilikuwa katika sehemu ya pili,  "kwa babu nimepokeya."

Mtu ukitaka kuhifadhi mpangilio wa sentensi kama ulivyo, unaweza, na tafsiri inaweza kuwa "from grandfather I received," au "from grandfather I got," au "from my grandfather I received," au "from my grandfather I got." Mtihani hapo ni kuchagua tafsiri ambayo unaona ina ladha nzuri masikioni, na ni fupi iwezekanavyo, kulingana kwa kadiri iwezekanavyo na ufupi wa "kwa babu nimepokeya." Shairi limeandikwa kwa namna ya kubana matumizi ya maneno. Kwa kuzingatia hayo, nikaona tafsiri yangu ya mstari wa kwanza iwe "There is an age-old story, I got from grandfather."

Mstari wa pili ulikuwa ni mtihani pia. Kwanza niliutafsiri hivi, "To the monkeys that time, a calamity came down." Lakini baada ya siku kadhaa, nimebadili tafsiri hiyo na kuifanya iwe, "Among the monkeys that time, a calamity came down." Ningefurahi zaidi iwapo ningesema "Among the monkeys long ago," kwani "long ago" ni usemi uliozoeleka katika hadithi. Lakini nimeona nizingatie usemi wa "zama zile" kama ulivyo.

Hata hivi, tafsiri ya hiyo sehemu ya pili hainiridhishi, kwani kiuhalisi, tafsiri ya "mkasa ulotokeya" kwa kuzingatia ubeti ulivyoanza, ni "a calamity that occured." Sasa, kama ningetafsiri hivi, ningeharibu mantiki ya sentensi ya ki-Ingereza. Hapo tunaona jinsi muundo wa sentensi katika lugha moja unavyohitaji kuwa tofauti katika lugha nyingine ili tafsiri iwe ipasavyo.

Jambo jingine linalonifanya nisiridhike na tafsiri ya huu mstari wa pili ni pana zaidi, kwani maana kamili ya mistari miwili ya kwanza ya shairi hili ni "There is an age-old story I got from my grandfather, about a calamity that occured among the monkeys long ago."

Baada ya juhudi yote hii, leo nimepata wazo kuwa badala ya kutumia neno "story," nitumie "tale." Kwa hivi, baada ya kuandika makala hii, nitabadili tafsiri. Badala ya "There is an age-old story," itakuwa "There is an age-old tale."

Mstari wa tatu ulikuwa mgumu. Mwanzoni niliutafsiri hivi, "Mere child that I was, I kept this in mind." Lakini leo asubuhi nimeamua kubadilisha na kuwa "Though I was still a child, I kept it all in mind." Naona tafsiri hii ya leo ina mtiririko mzuri zaidi. Hiyo ni hisia yangu, na wengine wanaweza wakawa na hisia tofauti.

Mstari wa mwisho nao umekuwa mgumu sana kuutafsiri. Kwanza niliutafsiri hivi, "And today I am imparting to you, the things I understood." Lakini tafsiri hii haikuniridhisha. Sikuona namna ya kutafsiri "nawadokezeya" ambayo ingependeza masikioni. Ningeweza kutumia neno "hinting," lakini maana halisi ya neno hili katika mustakabali wa shairi hili si kudokeza tu, kwani inasimuliwa hadithi nzima.

Kwa hivi, matumizi ya neno "nawadokezeya" yanaleta utata, kwani shairi lenyewe si dokezo tu bali ni hadithi nzima. Narejea kwenye dhana ya Cleanth Brooks kwamba lugha ya ushairi ni "language of paradox." Na kwa kweli, mtiririko wa shairi la Kibwangai limejengeka katika misingi ya "paradox." Hilo suala nategemea kulifafanua siku za usoni.

Baada ya kuutafakari huu mstari wa mwisho wa "Kibwangai," leo nimefikia uamuzi wa kuutafsiri hivi "Today I share with you, of what I understood." Tafsiri hii inaweza kuwa inapwaya kidogo, kwa namna mbili. Kwanza, maana halisi ya "Leo nawadokezeya," ikiwa nje ya shairi hili, ni "Today I am hinting to you." Lakini, kama nilivyosema, shairi halidokezi tu, bali linasimulia hadithi nzima. Pili, kwa kuwa mshairi katumia dhana ya kudokeza, na mimi sikutaka kuififisha kabisa dhana hiyo, nimeamua kutumia "of what I understood." Kwa kufanya hivyo, huenda nimeleta mkanganyiko juu ya mkanganyiko.

Nategemea kuwa maelezo yangu haya, ingawa mafupi, na yanahusu ubeti moja tu, yanathibitisha kuwa kutafsiri shairi au kazi za fasihi kwa ujumla ni mtihani ambao unaweza kuumiza kichwa na bado usiwe na ufumbuzi wa kuridhisha. Pamoja na hayo yote, hadi hii leo, tafsiri yangu ya ubeti wa kwanza wa "Kibwangai" ni hii:

There is an age-old tale, I got from grandfather
Among the monkeys that time, a calamity came down
Though I was still a child, I kept it all in mind
Today I share with you, of what I understood.2 comments:

********** said...

Shikamoo mwalimu,

Asante kwa elimu hii uliyotupa ya kutafsiri shairi la mzee Gora. Mzee Gora ni Gwiji hasa.Bado nakumbuka ulipokuja Taasisi Zanzibar kuonana na Mzee Gora. Nitakutumia picha tuliyopiga.

Mbele said...

Ndugu

Shukrani kwa ujumbe wako. Umenikumbusha ziara yangu ile, na ukarimu wenu watu wa Visiwani. Mzee Gora ana fikra za kina na pana na kipaji kikubwa cha utunzi. Ni hazina kwa Taifa letu na ulimwengu.

Nakushukuru kwa kuniandikia, na kwa wazo lako la kuniletea picha. Ubarikiwe sana.