Thursday, November 20, 2014

Ninasoma Vitabu Kiholela

Jana, baada ya kufundisha darasa langu la South Asian Literature, nilikuwa ofisini kwa muda, nikawa napekuapekua bila lengo maalum katika makabati ya vitabu vyangu. Niliamua, kiholela tu, kuchukua tamthilia ya Macbeth ya Shakespeare, nikarudi nayo nyumbani na kuanza kuisoma.

Nilikuwa na hamu ya kujikumbusha enzi za ujana wangu, nilipokuwa nasoma sekondari hadi chuo kikuu. Nilipenda kusoma vitabu vya waandishi mbali mbali, kama vile Shakespeare na Charles Dickens.

Leo asubuhi, nilipoamka, niliendelea kusoma Macbeth, lakini nikakumbuka kuwa kuna vitabu kadhaa ambavyo nilianza kuvisoma au nilikuwa navisoma siku kadhaa zilizopita, au wiki kadhaa zilizopita, au miezi kadhaa iliyopita, ambavyo sikuvimaliza. Mifano ni A Moveable Feast na Islands in the Stream, vilivyoandikwa na Ernest Hemingway; Lost For Words, kilichoandikwa na J.W. Patrick Creber, na Nomad, kitabu cha Ayaan Hirsi, yule dada m-Somali anayetishiwa maisha yake kwa vile anaukosoa u-Islam. Hiyo ni mifano tu ya viporo.

Wakati kuna viporo, inatokea mara kwa mara kuwa naanza kusoma kitabu kingine kabisa na kukimaliza. Hivi ndivyo ilivyokuwa niliposoma The Pearl, kitabu cha John Steinbeck. Nilikiongelea kitabu hiki katika blogu hii, hapa na hapa. Nilikianza nikakimaliza, huku viporo kadhaa ninavyo.

Pamoja na yote hayo, jana nimekurupuka na kuanza kusoma Macbeth. Kwa hakika, nimepania kumaliza kuisoma tamthilia hii, ingawa nimeichagua kiholela tu. Hakuna uhakika kuwa kesho na keshokutwa sitaanza kusoma kitabu kingine tofauti kabisa. Kusema kweli, jana hiyo hiyo nilianza pia kusoma kitabu cha Postcolonial Criticism, kilichohaririwa na Bart Moore-Gilbert na wengine ambacho nilikinunua miaka kadhaa iliyopita, nikawa nimechunguliachungulia tu kurasa zake, bila kukisoma.

Leo nimejikuta nikitafakari tabia yangu hii kama msomaji. Siongelei vitabu ninavyofundisha darasani. Hivyo huwa navisoma kwa nidhamu, tangu ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, kama impasavyo mwalimu, na ninawaongoza wanafunzi katika kuvijadili. Hii tabia ya kusoma vitabu kiholela inahusu vitabu ambavyo ninajisomea mwenyewe, bila msukumo kutoka kokote. Najiuliza kama ni jambo jema kusoma vitabu kiholela.

Lakini, papo hapo, sioni ubaya wake. Wakati huja ambapo napata hamu ya kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikiweka kando siku zilizopita. Ajabu ni kuwa, ninapoamua kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikianza siku zilizopita nikakiweka kando, kumbukumbu hunijia kuhusu yale niliyosoma kabla.

Naamini kila msomaji wa vitabu ana tabia yake katika usomaji. Nimeona nitafakari tabia yangu na kuieleza kama nilivyofanya. Labda hii itawapa wasomaji wengine fursa ya kujitafakari pia.

No comments: