
Niliangalia sehemu vinapowekwa, nikaviona vitabu ambavyo ninavifahamu. Lakini, kuna kimoja ambacho sikuwa ninakifahamu, Paris Without End: The True Story of Hemingway's First Wife. kilichotungwa na Gioia Diliberto. Ninafahamu kiasi habari za huyu mke, ambaye jina lake ni Hadley, na nilimtaja siku chache zilizopita katika blogu hii. Niliwazia kukinunua, lakini badala yake niliamua kununua kitabu cha By-Line cha Ernest Hemingway, ingawa nilishanunua nakala miaka kadhaa iliyopita, bali niliiacha Dar es Salaam mwaka 2013.

Mtu mwingine anaweza kuhoji mantiki ya kununua nakala ya kitabu ambacho tayari ninacho, lakini kwangu hii si ajabu. Nakala iliyoko Dar es Salaam ina jalada jepesi, niliyonunua leo ina jalada gumu. Hiyo kwangu ni sababu tosha. Jambo la zaidi ni kuwa kuna vitabu ambavyo napenda niwe navyo mwenyewe nilipo, hata kama ningeweza kuviazima maktabani. Hii si ajabu, kwani kila binadamu ana mambo yake anayoyapenda na yuko tayari kuyagharamia.
No comments:
Post a Comment