Friday, June 17, 2016

Maktaba ya John F. Kennedy

Wanasema tembea uone. Siku chache zilizopita, nilikwenda Boston kwenye maktaba ya John F. Kennedy kuendelea na utafiti wangu juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Maktaba hii ina hifadhi kubwa kuliko zote duniani za maandishi na kumbukumbu zingine zinazohusiana na mwandishi huyu.

Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kuitembelea maktaba hii, ingawa taarifa zake nilikuwa ninazifahamu na picha za jengo hili nilikuwa nimeziona mtandaoni. Nilijisikia vizuri nilipolikaribia jengo hili na kuingia ndani, nikafanya utafiti kama nilivyogusia katika blogu hii.

Katika kutafakari ziara hii, nimekuwa nikiwazia tofauti iliyopo baina yetu wa-Tanzania na wenzetu wa-Marekani katika kuwaenzi waandishi wetu maarufu. Je, sisi tumefanya nini kuhifadhi, kwa mfano, kumbukumbu za Shaaban Robert? Tuna mkakati gani wa kutafuta na kukusanya miswada yake. Huenda iko, sehemu mbali mbali. Mfano ni barua zake ambazo zilizohifadhiwa na mdogo wake Yusuf Ulenge, kisha zikachapishwa.

Lakini je, tumefanya juhudi gani za kutafuta barua zingine za Shaaban Robert, labda na marafiki na washirika wake, kwa wachapishaji wake, kama vile Witwatersrand University Press. Tumefanya juhudi gani kutafuta miswada ya mashairi yake na ya vitabu vyake, huko kwa wachapishaji wake, kama hao Watersrand University Press, Macmillan, Thomas Nelson, na kadhalika?

Tumefanya juhudi gani kuvitafuta vitu vingine vyovyote vya Shaaban Robert, kama walivyofanya na wanavyoendelea kufanya wa-Marekani juu ya waandishi wao, kama huyu Ernest Hemingway? Ninasema hivi kwa sababu ninafahamu kuwa hifadhi kama hii ya Ernest Hemingway bado inaendelea kutafuta na kupokea kumbukumbu zaidi, kama vile barua. Sijui, labda iko siku tutaamka usingizini.

No comments: