Showing posts with label A Moveable Feast. Show all posts
Showing posts with label A Moveable Feast. Show all posts

Saturday, June 25, 2016

Ninasoma "A Moveable Feast"

Nina tabia ya kusoma vitu vingi bila mpangilio, na niliwahi kutamka hivyo katika blogu hii. Kwa siku, naweza kusoma kurasa kadhaa za kitabu fulani, kurasa kadhaa za kitabu kingine, makala hii au ile, na kadhalika. Sina nidhamu, na sijui kama kuna umuhimu wa kuwa na nidhamu katika usomaji.

Siku kadhaa zilizopita, niliandika katika blogu hii kuhusu vitabu nilivyochukua katika safari yangu ya Boston. Nilisema kuwa kitabu kimojawapo kilikuwa A Moveable Feast cha Ernest Hemingway. Ni kweli, nilikuwa ninakisoma, sambamba na vitabu vingine, makala na kadhalika. Matokeo yake ni kuwa inachukua muda kumaliza kitabu.

A Moveable Feast ni kitabu kimojawapo maarufu sana cha Hemingway. Wako wahahiki wanaokiona kuwa kitabu bora kuliko vingine vya Hemingway, ingawa wengine wanataja vitabu tofauti, kama vile A Farewell to Arms, For Whom the Bell Tolls, na The Old Man and the Sea. Hemingway alikuwa mwandishi bora kiasi kwamba kila msomaji anaona chaguo lake.

Ninavyosoma A Moveable Feast, ninaguswa na umahiri wa Hemingway wa kuelezea mambo, kuanzia tabia za binadamu hadi mandhari za mahali mbali mbali. Picha ninayopata ya mji wa Paris na maisha ya watu katika mji huo miaka ya elfu moja mia tisa na ishirini na kitu haiwezi kusahaulika. Ni tofauti na picha ya Paris tuliyo nayo leo.

Hemingway haongelei maisha ya starehe na ulimbwende. Watu wanaishi maisha ya kawaida, na wengine, kama yeye mwenyewe na mke wake Hadley, wanaishi maisha ya shida. Mara kwa mara Hemingway anaongelea alivyokuwa na shida ya hela, ikambidi hata mara moja moja kuacha kula ili kuokoa hela.

Inasikitisha kusikia habari kama hizi, lakini pamoja na shida zake, Hemingway anasisitiza kwamba Paris ulikuwa mji bora kwa mwandishi kuishi. Anasema kuwa gharama za maisha hazikuwa kubwa. Alikuwa na fursa ya kuwa na waandishi maarufu waliomsaidia kukua katika uandishi, kama vile Gertrude Stein, Ezra Pound, na Scott Fitzgerald.

A Moveable Feast, kama vile Green Hills of Africa, ni kitabu chenye kuongelea sana uandishi na waandishi. Hemingway anatueleza alivyokuwa anasoma, akitegemea fursa zilizokuwepo, kama vile duka la vitabu la Shakespeare and Company lililomilikiwa na Sylvia Beach. Anatuambia alivyowasoma waandishi kama Turgenev, Tolstoy, D.H. Lawrence, na Anton Chekhov. Anatueleza alivyokuwa anajadiliana na wengine kuhusu waandishi hao.

Hayo, kama nilivyogusia, yananikumbusha Green Hills of Africa, ambamo kuna mengi kuhusu uandishi na waandishi. Katika Green Hills of Africa, tunamsikia Hemingway akiongelea uandishi hasa katika mazungumzo yake na mhusika aitwaye Koritchner. Vitabu kama A Moveable Feast vinatajirisha akili ya msomaji. Si vitabu vya msimu, bali ni urithi wa kudumu kwa wanadamu tangu zamani vilipoandikwa hadi miaka ya usoni.

Toleo la A Moveable Feast ninalosoma ni jipya ambalo limeandaliwa na Sean Hemingway. Toleo la mwanzo liliandaliwa na Mary Welsh Hemingway, mke wa nne wa Hemingway. Kutokana na taarifa mbali mbali, ninafahamu kuwa kuna tofauti fulani baina ya matoleo haya mawili, hasa kuhusu Pauline, mke wa pili wa Hemingway. Sean Hemingway amerejesha maandishi ya Hemingway juu ya Pauline ambayo Mary hakuyaweka katika toleo lake. Bahati nzuri ni kuwa miswada ya kitabu chochote cha Hemingway imehifadhiwa, kama nilivyojionea katika maktaba ya JF Kennedy.

Jambo moja linalonivutia katika maandishi ya Hemingway ni jinsi anavyorudia baadhi ya mambo kutoka andiko moja hadi jingine, iwe ni kitabu au hadithi, insha au barua. Kwa namna hiyo, tunapata mwanga fulani juu ya mambo yaliyokuwa muhimu mawazoni mwa Hemingway. Mfano moja ni namna Hemingway anavyoelezea athari mbaya za fedha katika uandishi. Mwandishi anaposukumwa au kuvutwa na fedha au mategemeo ya fedha anaporomoka kiuandishi. Dhana hiyo ya Hemingway inanikumbusha waliyosema Karl Marx na Friedrich Engels katika The Communist Manifesto, yakaongelewa pia na wengine waliofuata mwelekeo wa ki-Marxisti, kama vile Vladimir Ilyich Lenin.


Thursday, November 20, 2014

Ninasoma Vitabu Kiholela

Jana, baada ya kufundisha darasa langu la South Asian Literature, nilikuwa ofisini kwa muda, nikawa napekuapekua bila lengo maalum katika makabati ya vitabu vyangu. Niliamua, kiholela tu, kuchukua tamthilia ya Macbeth ya Shakespeare, nikarudi nayo nyumbani na kuanza kuisoma.

Nilikuwa na hamu ya kujikumbusha enzi za ujana wangu, nilipokuwa nasoma sekondari hadi chuo kikuu. Nilipenda kusoma vitabu vya waandishi mbali mbali, kama vile Shakespeare na Charles Dickens.

Leo asubuhi, nilipoamka, niliendelea kusoma Macbeth, lakini nikakumbuka kuwa kuna vitabu kadhaa ambavyo nilianza kuvisoma au nilikuwa navisoma siku kadhaa zilizopita, au wiki kadhaa zilizopita, au miezi kadhaa iliyopita, ambavyo sikuvimaliza. Mifano ni A Moveable Feast na Islands in the Stream, vilivyoandikwa na Ernest Hemingway; Lost For Words, kilichoandikwa na J.W. Patrick Creber, na Nomad, kitabu cha Ayaan Hirsi, yule dada m-Somali anayetishiwa maisha yake kwa vile anaukosoa u-Islam. Hiyo ni mifano tu ya viporo.

Wakati kuna viporo, inatokea mara kwa mara kuwa naanza kusoma kitabu kingine kabisa na kukimaliza. Hivi ndivyo ilivyokuwa niliposoma The Pearl, kitabu cha John Steinbeck. Nilikiongelea kitabu hiki katika blogu hii, hapa na hapa. Nilikianza nikakimaliza, huku viporo kadhaa ninavyo.

Pamoja na yote hayo, jana nimekurupuka na kuanza kusoma Macbeth. Kwa hakika, nimepania kumaliza kuisoma tamthilia hii, ingawa nimeichagua kiholela tu. Hakuna uhakika kuwa kesho na keshokutwa sitaanza kusoma kitabu kingine tofauti kabisa. Kusema kweli, jana hiyo hiyo nilianza pia kusoma kitabu cha Postcolonial Criticism, kilichohaririwa na Bart Moore-Gilbert na wengine ambacho nilikinunua miaka kadhaa iliyopita, nikawa nimechunguliachungulia tu kurasa zake, bila kukisoma.

Leo nimejikuta nikitafakari tabia yangu hii kama msomaji. Siongelei vitabu ninavyofundisha darasani. Hivyo huwa navisoma kwa nidhamu, tangu ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho, kama impasavyo mwalimu, na ninawaongoza wanafunzi katika kuvijadili. Hii tabia ya kusoma vitabu kiholela inahusu vitabu ambavyo ninajisomea mwenyewe, bila msukumo kutoka kokote. Najiuliza kama ni jambo jema kusoma vitabu kiholela.

Lakini, papo hapo, sioni ubaya wake. Wakati huja ambapo napata hamu ya kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikiweka kando siku zilizopita. Ajabu ni kuwa, ninapoamua kuendelea kusoma kitabu ambacho nilikianza siku zilizopita nikakiweka kando, kumbukumbu hunijia kuhusu yale niliyosoma kabla.

Naamini kila msomaji wa vitabu ana tabia yake katika usomaji. Nimeona nitafakari tabia yangu na kuieleza kama nilivyofanya. Labda hii itawapa wasomaji wengine fursa ya kujitafakari pia.

Wednesday, December 5, 2012

Barua za Ernest Hemingway, 1907-1922

Leo nimekipata kitabu cha barua za Hemingway ambacho nilikitaja katika blogu hii siku chache zilizopita. Kama nilivyoandika, nilikiona kwa mara ya kwanza katika duka la vitabu hapa Chuoni St. Olaf. Lakini nakala ile ilinunuliwa hima, ikabidi niagize.

Hemingway alikuwa mwandishi makini wa barua. Hata mwanae, Mzee Patrick Hemingway, amethibitisha hivyo. Kwa ujumla, Hemingway hakutaka wala kutarajia kuwa barua zake zichapishwe. Alikuwa na mazoea ya kuandika barua zake kwa uwazi na hata kutumia lugha ambayo inaonekana kali au yenye kukiuka maadili.

Baada ya Hemingway kufariki, mwaka 1961, suala la kuchapisha au kutochapisha maandishi ya Hemingway ambayo alikuwa hajayachapisha lilijitokeza na kuwa kubwa. Maandishi yake mengine alikuwa hajamaliza kuyarekebisha. Barua zake alikuwa hajaazimia zichapishwe. Suala likawa nini kifanyike.

Wasomaji wa maandishi ya Hemingway walisukumwa na kiu ya kutaka kusoma maandishi yake yote. Wahariri na watafiti walitaka hivyo pia. Familia yake ilikuwa katika mtihani mgumu. Lakini hatimaye, iliamuliwa kuwa bora kuchapisha maandishi hayo, hata barua zake. Ndivyo tulivyovipata vitabu vya Hemingway kama vile The Garden of Eden, Islands in the Stream, A Moveable Feast, na Under Kilimanjaro. Ni matokeo ya maamuzi magumu, na juhudi za wahariri kuhariri miswada aliyoicha Hemingway ikiwa haijakamilika, wakiongozwa na wazo kwamba bila shaka Hemingway mwenyewe angeafiki uhariri huo.

Tunaposoma vitabu hivi bado tunajiuliza iwapo kama Hemingway angeishi zaidi, angerekebisha vipi maandishi haya, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa mwandishi mwenye nidhamu ya hali isiyo ya kawaida katika kusahihisha na kuboresha maandishi yake. Alitaka kila neno liwe mahali pake na liwe kweli ni neno hilo, si jingine, na kila sentensi iwe imekamilika kwa kiwango cha juu kabisa.

Leo nilitaka nikumbushie pia kitabu cha barua za Shaaban Robert, ambacho niliandika habari zake katika blogu hii. Nilitaka nivijadili vitabu hivi vya barua kwa pamoja, kuelezea umuhimu wa vitabu vya aina hii, ambamo tunapata kuwafahamu waandishi hao maarufu kupitia njia ya barua walizoandika. Barua hizi ni kioo muhimu cha kutuwezesha kuyafahamu mambo ambayo pengine hatungeyafahamu kwa kuangalia tu vitabu vyao vingine. Nangojea nipate wasaa wa kuandika na kuzihusianisha barua za Hemingway na zile za Shaaban Robert.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...