Saturday, June 25, 2016

Ninasoma "A Moveable Feast"

Nina tabia ya kusoma vitu vingi bila mpangilio, na niliwahi kutamka hivyo katika blogu hii. Kwa siku, naweza kusoma kurasa kadhaa za kitabu fulani, kurasa kadhaa za kitabu kingine, makala hii au ile, na kadhalika. Sina nidhamu, na sijui kama kuna umuhimu wa kuwa na nidhamu katika usomaji.

Siku kadhaa zilizopita, niliandika katika blogu hii kuhusu vitabu nilivyochukua katika safari yangu ya Boston. Nilisema kuwa kitabu kimojawapo kilikuwa A Moveable Feast cha Ernest Hemingway. Ni kweli, nilikuwa ninakisoma, sambamba na vitabu vingine, makala na kadhalika. Matokeo yake ni kuwa inachukua muda kumaliza kitabu.

A Moveable Feast ni kitabu kimojawapo maarufu sana cha Hemingway. Wako wahahiki wanaokiona kuwa kitabu bora kuliko vingine vya Hemingway, ingawa wengine wanataja vitabu tofauti, kama vile A Farewell to Arms, For Whom the Bell Tolls, na The Old Man and the Sea. Hemingway alikuwa mwandishi bora kiasi kwamba kila msomaji anaona chaguo lake.

Ninavyosoma A Moveable Feast, ninaguswa na umahiri wa Hemingway wa kuelezea mambo, kuanzia tabia za binadamu hadi mandhari za mahali mbali mbali. Picha ninayopata ya mji wa Paris na maisha ya watu katika mji huo miaka ya elfu moja mia tisa na ishirini na kitu haiwezi kusahaulika. Ni tofauti na picha ya Paris tuliyo nayo leo.

Hemingway haongelei maisha ya starehe na ulimbwende. Watu wanaishi maisha ya kawaida, na wengine, kama yeye mwenyewe na mke wake Hadley, wanaishi maisha ya shida. Mara kwa mara Hemingway anaongelea alivyokuwa na shida ya hela, ikambidi hata mara moja moja kuacha kula ili kuokoa hela.

Inasikitisha kusikia habari kama hizi, lakini pamoja na shida zake, Hemingway anasisitiza kwamba Paris ulikuwa mji bora kwa mwandishi kuishi. Anasema kuwa gharama za maisha hazikuwa kubwa. Alikuwa na fursa ya kuwa na waandishi maarufu waliomsaidia kukua katika uandishi, kama vile Gertrude Stein, Ezra Pound, na Scott Fitzgerald.

A Moveable Feast, kama vile Green Hills of Africa, ni kitabu chenye kuongelea sana uandishi na waandishi. Hemingway anatueleza alivyokuwa anasoma, akitegemea fursa zilizokuwepo, kama vile duka la vitabu la Shakespeare and Company lililomilikiwa na Sylvia Beach. Anatuambia alivyowasoma waandishi kama Turgenev, Tolstoy, D.H. Lawrence, na Anton Chekhov. Anatueleza alivyokuwa anajadiliana na wengine kuhusu waandishi hao.

Hayo, kama nilivyogusia, yananikumbusha Green Hills of Africa, ambamo kuna mengi kuhusu uandishi na waandishi. Katika Green Hills of Africa, tunamsikia Hemingway akiongelea uandishi hasa katika mazungumzo yake na mhusika aitwaye Koritchner. Vitabu kama A Moveable Feast vinatajirisha akili ya msomaji. Si vitabu vya msimu, bali ni urithi wa kudumu kwa wanadamu tangu zamani vilipoandikwa hadi miaka ya usoni.

Toleo la A Moveable Feast ninalosoma ni jipya ambalo limeandaliwa na Sean Hemingway. Toleo la mwanzo liliandaliwa na Mary Welsh Hemingway, mke wa nne wa Hemingway. Kutokana na taarifa mbali mbali, ninafahamu kuwa kuna tofauti fulani baina ya matoleo haya mawili, hasa kuhusu Pauline, mke wa pili wa Hemingway. Sean Hemingway amerejesha maandishi ya Hemingway juu ya Pauline ambayo Mary hakuyaweka katika toleo lake. Bahati nzuri ni kuwa miswada ya kitabu chochote cha Hemingway imehifadhiwa, kama nilivyojionea katika maktaba ya JF Kennedy.

Jambo moja linalonivutia katika maandishi ya Hemingway ni jinsi anavyorudia baadhi ya mambo kutoka andiko moja hadi jingine, iwe ni kitabu au hadithi, insha au barua. Kwa namna hiyo, tunapata mwanga fulani juu ya mambo yaliyokuwa muhimu mawazoni mwa Hemingway. Mfano moja ni namna Hemingway anavyoelezea athari mbaya za fedha katika uandishi. Mwandishi anaposukumwa au kuvutwa na fedha au mategemeo ya fedha anaporomoka kiuandishi. Dhana hiyo ya Hemingway inanikumbusha waliyosema Karl Marx na Friedrich Engels katika The Communist Manifesto, yakaongelewa pia na wengine waliofuata mwelekeo wa ki-Marxisti, kama vile Vladimir Ilyich Lenin.


No comments: