Monday, May 25, 2009

Jiwe la Mmbuji

Hili ni Jiwe la Mmbuji. Liko mahali paitwapo Ngwambo, katika nchi ya Umatengo, wilayani Mbinga, mashariki ya Ziwa Nyasa. Jiwe hili kubwa linasemekana lina maajabu. Wamatengo tangu zamani wanasimulia mambo ya ajabu yanayotokea hapa.

Wamatengo wanaamini kuna viumbe viitwavyo ibuuta. Ni kama binadamu, ila wadogo sana, na wa ajabu, na katika mataifa mengine wanajulikana pia, kwa majina mbali mbali. Wamatengo wanasema kuwa ibuuta wanakuwepo kwenye jiwe hili usiku wakifanya mambo yao.

Nyumbani kwangu sio mbali na hapo, na jiwe hili tulikuwa tunalisikia tangu tukiwa wadogo. Tukipanda mlimani kijijini kwetu, tulikuwa tunaliona. Mwaka jana nilipita karibu na eneo hili, nikapiga picha ya jiwe hili kama inavyoonekana hapa. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kulikaribia jiwe hili namna hii.

Nilishangaa kuona watu wamelima mashamba karibu yake, na wanaishi sio mbali na hapo. Habari nilizozisikia tangu utoto wangu kuhusu jiwe hili zilinifanya niamini kuwa hakuna mtu anaweza kusogea hapo, achilia mbali kuishi karibu na hapo.

Mawe ya ajabu yako sehemu mbali mbali Tanzania, Afrika na sehemu zingine za dunia. Baadhi nimeshayaona sehemu kadhaa Tanzania, katika safari zangu za utafiti juu ya masimulizi na imani za jadi. Mawe hayo, pamoja maajabu mengine, kama vile miti mikubwa, maporomoko ya maji, na mapango, ni urithi mkubwa katika nchi yetu.

Utafiti juu ya mambo hayo unatufungua macho kuhusu mila, desturi, imani, na maisha ya binadamu. Tunagundua jinsi wanadamu tunavyofanana. Ni muhimu tuyajumlishe hayo katika mambo tunayofundisha mashuleni, pamoja na mengine, kama vile hadithi. Mtu wa mbali, kama vile mtalii, akija kuangalia jiwe la Mmbuji, kwa mfano, na kusikia habari zake, atakuwa amepiga hatua katika kuwaelewa waMatengo, na atawaelewa zaidi akijifunza pia historia yao, na hadithi zao, kwa mfano kama zilivyo katika kitabu hiki.

8 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Oh akanono! hicho kitabu mpaka nikipate kwani ni lazima.Wamatengo ni ndugu zangu wa karibu sana.

Mbele said...

Kitabu hiki ni mkusanyiko wa hadithi kumi nilizorekodi kule nyumbani Litembo katika kaseti, nilipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar, miaka ya katikati ya sabini na kitu.

Baada ya kurekodi, kazi iliyofuata ni kuzisikiliza kwa makini na kuzitafsiri kwa kiIngereza. Kazi hii ni ngumu sana. Unajaribu hiki na kile, na daima unaona hujafanikiwa, maana lugha zinatofautiana, na yaliyomo katika lugha fulani ni kioo cha utamaduni na mtazamo wa watu wa utamaduni ule, ambao ni wa pekee, tofauti na tamaduni zingine.

Pamoja na kuhangaika na tafsiri, nilifanya pia kazi ya kuzichambua hadithi hizi, kwa mujibu wa taaluma ya fasihi simulizi. Hapo niliangalia fani, falsafa, na masuala mengine. Kwa hivi, kila hadithi katika kitabu hiki imefuatiwa na insha ya uchambuzi wake. Na mwishoni kabisa nimeweka insha ndefu kiasi ya kitaaluma, kuhusu hadithi, kama inavyojitokeza katika hadithi hizi, na katika utafiti sehemu mbali mbali duniani.

Nilihangaika na shughuli hii kwa miaka yapata 23, na hatimaye nikaona bora niachie ngazi, nichapishe huu mswada. Ndio kitabu hiki.

Kitabu hiki kimewavutia walimu hapa Marekani na wanakitumia vyuoni. Hata wasio walimu au wanafunzi, nao wanakisoma, na mimi hupata fursa mara kwa mara kwenda kuwasilimulia hadithi hizi na kusaidiana nao kuzichambua, kama unavyoona hapa.

Albert Kissima said...

Profesa Mbele nakushukuru kwa kutujuza kuhusu jiwe hili la Mmbuji.

Niliwahi kusikia kuwa ktk ziwa Victoria kuna jiwe ambalo limegawanyika katika ncha tatu kila moja iki-point upande wa Uganda, Tanzania na Kenya. Pengine katika upekuzi wako ulishakutana na ajabu hili utujuze kwa undani zaidi.

Mzee wa Changamoto said...

Nimejifunza mengi kuhusu hili jiwe na nashukuru Kaka Kissima kwa swali ambalo kama Prof atakuwa na jibu, basi litakuwa darasa jingine ambalo tunalipata na lina manufaa kwetu.
Asante sana Prof

Mbele said...

Ndugu Kissima na mashabiki wangu wote, kuhusu haya masimulizi mengine, nilitaka kuwaambieni kuwa najiandaa, kaeni mkao wa kula :-)

Tatizo ni kuwa nilibanwa na bado nimebanwa na shughuli za kusahihisha mitihani. Ila, kifupi ni kuwa nimeshafanya utafiti Ukerewe na Ukara, ambavyo ni visiwa maarufu katika Ziwa Victoria.

Ni kweli, kuna masimulizi mengi sana kule, yakiwemo ya ajabu sana, yanayohusu mawe, viumbe vya majini, na kadhalika. Nimewahi kwenda kuliona Jiwe la Ukara, ambalo linacheza. Hili ndilo jiwe maarufu kuliko yote katika Ziwa Victoria, kwa upande wa Tanzania.

Masimulizi kuhusu mawe ni mengi, na sishangai kusikia hayo unayoongelea Ndugu Kissima. Inatakiwa mtafiti uwe na subira na uwe sehemu husika kwa muda mrefu, hata miaka. Kwa vipindi nilivyofanya utafiti kule, kuanzia mwaka 1993 hadi 1997, sikuweza kusikia kila simulizi, na haiwezekani, hata ukikaa maisha yako yote.

Kutokana na msisimko wa mada hii, napangia siku za karibuni kuwaleteeni hapa kwenye blogu habari za Jiwe la Ukara. Kwa hivi, kama wasemavyo vijiweni, kaeni mkao wa kula :-)

Albert Kissima said...

Hapa nimeshameza mafundo mengi tu ya mate, nakisubiria hicho chakula kwa hamu kweli kweli.Hakika ninajifunza mengi ambayo sikuwa nayafahamu na nitazidi kujifunza mengi katika kibaraza hiki.

Mbele said...

Nimeona taarifa kuhusu kijana Mmarekani ambaye amepata ajali na kufariki hapa Mbuji. Bofya hapa.

Mbele said...

Jiwe la Mmbuji, maana lina mengi. Hivi karibuni, nimeandika makala nyingine kuhusu Jiwe hili katika blogu yangu ya ki-Ingereza. Makala ni hii hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...