Leo nimeona niandike kuhusu jinsi nilivyoanza kuuza vitabu vyangu. Naamini habari yangu itawasaidia waandishi wengine.
Mimi ni mwalimu, mtafiti, na mwandishi. Nimeshachapisha vitabu kadhaa. Lakini napenda niongelee vitabu viwili: Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.
Nilichapisha Matengo Folktales mwaka 1999 hapa Marekani. Lazima nikiri kuwa mara baada ya kitabu kutoka, sikuwa na furaha sana. Ingawa nilikuwa nimetumia yapata miaka 23 kukiandaa kitabu hiki, na ingawa kutokana na ujuzi wangu wa taaluma hii nilijua kuwa ni kitabu muhimu, sikuwa na raha kilipotoka mtamboni. Kwa namna isiyoelezeka, nilijiuliza kama watu watakionaje. Vile vile nilifahamu kuwa, ingawa nilikuwa nimechoka kabisa kukiboresha kitabu hiki, kama ningeendelea kukishughulikia, ningeweza kukiboresha zaidi. Uandishi ndivyo ulivyo. Huwezi ukafikia hatua ya kusema kitabu chako kimekamilika, hakina upungufu wowote, na hakiwezi kuboreshwa zaidi.
Hata hivi, wasomaji walipoanza kunieleza kuhusu kitabu hiki, nilianza kupata hisia tofauti, kwani walikipenda kwa namna moja au nyingine. Basi nilianza kutulia, na kukiacha kitabu kiendelee kuwepo na kusambaa duniani. Mwaka 2005 nilichapisha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Kitabu hiki kinapigiwa debe na watu wengi, taasisi, vyuo, ma mashirika kama vile Global Service Corps, shirika la kiMarekani linalowaleta watu wa kujitolea huko Tanzania.
Nilianza kujifunza zaidi habari za uuzaji wa vitabu. Kama waandishi wengine, nilikuwa nadhani kuwa maadam kitabu kimetoka, kazi ya kukitangaza na kukiuza ni ya mchapishaji, na mimi naendelea na shughuli zangu zingine.
Lakini kujitafutia elimu katika vitabu na makala mbali mbali kulinisaidia kufahamu kuwa ukweli ni tofauti. Mwajibikaji mkuu wa kutangaza na kuuza vitabu ni mwandishi mwenyewe. Wachapishaji hawana uwezo wa kukitangaza kila kitabu kwa namna inayotakiwa. Kama mwandishi ni maarufu sana, wanakuwa na motisha ya kufanya hivyo. Na hata hivyo, umaarufu wa mtu kama huyu ni motisha ya kutosha kwa wasomaji kukitafuta kitabu chake wao wenyewe. Mtu kama Bill Gates au Osama bin Laden akiandika kitabu, wengi duniani watataka kukisoma, bila hata mchapishaji kukipigia debe.
Sasa, baada ya
kutambua kuwa jukumu la kuvitangaza vitabu vyangu ni langu, nilipata tatizo jingine. Mimi nafundisha chuo kikuu. Je, nina ubavu wa kukaa gengeni au kijiweni na kuuza vitabu? Watu watanionaje? Hii ilikuwa pingamizi kubwa. Ilikuwa ni kasumba ya usomi, ambayo baadaye niligundua haina mantiki nzuri.
Lakini, nilianza kujitafakari zaidi, kama ifuatavyo. Mimi ni mwalimu. Kazi yangu muda wote ni kuwaeleza watu fikra na mitazamo yangu. Katika taaluma yangu, hakuna ninachowaficha wanafunzi na watu wengine. Sasa iweje nisite kuvitngaza au kuviuza vitabu vyangu, wakati vitabu hivi ni sehemu ya yale yale ninayowaeleza watu siku zote? Je, kuwaonyesha watu vitabu vyangu kuna ubaya gani wakati lengo langu siku zote ni kuwagawia ujuzi wangu? Yaliyomo vitabuni ni yale yaliyomo kichwani mwangu, na ni sehemu ya nafsi yangu. Ninapoongea na watu, najitoa nafsi yangu. Kwa nini vitabu vyangu nivitenge kama vile si sehemu ya nafsi yangu?
Baada ya kupata utambuzi huo, nilianza kupata ujasiri wa kuviongelea vitabu vyangu kwa watu, sawa na ninavyoongelea masuala mengine yaliyomo katika uzoefu na ujuzi wangu. Nilianza kuhudhuria tamasha za vitabu nikiwa na meza ya vitabu vyangu. Nilianza kuona umuhimu wa shughuli hii. Watu wanakuja pale mezani na wanataka kusikia habari za shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, na uandishi. Na huwa sikosi kuwaelezea furaha ninayopata katika utafiti vijijini Tanzania na sehemu zingine, ingawa utafiti ni mgumu. Nawaeleza pia shughuli ninazofanya katika kuendeleza programu za kuwapeleka wanafunzi wa kiMarekani Afrika.
Jambo la msingi si kuuza vitabu; ni kukutana na watu, kuongea nao. Suala la vitabu linajitokeza lenyewe, bila hata juhudi ya pekee kwa upande wangu, kwani wakati wa mazungumo, watu hupenda kuangalia pia vitabu. Wanavyoridhishwa au kufurahishwa na taarifa za shughuli zangu, wanapata msukumo wa kujipatia kitabu. Cha muhimu ni kuwa na mazungumzo ya maana na ya kuvutia, na ni hayo ndio yanayowafanya watu wavutiwe na wazo la kununua vitabu.
Wengine, kwa hakika, wanatafuta vitabu, na wanavinunua hata bila maongezi. Wakishaona tu kitabu na kukiangalia kidogo, wanataka kukinunua. Na pengine wanaondoka bila hata mazungumzo, mbali ya kusalimiana tu na kuagana. Hao nao nawaheshimu, kama wale wanaopenda sana mazungumzo.
Naiona shughuli ya kuviongelea na kuvitangaza vitabu kama sehemu ya shughuli yangu ya ufundishaji. Ukweli ni kuwa mtu anayetaka kujifunza kutoka kwangu, atafanya vizuri akivisoma vitabu hivi na maandishi yangu mengine. Sioni sababu ya kuiona shughuli ya kuviongelea vitabu kwa namna nyingine. Naifurahia kama ninavyofurahia kufundisha darasani. Nakutana na watu wa kila aina, wenye taarifa na uzoefu wa namna mbali mbali. Kukaa kwenye meza na vitabu vyangu ni kivutio, na watu wanakuja wenyewe. Nafaidika sana na mazungumzo yangu na watu hao.
Kwa kumalizia, napenda nitaje jambo kuhusu waTanzania ambao wanapenda sana kulalamika kwamba watu kama mimi tunatumia nguvu zetu kuwafundisha watu wa nje badala ya kufundisha nchini. Lalamiko hili halina msingi madhubuti katika dunia ya leo yenye tekinolojia zinazowezesha mawasiliano kirahisi sana. Vitabu vyangu vinapatikana mtandaoni, kama nilivyoonyesha hapo juu. Hata kama mtu yuko Arusha, Mbeya, au Mtwara, anaweza kuviagiza akaletewa.
Lakini, kwa kuwa waTanzania wengi hawana uwezo wa kuagiza kwa njia hiyo, nimehakikisha kuwa vitabu hivi vinapatikana Tanzania, kama vile Dar es Salaam, simu namba 0717 413 073 au 0754 888 647. Kama kweli mtu ana nia ya kujifunza kutoka kwangu, anachoweza kufanya ni kuvitafuta vitabu hivi na kuvisoma, na baada ya hapo tunaweza kuendeleza mjadala kwa njia ya barua pepe. Watu huku Marekani, Ulaya, na sehemu zingine duniani tunawasiliana hivyo, bila kuonana uso kwa uso. Kwa jinsi mawasiliano yalivyo leo, mwalimu anaweza kukaa ofisini kwake Tanga na akafundisha darasa lenye watu walioko Morogoro, London, Pretoria, Kinshasa, na New Delhi. Watu waache kutoa visingizio, na badala yake wawajibike.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
6 comments:
Prof. asante kwa maelezo haya ya kuuza vitabu who knows labda hapo baadaye na wengine tunaweza tukafuata nyayo na kuandika walau kitabu kimoja.
Pia nimependa usemi wako huu nanukuu "Je, nina ubavu wa kukaa gengeni au kijiweni na kuuza vitabu? Watu watanionaje? Hii ilikuwa pingamizi kubwa. Ilikuwa ni kasumba ya usomi, ambayo baadaye niligundua haina mantiki nzuri."
Nimecheka maana hii ni kweli ni kasumba ya usomi inayotupata wengi,hata sisi akina mama inatupata katika transition ya kukaa nyumbani kulea watoto kwa muda au kuamua kurudi kufanya kazi ofisini mapema baada ya kuwa na mtoto.Kwa upande wangu nafikiri huu usemi wa watu watanionaje haumsidii mtu badala yake huwa unamuongezea mtu stress na kukurudisha nyuma kutofikia malengo uliyojiwekea.Cha muhimu ni kutoangalia macho ya watu na kufanya kile unachokiona ni bora kwako na wale unaowalenga.
Dada Sophie, shukrani kwa ujumbe wako. Itakuwa jambo jema ukijikongoja na kuandika kitabu. Unayo mengi ya kutuelimisha kutokana na uzoefu wako. Nitafurahi kukupa mawaidha kutokana na kauzoefu kangu.
Ni kweli, kunakuwa na huu wasi wasi kuhusu kuwaeleza watu habari ya vitabu vyako. Unajisikia kama si wewe, na kama si vizuri kufanya hivyo. Unajiuliza, hivi sijishushi hadhi yangu kweli?
Nimeuweka kama mchapo lakini ni wasi wasi unaotupata. Na haikuwa rahisi hata kidogo kuufuta wasi wasi huu na kujijengea mtazamo kama nilivyoeleza. Nimeandika kama mchapo kwa sababu, kama unavyojua kutokana na kile kitabu changu, huwa napenda kupunguza uzito wa tatizo kwa kuliangalia kimchapo.
Na kusema kweli, ninapoangalia picha hii ya nne kutoka juu, natabasamu, kwani nimekaa na kustarehe sawa sawa na mchuuzi gengeni :-)
Asante kwa hili Profesa. Kweli Watanzania visingizio tumezidisha jamani.:-(
Naitwa Charles , yaani ndo nimeanza kuandika kitabu changu kwa kweli ujumbe wako umenigusa sana sana , Hongera prof naomba pia email yako
Ndugu Charles Cosmas, shukrani kwa ujumbe wako. Anwani yangu mojawapo ni africonexion@gmail.com
Ningependa kufahamu namna ninavyoweza kuuza vitabu vyangu mtandaobi, mi mwandishi chipukizi.
Post a Comment