Makala hii imechapishwa katika Kwanza Jamii.
Profesa Joseph L. Mbele
Leo nimeamua kuongelea safari za Rais Kikwete, maarufu kama JK, katika nchi za nje. Suala hili linazungumzwa sana na waTanzania. Wako wanaodai kuwa JK anatumia muda mwingi mno nje ya nchi badala ya kubaki nchini na kushughulikia masuala ya nchi. Wako wanaodai kuwa JK anaenda kuomba omba misaada. Wengine wanasema kazi ya kuzunguka nje ni ya waziri wa mambo ya nchi za nje, na kwamba kwa vile JK alizoea kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje, bado hajabadilika, hata baada ya kuwa rais. Basi, kila mtu anasema yake, nami nimeona nichangie.
Naanza kwa kukiri kuwa nchi ya nje ninayoifahamu kuliko zote ni Marekani. Nimeishi na waMarekani katika nchi yao kwa miaka mingi, nikiwafundisha na kujumuika nao kwa namna mbali mbali. Naweza kusema nawafahamu, na suala la safari za JK katika nchi za nje, naweza kuliongelea kwa kutumia mfano wa Marekani.
Rais Kikwete ameshatembelea Marekani mara kadhaa, tangu awe rais. Binafsi, naona safari zake ni za manufaa. Kwanza, waMarekani kwa ujumla hawazijui nchi za Afrika kwa majina. Sana sana wanajua tu Afrika. Kuja kwa JK daima imekuwa ni fursa nzuri ya waMarekani kuijua na kuikumbuka nchi inayoitwa Tanzania. Kwa vile JK ni mtu mkubwa, ujio wake unatangazwa vilivyo, na hivi wahudhuriaji wanakuwa wengi. Fursa ya kuitangaza Tanzania inakuwa kubwa zaidi kuliko kama angekuja mbunge au waziri kama wanavyotaka baadhi ya Watanzania. Sio rahisi mbunge au waziri aje Marekani aweze kuwavuta watu kama anavyowavuta JK.
Watanzania wanaoishi Marekani wanayo fursa ya kuitangaza Tanzania, na wako wanaofanya hivyo, kwa kadiri ya uwezo wao. Lakini mtu kama Rais Kikwete anapokuja, suala hili linakuwa na mafanikio mara dufu. Kinachosaidia zaidi ni kuwa JK ana mvuto wa pekee kwa watu. Wamarekani walishangaa kuona alivyokuwa na uhusiano wa karibu na Rais Mstaafu Bush. Na hilo niliwahi kuelezwa pia na mzee mmoja Mmarekani, ambaye ni balozi mstaafu na mtu mashuhuri. Tayari, dalili zinaonekana kuwa JK na Rais Obama wataelewana vizuri. Kwa mtazamo wangu, ziara za JK zinatuweka waTanzania kwenye chati inayohitajika vichwani mwa watu wa huku nje.
Suala la uwezo wa JK kuitangaza Tanzania nililishuhudia alipofika katika jimbo la Minnesota, Septemba 26, 2006. JK alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thomas, mjini Minneapolis. Baada ya Chuo kutoa wasifu wa JK na msingi wa kumpa tuzo hiyo, JK alitoa hotuba ambamo aliwaelimisha watu wa Minnesota kuhusu hali halisi, uwezo, malengo na mahitaji ya Tanzania na Afrika. Alielezea utajiri na fursa zilizomo katika nchi yetu na bara letu. Katika kuiongelea Tanzania, alitaja rasilimali tulizo nazo, kama vile madini, ardhi ya kilimo, vivutio vya utalii, na taratibu muafaka za kuwezesha uwekezaji. Aliongelea pia hali ya kijamii na kisiasa, kuwa ni nchi ya amani, ukifananisha na nchi zingine. Alisisitiza kuwa mazingira ya uwekezaji na ubia ni mazuri katika Tanzania na kuwa yanazidi kuboreshwa.
Hakuishia hapo, bali aliezea pia matatizo na mahitaji. Alisema kuwa pamoja na rasilimali zake, Tanzania haina uwezo wa kuziendeleza ipasavyo bila ushiriki wa wengine. Alisema kuwa Tanzania inahitaji mitaji na wawekezaji. Alisisitiza kuwa Tanzania si maskini anayehitaji kuhurumiwa na kutupiwa misaada. Inachohitaji ni washiriki katika kuufanyia kazi huu utajiri na kuleta faida kwa pande zote.
Kwa namna hii, JK alituweka Watanzania na Waafrika katika akili za WaMarekani, kwa namna tofauti na walivyozoea. Wao wamezoea kuisikia Afrika, na wengi wanadhani Afrika ni nchi ndogo, ambayo ni hoe hae kwa dhiki, njaa, maradhi na vita. JK alijenga picha tofauti miongoni mwa wali0hudhuria. Kwa yeyote anayewafahamu waMarekani, huu ni mchango mkubwa wa fikra, hasa tukizingatia kuwa vyombo vya habari viliripoti vizuri ujio wake.
Rais Kikwete alikuja na ujumbe mkubwa kutoka Tanzania, hasa wafanyabiashara. Kuja kwake na ujumbe wa wafanyabishara kulimaanisha kuwa Tanzania inataka kufanya biashara, si kuomba misaada. Ilifanyika semina kuhusu masuala ya biashara na uwekezaji Tanzania. WaTanzania wengi wanaoishi huku Minnesota walihudhuria, na walikiri kuwa semina hii ilikuwa muhimu sana. Kwa maoni yangu, JK alitekeleza vizuri jukumu lake.
Kilichobaki ni upande wetu waTanzania. Ingekuwea bora kama waTanzania waliohudhuria wangefanya utaratibu wa kuwaelezea wenzao ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria, ili kuyatafakari na kuyafanyia kazi yale ambayo yalitokana na ujio wa JK. Ulihitajika utaratibu wa sisi waTanzania kuendeleza mawasiliano na waMarekani, baada ya JK kuwahamasisha. Sisi tungepaswa tuikuze ile mbegu ambayo JK alikuwa ameipanda.
Lakini waTanzania hatukujizatiti kufanya hayo. Inawezekana wako wanaoendeleza masuala aliyoanzisha Rais Kikwete, lakini sio kama jumuia. Labda wako ambao wanafuatilia, lakini hakuna taarifa. Hatuna vikao ambapo tunaelimishana na kuhamasishana. Tunakutana tu kwenye misiba au sherehe. Kama vile ilivyo Tanzania, kwenye sherehe waTanzania tunajitokeza kwa wingi. Lakini kwenye masuala ya kushirikiana katika maendeleo, ni wazi tunahitaji kujirekebisha.
Ziara ya JK ilileta msisimko miongoni mwa watu wa Minnesota, na iliripotiwa vizuri katika vyombo vya habari. Ilikuwa ni juu yetu waTanzania kutumia fursa hii iliyotengenezwa na JK ili kuendelea kuwa karibu na watu wa Minnesota, na kuwa nao bega kwa bega, kupanga mipango na mikakati ya uwekezaji, ubia, biashara, na kadhalika.
Kwa maoni yangu, wale wanaosema JK anazunguka nchi za nje kuomba omba misaada hawasemi ukweli. Kuhusu hoja kuwa kazi ya kuzunguka nje JK awaachie wengine, sina hakika kama tutapata mafanikio kama anayoyapata yeye. Ikiwa tutamleta mbunge au waziri, sina hakika ni waMarekani wangapi watavutiwa kuja kumsikiliza. Wanaosema JK akae nchini ashughulikie matatizo ya ndani, huenda wana hoja, lakini, kwa mtazamo wangu, si rahisi kutenganisha mambo ya ndani na ya nje. Pengine kwa kujishughulisha na mambo ya nje Rais Kikwete anajenga mazingira mazuri ya kutusaidia kwa mambo ya ndani. Vile vile Tanzania ina viongozi wengi au watu wengi ambao tunawaita viongozi. Hao wanafanya kazi gani? Kwani ni lazima awepo JK kuwaelekeza watu wa wilayani au mkoani wajibu wao? Je tunamhitaji rais aje kuwahamasisha watu wazoe taka taka mitaani, au waendeshe magari kwa uangalifu? Tunao viongozi wengi, kuanzia mtaani hadi kwenye ngazi ya Taifa. Wanafanya nini, na wanashindwa nini mpaka awepo rais?
Watanzania tumezoea kukaa vijiweni na kutoa lawama kwa wengine. Nayachukulia malamiko kuhusu safari za nje za JK kwa msingi huo. Kama kila mwananchi na kiongozi angewajibika pale alipo, nchi yetu ingekuwa mbali. Lakini hii tabia ya kumlaumu rais na kumtaka awepo nchini kutuelekeza namna ya kusafisha mitaro iliyoziba ni visingizio vya waTanzania ambao wanapenda zaidi kukaa vijiweni na kukosoa kuliko kuwajibika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
Huku niliko huwa Taarifa za habari hazitangazi ujio wa Viongozi wa Afrika ipaswavyo.
Mpaka huwa namuonea wivu Rais wa North Korea kwa jinsi anavyo lazimisha kwa vitisho hawajamaa wamsikilize kitu ambacho labda si poa lakini kinafanya kazi zake labda kuliko juhudi za viongozi wa Afrika. Kwa maana akijikuna tu huko North Korea huku lazima tupashwe.
Na leo moja ya habari kuu ilikuwa ni ya Mbwa wa Obama kauma Microphone.Rais Kikwete na wengine wa Afrika mara nyingi hawapati Coverage hata kumshinda mbwa wa Obama mitaa ya huku:-(
Duh!! Poleni Mkodo.
Profesa. Heshima kwako.
Nami nimekuwa mmoja wa wasioona umuhimu wa ziara za Rais. Na sababu ni kuwa hazionekani kuinufaisha nchi na kama zinainufaisha, basi hazielezwi zainufaisha vipi. Labda nikuulize wewe Prof kama umeshawahi kusoma uchambuzi wa UMUHIMU NA MWENENDO wa ziara za Rais kama ambavyo umeandika hapa. Ingekuwa hivi, nina hakika kuwa asilimia kubwa ya sisi tunaolaumu tungeelewa na kutambua faida (hata za miaka kadhaa ijayo)lakini hatupati. Tunaona picha za walivyoonana na wacheza filamu, walivyokutana na Obama, walivyotembelea studio na mengine as if ndilo kuu tutakalo kuona. Kama kuna lawama basi inaenda kwa Rais kwa kuwa anakumbatia timu isiyomuwakilisha vema kwa wapiga kura.
MAANDISHI YAKO YANAELEZA NA KUELEWESHA NA KAMA YOTE YANGEKUWA HIVI, TUSINGEPATA SHIDA KUUTAMBUA UMUHIMU WA ZIARA ZA RAIS.
Labda niongeze hii niliyoikuta kwa Dr Faustine kuhusu IDARA YA HABARI YA IKULU.
Baadhi ya maandishi yake n(ninayokubaliana nayo kwa asilimia kubwa) yanasema
"
Hapo nyuma kulikuwa na tovuti ya ikulu. Sitaki kusema mengi, nakushauri utembelee www.ikulu.go.tz na www.statehouse.go.tz ujionee kulichopo.
Mwaka 2008, Idara ya mawasiliano Ikulu ilianzisha blogu iliyohusu shughuli na safari mbali mbali zinazofanywa na Rais. Tatizo la blogu ni kwamba wahusika wanachelewa sana kuweka mambo mapya (updating).
Kupata taarifa muhimu kuhusu kinachoendelea nchini sio anasa ni haki. Watanzania wengi walio ndani na nje ya nchi wanatumia mfumo wa mtandao kupata taarifa ya vitu vinavyojiri ndani na nje ya nchi. Kwa kutokuwa na mtandao unaoaminika Idara ya Mawasiliano Ikulu haiwatendei haki watanzania. Idara hii ingeweza kutumia mfumo huu wa mawasiliano kuwapa taarifa wananchi kuhusu yale anayofanya Rais.
Mwakani tutakuwa na uchaguzi, Mimi nilitarajia kuwa Idara ya Mawasiliano ingekuwa imeweka mikakati ya kufufua na kuboresha mifumo ya mawasiliano kuelekezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya nne.
Kwa kutokuwa na mfumo unaoeleweka wa mawasiliano, Idara yaMawasiliano inamwangusha Rais na pia inawanyima haki watanzania kujua nini Rais wao anafanya. Natumai watatusikia na kufanya marekebisho. "
Post a Comment