Showing posts with label kuuza vitabu. Show all posts
Showing posts with label kuuza vitabu. Show all posts

Thursday, June 9, 2016

Kitabu Andika Kwa Ajili Yako

Mara kwa mara ninapata ujumbe kutoka kwa watu wanaohitaji ushauri kuhusu uandishi wa vitabu. Baadhi wanakuwa wameshaandika miswada na wanatafuta ushauri kuhusu kuchapisha vitabu.

Wengine, baada ya kupata ushauri wangu ambao kwa kawaida unahusu uchapishaji wa mtandaoni, wanaulizia utaratibu wa malipo. Yaani wanataka kujua watalipwaje kutokana na mauzo ya vitabu vyao.

Ninakaribisha maulizo kuhusu masuala haya ya uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu, kama ninavyothibitisha katika blogu hii. Hapa ninapenda kusema neno la jumla kwa watu hao, hasa wanaowazia mauzo na malipo: kitabu andika kwa ajili yako.

Nimeona kuwa watu wana kiherehere cha kuchapisha vitabu na kuviuza, wajipatie fedha. Wanaamini kuwa wakishachapisha kitabu, kuna utitiri wa watu watakaonunua, na wao waandishi watajipatia fedha, na labda fedha nyingi.

Kwa ujumla, hii ni ndoto. Kwanza, ni waandishi wachache sana duniani wanaopata fedha kutokana na vitabu vyao za kutosha hata kumudu gharama za kawaida za maisha. Pili, tutafakari hali halisi ya mwamko wa jamii katika suala la kununua na kusoma vitabu. Je, tuna utamaduni wa kununua na kusoma vitabu? Wewe mwenyewe unanunua na kusoma vitabu? Kama sivyo, una sababu gani au una haki gani ya kudhani kuwa wengine watanunua kitabu chako?

Pamoja na yote hayo, ni kweli kuwa kama unaandika vitabu vinavyoitwa vya udaku, au vya mambo ya kusisimua hisia, kama vile mapenzi, kuna uwezekano kuwa vitanunuliwa. Lakini hivi ni vitabu vya msimu, au vitabu vya chap chap, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii. Havina thamani ya kuvifanya vidumu kama vinavyodumu vitabu vya akina William Shakespeare, Charles Dickens, Leo Tolstoy, au Shaaban Robert. Waandishi wa vitabu vya msimu wanaweza kujipatia fedha kiasi.

Kuna aina nyingine ya waandishi ambao nao wanaweza kujipatia fedha. Hao ni waandishi wanaofuata jadi mbaya ambayo imekuwepo Tanzania, ya watu kuandika vitabu na kuvisukumia mashuleni. Mashule yamekuwa kama majalala ya kupokea vitabu kiholela. Wahusika wanatafuta fedha na wanafunzi wanaathirika, kwa kuwa vitabu hivi havikidhi viwango vya hali ya juu kabisa vya taaluma na uandishi sahihi.

Tukiachilia mbali aina hizi za uandishi, tutafakari uandishi wa vitabu vya kuelimisha jamii, ambavyo havisukumwi na mahitaji ya shule. Tutafakari vitabu ambavyo mwandishi makini mwenye ujuzi fulani anaandika ili kuelezea yale anayoyajua kwa umahiri wote awezao. Ni aina ya uandishi unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi ya mwandishi, kiasi kwamba hawezi kutulia bila kuhitimisha kazi ya kujikomboa kutokana na msukumo huo.

Uandishi huo huwa ni kwa manufaa ya mwandishi mwenyewe. Ninaamini kuwa huo ndio uandishi wa dhati. Ndio uandishi wa kweli. Kitabu cha namna hiyo kikishachapishwa, haijalishi kama kinanunuliwa na kusomwa na yeyote. Mwandishi unakuwa umetua mzigo. Umejikomboa, na uko tayari kuanza shughuli nyingine, kama vile kuandika kitabu kingine.

Binafsi, nina ajenda yangu ya vitabu ninavyotaka kuandika. Siangalii kama vitasomwa au kama vitatumika mashuleni. Kuna vitabu vya fasihi ambavyo nimevisoma, ambavyo ninaviandikia tahakiki, kwa kupenda mimi mwenyewe, wala si kwa kusukumwa na mahitaji ya wengine.

Kwa mfano, kwa miaka mingi nilikuwa ninatafakari utungo wa Okot p'Bitek, uitwao Song of Lawino, na kuandika mawazo yangu, hadi hivi karibuni nikachapisha mwongozo, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Vile vile, nilishawahi kuandika katika blogu hii kuwa ninataka kuandika mwongozo kuhusu kitabu cha Camara Laye kiitwacho The African Child. Ninaridhika kabisa na mtazamo wangu kwamba kitabu andika kwa ajili yako mwenyewe, na dhana hii nimeigusia kabla katika blogu hii.


Tuesday, July 28, 2015

Kitabu Umechapisha, Kazi ni Kukiuza

Pamoja na kuandika vitabu, ninajitahidi kujielimisha kuhusu masuala yanayohusiana na uchapishaji, utangazaji, na uuzaji wa vitabu. Kwa bahati nzuri, kuna vitabu vingi na vingine vinaendelea kuchapishwa, na pia makala nyingi kuhusu masuala hayo.

Napenda kuongelea suala la kukiuza kitabu. Niliwahi kuongelea suala hili katika blogu hii. Nimeliongelea pia katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Ni suali linalonigusa na kunifikirisha daima, nami napenda kuwashirikisha waandishi wengine katika kulitafakari.

Usemi kwamba chema chajiuza, kibaya chajitembeza unaweza kuwa na mantiki nzuri kuhusiana na vitabu. Wateja wakiridhishwa au kufurahishwa na kitabu, hawakosi kuwaambia wengine. Aina hii ya utangazaji, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "word of mouth," ni muhimu sana.

Mimi mwenyewe nimeshuhudia hivyo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Tangu nilipokichapisha kitabu hiki, mwaka 2005, wasomaji wamekuwa wakiwaambia wengine. Kwa lugha ya mitaani, wanakipigia debe.

Waandishi wengi hawajui kuwa baada ya kuchapisha kitabu, wana jukumu la kukitangaza na kukiuza. Wengi wanamtegemea mchapishaji afanye kazi hiyo. Hakuna shaka kwamba mchapishaji hujitahidi kukitangaza kitabu. Anawajibika kufanya hivyo, kwani anatafuta fedha za kugharamia uchapishaji, kuwalipa wafanyakazi wake, na kujipatia faida.

Lakini, waandishi tunapaswa kuona mbali zaidi. Kwanza, tusijiziuke. Mchapishaji hawezi kufanya kila kitu, hata kama angependa. Gharama za kukitangaza kitabu ni kipingamizi kwa mchapishaji, hasa yule ambaye si tajiri.

Pili, dunia inabadilika muda wote, nasi tunawajibika kujifunza mambo mapya muda wote. Leo hii kuna tekinolojia zinazomwezesha mwandishi kujichapishia kitabu chake. Katika mazingira haya, mwandishi anawajibika kubeba jukumu la kutangaza na kuuza kitabu. Si busara kutegemea "word of mouth" pekee.

Haikuwa rahisi kwangu kuanza kuvitangaza vitabu vyangu. Kutokana na malezi, mila na desturi, nilijiuliza italeta picha gani katika jamii iwapo ningekuwa natangaza na kuuza vitabu vyangu. Nilielezea wasi wasi huo katika blogu hii, na jinsi nilivyojikomboa.

Leo sioni tatizo kutangaza vitabu vyangu. Nimejifunza na ninaendelea kujifunza umuhimu na mbinu za kufanya hivyo, kwa kusoma vitabu na makala mbali mbali. Ndio maana mara kwa mara naandika katika blogu hii kuhusu matamasha ya vitabu ninayoshiriki. Kusoma kumenileta katika upeo huu mpya. Elimu ni mkombozi.

Saturday, May 9, 2015

Neno Jingine Kuhusu Uandishi na Uchapishaji

Mimi ni mwandishi wa vitabu. Ninaandika vitabu vya tahakiki ya fasihi, juu ya masuala ya jamii, fasihi simulizi, na masuala ya athari za tofauti za tamaduni, hali halisi ya uandishi wa vitabu, mbinu za kujichapishia vitabu. Naandika kuhusu utangazaji na uuzaji wa vitabu, na kuhusu hali halisi ya usomaji wa vitabu Tanzania na ughaibuni.

Ninatoa ushauri kwa wengine kupitia blogu hii na katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Yeyote anayetaka kujifunza kutoka kwangu anaweza kufanya hivyo, bila kipingamizi. Lakini namtegemea aanze kwa kusoma nilichoandika, mawasiano ya ziada yafuate baadaye.

Siwezi kuwasiliana na kila mtu na kuongelea hata yale ambayo tayari nimeshaandika. Nina kazi yangu na majukumu mengine kila siku. Nikisema niwasiliane na kila mtu hata kwa yale ambayo nimeshaandika, nitashindwa kufanya kazi zangu zinazoniwezesha kuishi, kulipia nyumba, matibabu, na mahitaji mengine.

Labda niache kazi niliyoajiriwa kufanya, nijiajiri kama mshauri. Ikiwa hivyo, kila anayetafuta ushauri kwangu atatakiwa alipie. Ndivyo wanavyofanya watoa ushauri. Nami ujuzi na uzoefu ninao, kama inavyodhihirika katika taarifa ninazoandika katika blogu hii ya hapakwetu na blogu ya ki-Ingereza.

Suali ambalo ninaulizwa tena na tena ni kuhusu mikakati ya kuchapisha miswada. Ni wazi kuwa watu bado wana fikra za jadi kuhusu uchapishaji. Nawashauri waondokane na fikra za kuwateemea wachapishaji. Badala yake, waingie katika ulimwengu wa kujichapishia vitabu.

Wafanyeje au waanzie wapi ndio aima ya masuala ninayoongelea katika blogu na katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Kama mtu anataka mafanikio, ni lazima awekeze katika elimu inayohusiana na shughuli anayotaka kufanya. Kununua vitabu na kuvisoma ni uwekezaji, sawa na uwekezaji wa kununua trekta ya kilimo au nyavu za kuvulia samaki.

 Suala la kujichapishia vitabu ni tata, hasa kwa upande wa wanataaluma. Jadi iliyopo katika kuchapisha vitabu vya kitaaluma au makala za kitaaluma imekuwa ya kuzingatia umuhimu wa wanataaluma tofauti na mwandishi kufanya uhakiki na udhibiti wa andiko kabla ya kuchapishwa. Ninapangia kuandika zaidi kuhusu suala hilo.  

Saturday, February 28, 2015

Kitabu Kinapoingia Amazon

Kati ya majina yanayojulikana sana mtandaoni ni Amazon, duka la mtandaoni ambamo vinapatikana vitu mbili mbali. Wengi wetu, kama sio wote, tunalihusisha jina la Amazon na vitabu.

Wanunuaji wa vitabu mtandaoni moja kwa moja huwazia duka la Amazon. Mimi mwenyewe, katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki, nimezoea kuulizwa na watu iwapo vitabu yangu vinapatikana Amazon. Hao ni watu ambao wangependa kununua vitabu vyangu ila hawana hela wakati huo. Waandishi wanaitegemea Amazon kama sehemu ya kuuza vitabu kwa urahisi, hasa ikizingatiwa kwamba Amazon imejijenga sehemu nyingi za dunia.

Binafsi, sikutaka kuviweka vitabu vyangu Amazon. Sikupendezwa na jinsi kampuni hii kubwa inavyowaharibia biashara wauzaji wadogo wadogo, kama yanavyofanya makampuni makubwa katika mfumo wa ubepari.

Nilitaka vitabu vyangu viuzwe na maduka madogo madogo, ya watu wa kawaida au taasisi za kawaida. Niliridhika kuona vitabu yangu vinauzwa na duka la vitabu la Chuo cha St. Olaf, kwa mfano.

Lakini, nilikuja kushangaa baadaye kuwa, ingawa sikuvipeleka vitabu yangu Amazon, vilianza kuonekana kule. Hapo nilitambua kuwa Amazon ina nguvu au mvuto kuliko nilivyodhania. Ni kama kifaru anayetembea nyikani bila kubughudhiwa na wanyama wadogo wadogo.

Amazon inauza vitabu vipya na pia nakala zilizotumika. Mtu akishanunua na kusoma nakala yake, anaweza kuiuza Amazon. Ukiangalia tovuti ya Amazon, utaona vitabu vyangu vipya vinauzwa sambamba na vilivyotumika.

Kutokana na hali halisi ya ushindani katika uchumi wa kibepari, Amazon inauza au inaweza kuuza vitabu kwa bei ya chini kidogo au sana, ukifananisha na wauzaji wengine, kuanzia wachapishaji hadi hasa wauzaji wadogo wadogo. Vile vile, malipo ("royalties") anayopata mwandishi kutokana na mauzo ya vitabu vyake Amazon huwa ni pungufu kuliko yale ayapatayo au anayoweza kuyapata kutoka kwa wachapishaji, ingawa nayo si makubwa, bali ni asilimia ndogo ya bei ya kitabu.

Pamoja na yote hayo, Amazon imetamalaki katika uwanja huu wa uuzaji wa vitabu mtandaoni. Ingawa kuna makampuni mengine pia, kama vile Barnes and Noble, Amazon ndio inayoonekana kutawala vichwani mwa watu.

Amazon inauza vitabu halisi, yaani vya karatasi, na vitabu pepe. Ni juu ya mwandishi kuamua kama anataka kukiweka kitabu chake katika mtindo wa kielektroniki. Inavyoonekana, kadiri siku zinavyopita, watu wengi zaidi na zaidi wanaingia katika mkondo huu wa kununua vitabu pepe. Mimi mwenyewe nimeshuhudia hayo, na nimekuwa nikijitahidi kwenda na wakati. Baadhi ya vitabu vyangu vinapatikana kama vitabu pepe kwenye mtandao wa lulu na mtandao wa Amazon.

Hata hivi, kuna mjadala mkubwa unaoendelea kuhusu hatima ya vitabu tulivyovizoea, yaani vya karatasi. Wakati wengine wanaamini kuwa vitabu hivi vitadidimizwa na vitabu pepe, wengine wanasema kuwa hilo halitawezekana, kutokana na mazoea na mapenzi yaliyojengeka kwa vitabu kama vitabu. Wanasema kuwa hivi vitabu vya jadi vitakuwepo sambamba na hivi vya kielektroniki.

Nimeona niseme hayo, kwa manufaa ya wengine ambao ni waandishi au wanawazia kuwa waandishi.

Friday, January 23, 2015

Kwa Anayewazia Kuchapisha Kitabu

Wazo la kuchapisha kitabu linawavutia watu wengi. Ni wazo lenye ndoto za mafanikio.Wako wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawapa umaarufu. Kuna wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawaletea fedha nyingi. Wengi, labda wote, wanaamini kuwa wakisha chapisha kitabu, kazi yao inakuwa imemalizika; kinachobaki ni kungojea matokeo, kama vile umaarufu na fedha.

Ni bora mtu anayewazia kuchapisha kitabu ajielimishe zaidi kuhusu jambo hili, nami hupenda kuchangia yale ninayoyafahamu, kwa kadiri ya uwezo wangu. Vipengele ni vingi, lakini hapa nitaongelea vichache tu.

Mtu uandike kitabu kutokana na kujua kuwa una jambo la kusema kimaandishi. Uwe una jambo ambalo linakuelemea akilini mwako na kukusukuma uandike. Msukumo utoke ndani ya nafsi yako. Ukishaandika kitabu kwa msingi huo, utajisikia una raha sawa na mtu aliyetua mzigo. Kuridhika kwako ndilo jambo mihimu. Mengine yanafuata baadaye.

Huenda kitabu chako kitawavutia watu wakakinunua na kukisoma, au huenda kisiwavutie. Lakini sidhani kama hili ni tatizo lako, maadam umeshakidhi haja ya kutua mzigo uliokuwemo akilini mwako, na sasa uko huru kuwazia mambo mengine. Uhuru huu ni jambo muhimu.

Katika miaka yangu ya kuandika, na hata kuchapisha vitabu, nimekuwa nikisoma kuhusu uandishi, uchapishaji na uuzaji wa vitabu. Kitu kimoja mihimu nilichojifunza ni kuwa kuandika na kuchapisha kitabu sio mwisho wa kazi yako kama mwandishi. Kuna kazi kubwa mbele yako, kazi ya kuutangazia ulimwengu kuhusu kuwepo kwa kitabu chako, na kazi ya kukiuza kitabu chako.

Watafiti na waandishi wa masuala hayo wanasisitiza kuwa wajibu wa kuuza kitabu ni yako wewe mwandishi. Kabla ya kuanza kusoma mawazo haya, niliamini, kama wengi wanavyoamini, kwamba kazi ya kutangaza na kuuza kitabu ni ya mchapishaji. Kumbe, hata kama mchapishaji anaweza kuchangia katika jukumu hilo, mwandishi unawajibika sana, na pengine zaidi kuliko mchapishaji.

Kwa upande wa Tanzania, kwa hali ilivyo, tatizo kubwa ni kwamba utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ni hafifu sana. Watu wengi wanadhani kusoma vitabu ni shughuli ya wanafunzi, na hivi vitabu viwe vimo katika mitaala ya shule.

Kujisomea vitabu bila shinikizo la shule au mitihani ni utamaduni ambao unakosekana. Hii ni sababu moja inayonifanya nitoe angalizo kuwa mtu unaweza kuchapisha kitabu na kisiwe na wasomaji.

Masuala haya ya uandishi na uuzaji wa vitabu nimeyaelezea katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, na katika makala mbali mbali katika blogu hii. Ninaendelea kujielimisha kuhusu masuala hayo, na nitaendelea kuandika.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...