Hapa Marekani, mtu unapoalikwa kwenda kutoa mhadhara, nawe ukakubali, huwa unaulizwa malipo yako ni kiasi gani. Hapo unawatajia kiwango cha malipo unayotegemea. Unazingatia umaarufu wako, na wale wanaokualika wanategemea uwatajie kiwango chako bila maneno zaidi. Hata siku chache zilizopita, nilipoletewa mwaliko wa kwenda kutoa mhadhara mjini Zumbrota, niliulizwa malipo yangu ni kiasi gani.
Miaka yapata mitano iliyopita, kwa nyakati tofauti, nilipata wasaa wa kuongea na wa-Marekani wawili wenye wadhifa katika jamii kuhusu suala hili. Tulikuwa katika mazungumzo kuhusu shughuli zangu za uandishi na utoaji mihadhara katika jumuia na taasisi mbali mbali. Ndipo wakaja na hili wazo la malipo. Ingawa waliongea nami kwa nyakati tofauti, wote walisema kuwa kufuatana na umaarufu niliokuwa nao wakati ule, nilikuwa na haki ya kutegemea kiasi cha dola 2,500 au 3,000 kwa mhadhara.
Kwangu, huu umekuwa ni mtihani miaka yote. Sijaweza kutaja hata siku moja nilipwe kiasi gani. Ukiniuliza sababu zangu, unaweza kushangaa au kunionea huruma. Imekuwa ni kawaida yangu, ninapoulizwa malipo yangu ni kiasi gani, kusema kuwa suala hili nawaachia wanaonialika. Waamue wenyewe wana uwezo gani, nami sitakuwa na tatizo.
Imekuwa hivyo miaka yote. Sibagui wenye pesa na wasio na pesa, au wenye pesa nyingi na wenye pesa kidogo. Nikialikwa kutoa mhadhara, ninakwenda, ili mradi mhadhara hauingiliani na ratiba yangu ya masomo.
Kuna vikundi ambavyo vina hela kidogo tu, au havina. Kwangu hiki si kipingamizi. Ninazingatia kuwa uwezo nilio nao umetoka kwa Mungu, na nina wajibu wa kuutumia kwa faida ya wanadamu. Wako ambao wana uwezo wa kunilipa, tena vizuri kabisa, lakini sijawa tayari kuwaweka kando wale ambao hawana hela za kunilipa. au wale wenye uwezo mdogo. Ninapokea chochote ambacho wameamua kipo katika uwezo wao. Na kama hawana uwezo, nawaambia kabisa kuwa hiki kwangu sio kizuizi.
Wa-Marekani wananishangaa kwa msimamo huo, kwani hauendani na utamaduni waliouzoea. Lakini mimi nafuata dhamiri yangu. Kama watu wengine wengi, nina mahitaji makubwa ya fedha. Wale wanaoishi Marekani wanajua kuwa hii ni nchi ya madeni kila upande, na hayamaliziki. Hasa wakati huu, ambao nimekuwa katika matibabu kwa miezi mingi, pesa hazishikiki, na pamoja na kuwa na bima nzuri, madeni ni mpaka shingoni.
Lakini hayo yote hayajanifanya nibadili msimamo wangu kuhusu malipo ya mihadhara yangu. Ningekuwa nataja angalau hizo dola 2,500 au 3,000 kwa kila mhadhara, ningekuwa sina madeni, na labda ningeanza kuwa tajiri.
Roho yangu haiko huko.Nawashangaa mafisadi waroho wanaokwapua mabilioni ya hela za nchi yetu, wakati wananchi wana dhiki zisizosemeka, kama vile hospitali zisizo na vifaa na madawa, na madaktari na wahudumu wanateseka kwa kutolipwa wanavyostahili. Nawashangaa mafisadi hao kwa jinsi walivyo waroho wa pesa, na wasivyo na huruma, wakati watoto wengi mashuleni hawana viti wala madawati, wala vitabu, na mazingira ya walimu yanasikitisha.
Hapo juu nimeongelea malipo halali, ambayo naambiwa ningeweza kuyataja kwa wale wanaonialika. Lakini bado roho yangu inasita. Lazima niwashangae mafisadi, ambao hawachukui malipo halali, bali wanaliibia Taifa bila huruma.
Nimewazia kwa miezi mingi kuandika ujumbe huu, lakini sikujua niuandikeje. Leo nimeamua kuandika. Labda kuna wadau wenye ushauri wa kunipa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment