Thursday, June 9, 2016

Kitabu Andika Kwa Ajili Yako

Mara kwa mara ninapata ujumbe kutoka kwa watu wanaohitaji ushauri kuhusu uandishi wa vitabu. Baadhi wanakuwa wameshaandika miswada na wanatafuta ushauri kuhusu kuchapisha vitabu.

Wengine, baada ya kupata ushauri wangu ambao kwa kawaida unahusu uchapishaji wa mtandaoni, wanaulizia utaratibu wa malipo. Yaani wanataka kujua watalipwaje kutokana na mauzo ya vitabu vyao.

Ninakaribisha maulizo kuhusu masuala haya ya uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu, kama ninavyothibitisha katika blogu hii. Hapa ninapenda kusema neno la jumla kwa watu hao, hasa wanaowazia mauzo na malipo: kitabu andika kwa ajili yako.

Nimeona kuwa watu wana kiherehere cha kuchapisha vitabu na kuviuza, wajipatie fedha. Wanaamini kuwa wakishachapisha kitabu, kuna utitiri wa watu watakaonunua, na wao waandishi watajipatia fedha, na labda fedha nyingi.

Kwa ujumla, hii ni ndoto. Kwanza, ni waandishi wachache sana duniani wanaopata fedha kutokana na vitabu vyao za kutosha hata kumudu gharama za kawaida za maisha. Pili, tutafakari hali halisi ya mwamko wa jamii katika suala la kununua na kusoma vitabu. Je, tuna utamaduni wa kununua na kusoma vitabu? Wewe mwenyewe unanunua na kusoma vitabu? Kama sivyo, una sababu gani au una haki gani ya kudhani kuwa wengine watanunua kitabu chako?

Pamoja na yote hayo, ni kweli kuwa kama unaandika vitabu vinavyoitwa vya udaku, au vya mambo ya kusisimua hisia, kama vile mapenzi, kuna uwezekano kuwa vitanunuliwa. Lakini hivi ni vitabu vya msimu, au vitabu vya chap chap, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Havina thamani ya kuvifanya vidumu kama vinavyodumu vitabu vya akina William Shakespeare, Charles Dickens, Leo Tolstoy, au Shaaban Robert. Waandishi wa vitabu vya msimu wanaweza kujipatia fedha kiasi.

Kuna aina nyingine ya waandishi ambao nao wanaweza kujipatia fedha. Hao ni waandishi wanaofuata jadi mbaya ambayo imekuwepo Tanzania, ya watu kuandika vitabu na kuvisukumia mashuleni. Mashule yamekuwa kama majalala ya kupokea vitabu kiholela. Wahusika wanatafuta fedha na wanafunzi wanaathirika, kwa kuwa vitabu hivi havikidhi viwango vya hali ya juu kabisa vya taaluma na uandishi sahihi.

Tukiachilia mbali aina hizi za uandishi, tutafakari uandishi wa vitabu vya kuelimisha jamii, ambavyo havisukumwi na mahitaji ya shule. Tutafakari vitabu ambavyo mwandishi makini mwenye ujuzi fulani anaandika ili kuelezea yale anayoyajua kwa umahiri wote awezao. Ni aina ya uandishi unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi ya mwandishi, kiasi kwamba hawezi kutulia bila kuhitimisha kazi ya kujikomboa kutokana na msukumo huo.

Uandishi huo huwa ni kwa manufaa ya mwandishi mwenyewe. Ninaamini kuwa huo ndio uandishi wa dhati. Ndio uandishi wa kweli. Kitabu cha namna hiyo kikishachapishwa, haijalishi kama kinanunuliwa na kusomwa na yeyote. Mwandishi unakuwa umetua mzigo. Umejikomboa, na uko tayari kuanza shughuli nyingine, kama vile kuandika kitabu kingine.

Binafsi, nina ajenda yangu ya vitabu ninavyotaka kuandika. Siangalii kama vitasomwa au kama vitatumika mashuleni. Kuna vitabu vya fasihi ambavyo nimevisoma, ambavyo ninaviandikia tahakiki, kwa kupenda mimi mwenyewe, wala si kwa kusukumwa na mahitaji ya wengine.

Kwa mfano, kwa miaka mingi nilikuwa ninatafakari utungo wa Okot p'Bitek, uitwao Song of Lawino, na kuandika mawazo yangu, hadi hivi karibuni nikachapisha mwongozo, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Vile vile, nilishawahi kuandika katika blogu hii kuwa ninataka kuandika mwongozo kuhusu kitabu cha Camara Laye kiitwacho The African Child. Ninaridhika kabisa na mtazamo wangu kwamba kitabu andika kwa ajili yako mwenyewe, na dhana hii nimeigusia kabla katika blogu hii.


1 comment:

NN Mhango said...

Usemayo ndugu Mbele ni kweli. Mimi huingiza fedha nyingi toka kwenye Makala zangu magazeti kuliko nipatazo toka kwenye vitabu vyangu. Kuna rafiki yangu mwandishi nguli aliwahi kunilaumu kwanini napoteza muda kuandika vitabu wakati havilipi kama Makala. Nilimjibu kuwa siandiki kwa ajili ya fedha bali kipawa; maana nisipofanya hivyo huenda hata nikafa. Hakunielewa. Nilipomwambia kuwa nina nyumba kadhaa na nimeridhika na nilicho nacho ila sijaridhika na nilichokwisha weka kwenye vitabu alishangaa Zaidi.
Kwa ufupi ni kwamba uandishi wa vitabu si utajiri wa fedha bali maarifa. Mimi nimeishaandika vitabu saba, vitatu vya kiada ambayo vingine vimeanza kufundishwa vyuoni na vinne ya kubuni. Ninachotegemea kupata ni mawazo yangu kuishi hata baada ya mimi kutoweka lakini si fedha. Ukitaka utajiri andika vitabu vya kipuuzi na udaku vyenye kupotesha na kujaa uzushi lakini si vitabu fikirishi au vya kiada.