Sunday, June 26, 2016

Nilivyokutana na Askofu Yakobo Komba (Yafunani)

Kati ya mambo ninayoyakumbuka sana ya ujana wangu ni jinsi nilivyokutana na Askofu Yakobo Komba, ambaye sasa ni marehemu. Alikuwa anajulikana zaidi kwa jina la Yafunani, ambalo ni jina la baba yake. Nilikutana na kuongea naye mwaka 1970, nilipokuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika seminari ya Likonde, mkoani Ruvuma, Tanzania.

Baada ya kusoma shule ya msingi Litembo, 1959-62, nilijiunga na seminari ya Hanga, mkoani Ruvuma, 1963-66, na baadaye seminari ya Likonde, 1967-70. Seminari hizi ni za Kanisa Katoliki. Zilikuwa zinachagua wanafunzi waliojipambanua kimasomo na kitabia katika shule zao. Pamoja na masomo ya kawaida ya shule zingine nchini, tulikuwa tunaandaliwa kuwa mapadri.

Kwa miaka yetu ile, ili kuwa padri ilikuwa lazima mtu afaulu masomo ya angalau kidatu cha nne, na baada ya hapo alikwenda kusomea falsafa na teolojia katika seminari kuu, kwa miaka kadhaa. Kanisa Katoliki lilihakikisha kuwa mapadri wana elimu ya shuleni kuizidi jamii waliyokuwa wanaihudumia. Miaka ile, elimu ya kidato cha nne ilikuwa ni elimu ya juu.

Nilipokuwa Hanga na Likonde, nilikuwa ninapenda sana kusoma. Kila siku, wakati wa mapumziko, nilikuwa napenda kwenda maktabani kusoma. Ninavyokumbuka, Hanga na Likonde zilikuwa na maktaba kubwa kuliko shule nyingine mkoani Ruvuma.

Kutokana na tabia yangu ya kusoma sana, nilifahamu mambo mengi, na nilikuwa na tabia ya kuwaelezea wanafunzi wengine mambo niliyokuwa ninayapata katika majarida, vitabu, na magazeti. Nilikuwa ninafahamu mambo kuhusu Kanisa Katoliki katika nyanja za historia na siasa ambayo hayakuniridhisha. Hayo sikuwa nawaambia wengine.

Yaliyonikera zaidi ni mawili. Kwanza ni matamko ya Papa ya karne kadhaa zilizopita kuruhusu uvamizi na uporaji wa nchi za mbali uliokuwa ukifanywa na mataifa ya Ulaya. Pili ni msimamo wa kanisa nchini Msumbiji juu ya harakati za ukombozi zilizokuwa zinaendelea nchini humo. Kanisa nchini Msumbiji lilikuwa likiwaasa waumini kutojihusisha na harakati za ukombozi.

Nilianza kuwa na mashaka kama kweli nitaweza kuwa padri. Nilifadhaika sana. Niliogopa kumwambia mkuu wa shule kuwa ninasita kuendelea na njia ya upadri. Niliogopa wazazi wangu, ambao walikuwa wa-Katoliki wa dhati, watajisikiaje. Nilisongwa sana na mawazo. Kilikuwa ni  kipindi kigumu sana kimawazo katika maisha yangu. Sikuwa na raha.

Siku zilivyokwenda, tukiwa kidato cha nne, nilijua kuwa itafika siku lazima ukweli ujulikane. Nilijipiga moyo konde, nikaenda kwa mkuu wa shule na kumweleza kwa kifupi kuwa ninajisikia kuwa sina wito wa upadre. Kama ninakumbuka vizuri, alinijibu vizuri akanishauri niendelee kutafakari.

Siku moja, ndipo akaja Askofu Yakobo Komba shuleni Likonde. Wote tulikuwa tunamwogopa sana. Niliingiwa na hofu kubwa mkuu wa shule aliponiambia kuwa  Askofu amekuja kuongea nami. Nilikuwa sijawahi kuongea na Yafunani ana kwa ana.

Nilikwenda ofisini. Nilishangaa alivyonipokea kwa utulivu. Ninakumbuka maneno aliyoniambia. Daima yamekuwa akilini mwangu. Alisema: Waalimu wako wamekuwa wakiniambia kuwa wewe ndiye mwanafunzi unayeongoza darasani, nami nilikuwa natarajia kuwa ukishakuwa padri, uwe sekretari wangu. Lakini walimu wameniarifu kuwa umebadili mawazo kuhusu upadri. Ingawa nilikuwa na mategemeo, Mungu ndiye anayejua na kuongoza. Tafadhali, kokote utakakoenda, zingatia kuishi na kufanya kazi kwa uaminifu kufuatana na mapenzi ya Mungu.

Kusema kweli, sikuamini kama huyu aliyekuwa anaongea nami kwa utulivu na upendo ni huyu huyu Yafunani tuliyekuwa tunamwogopa. Maneno yake na nasaha zake zilinituliza kabisa moyo wangu. Tangu hapo, niliishi nikiwa na utulivu wa moyo na mawazo. Niliendelea na kazi zangu za kusoma, kujiandaa kwa mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne. Tulifanya mtihani ule mwaka 1970, na matokeo yalipofika nilishika nafasi ya kwanza katika kufaulu katika seminari ya Likonde.

Ninavyokumbuka hayo, ninatambua wazi kuwa mambo ya kanisa yaliyonikera miaka ile hayako leo. Kanisa lilichukua mwelekeo wa kukiri makosa ya zamani, na kubadilika. Misimamo ya Kanisa Katoliki leo haina utata kwangu, bali ni ya kujivunia. Mfano halisi ni Laudato Si, waraka wa kichungaji wa Papa Francis.

No comments: