Thursday, May 14, 2009

Kipanya na Usomaji Vitabu

Mimi kama mwalimu na mwandishi ninaliongelea sana suala la usomaji wa vitabu. Katika blogu hii, maandishi yangu mengi yanahusu suala hilo. Hapa kuna katuni ya Kipanya, ambayo nimeiona kwa Profesa Matondo. Inatoa mchango wake kwa mtazamo unaofanana na wangu. Nitatoa mfano mmoja.













Tarehe 21 Juni, 2008, niliendesha warsha Arusha, na katika mazungumzo yangu nililalamikia tabia ya waTanzania kutopenda kusoma vitabu. Nilitoa mfano kama huu wa Kipanya, kwamba waTanzania wanaposafiri katika basi, hutawaona wakisoma vitabu. Hapo mwanawarsha mmoja, mama Mwingereza, alitoa hoja kuwa utamaduni wa waTanzania wa kuongea na wenzao ndani ya basi unaonyesha wanavyojali mahusiano ya mtu na mtu, tofauti na wazungu, ambao kwao ni kila mtu na lwake. Alimaanisha kuwa jamii ya wazungu imekosa mshikamano; badala ya kuongea na binadamu mwenzao, wanashikilia kitabu. Hoja hii ilinifungua macho.

Kipanya ana tovuti yake hapa

4 comments:

Christian Bwaya said...

Hili suala la kutokupenda kusoma, linaweza kuwa na historia ndefu. Jamii zetu zimetuzoesha masimulizi mepesi na vichekesho.

Taarifa chache tulizo nazo tumezipata kupitia masimulizi. Pengine ni kwa sababu vitabu vilivyopo vinaonekana kuwa si sehemu ya utamaduni wetu. Lugha. Maudhui. Na kadhali. Ndio maana hata ukikishika, yale matarajio yako yenyewe yanatia shaka. Kwamba utakachokipata mumo hakikuhusu sana. Ni elimu ya ziada ambayo hata usingeipata hupati hasara ya maana.

Nadhani tusichoke kuhamasisha. Lakini pia tunaoweza kuandika mambo yanayohusu maisha ya kawaida ya watu wetu, basi na tufanye hivyo hata kama wachapishaji hawajishughulishi kuchangamkia wazalendo wenye nia hii.

Pengine kutokuwa na vitabu vyenye kuhusiana moja kwa moja na watu, nako kunachangia.

Bennet said...

Bado sijajua tatizo ni nini hasa, tuna vitabu vichache au usambazaji wa vitabu vyetu unahitilafu?
WaTanzania tunasoma sana magazeti na majarida

Mzee wa Changamoto said...

Baado naamini kuwa tunapandikizwa tabia mbaya ya kutosoma. Si vitabu tu, bali hata magazeti na hata hizi blogu na mitandao. Vyenye kuandika na kueleza yasiyoonekana kuifikirisha jamii ndivyo vionekanavyo kupata wafuasi. Labda ni kweli kuwa hakuna vitabu vya kutosha, lakini mbona hata wenye dhamana ya kulirekebisha hili hawaonekani kufuatilia? Kwa kuwa wananufaika na udaku huu. Na pia kwanini hata waandishi kama Prof Mbele wanapoandika vitabu na kueleza vilipo hawaoni huko "kukimbizana" kwa hao wenye uhitaji?
"Tumetindiishwa" ubongo kwa kupenda habari zisizofikirisha.
Kila kitu kikizidi ni kibaya, na pengine wazungu wamezidi kujisomea kuliko kuongea na wenzao, lakini na sisi tumezidi kutongea na wenzetu kuliko kusoma.
Baraka kwenu nyote

Mbele said...

Shukrani kwenu nyote. Tuendelee kuelimishana. Mzee wa Changamoto, uzoefu wangu na waTanzania unaendana na yote unayosema. Ni watu ambao hawagutuki na masuala ya vitabu. Isipokuwa ikitokea sherehe ya uzinduzi wa baa mpya, ukumbi unafurika, na ukichelewa, kiti hutapata. Utaishia kunywa kabia kako ukiwa umesimama kaunta:-)

Nikupe mfano moja tu. Kijitabu changu kimoja ni mwongozo wa ile riwaya maarufu ya "Things Fall Apart," iliyoandikwa na Chinua Achebe.

Kijitabu hiki kinatumiwa na walimu, wanafunzi na wengine huku Marekani na sehemu zingine za dunia, kwani nilikichapisha mtandaoni, ambapo kinaweza kuagizwa na yeyote duniani kwa kutumia "credit card."

Lakini, kwa kuwafikiria waTanzania, ambao wengi hawana uwezo wa kuagiza mtandaoni, niliamua, mwezi Mei 2003, kujikongoja na kukichapisha pale Dar es Salaam, kwa gharama ya dola 500.

Baada ya kukichapisha, nilitegemea sasa waTanzania watapanga foleni kukipata, kama wanavyopanga foleni kwenye kitimoto. Wapi! Mtu moja moja ananunua. Siku moja, pale Tanzania Publishing House, nilimkuta Mmarekani anakinunua, ili aje nacho huku Marekani. Ni mhusika mmoja wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Illinois.

Hapo nilibaki mdomo wazi, kuona kitabu nilichowealetea waTanzania kinarudi tena Marekani! Hali hii inavikumba vitabu vyangu vyote ambavyo nimevipeleka Tanzania. Wazungu wanavinunua pale na kuja navyo ughaibuni.

Nikirudi kwenye kile kijitabu nilichotaja mwanzo, ni kuwa kimewahi kutumiwa hata na Chuo Kikuu cha Cornell, ambacho ni chuo kimoja maarufu kabisa hapa Marekani na duniani. Katika somo la kIngereza, Chuo Kikuu cha Cornell ni kati ya vyuo vinavyowika hapa Marekani. Na walikipigia debe kijitabu hicho, kama unavyoona hapa.

Sasa, mbele ya ushahidi kama huu, kwa nini waTanzania wasizinduke na kukipigia foleni pale pale Dar es Salaam? Wakati huo huo, Watanzania hao wanahangaika kuwaleta watoto wao Marekani kusoma. Ndio hali ilivyo: vijana wa Bongo waje Cornell, wasome kitabu ambacho wamekiacha pale pale Bongo.

Halafu, waTanzania ni wepesi kulalamika kwa nini watu kama mimi tunawafundisha wazungu badala ya kurudi nyumbani kuwafundisha walalahoi.

Mimi naandika vitabu. Yale ninayomfundisha mzungu yamo humo vitabuni. Na vitabu hivi nahakikisha viko Tanzania. Anayetaka kweli kujifunza kutoka kwangu, hahitaji kuningoja nirudi Tanzania. Anaweza kuanza kwa kusoma vile vitabu, na akiwa na masuali, anaweza kuniletea barua pepe tukaelekezana. Siku hizi watu wanatumia tekinolojia ya mawasiliano katika elimu. Mtu anaweza kukaa London, akafundisha darasa ambalo wanafunzi wamezagaa duniani kote. Kwa hivi, umbali si hoja katika dunia ya leo. Kwamba tunawafundisha wazungu tu ni vizingizio vya wapenda bia na kitimoto. Cha zaidi ni kuwa, ninapokuwa Tanzania yeyote anaweza kuongea nami au kuhudhuria warsha zangu. Lakini ninapofanya hizo warsha kule, jamaa wako kitimoto :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...