Friday, May 1, 2009

Mchango wa Wabeba Boksi

Leo, siku kuu ya wafanyakazi duniani, napenda kuwakumbuka wabeba boksi. Hao ni waTanzania wanaoishi ughaibuni, wakifanya kazi za mikono, kama vile kubeba na kupanga mizigo ya bidhaa madukani, kusafisha maofisi, kusafisha vyombo mahotelini, kuwatunza wazee, na kadhalika. Watanzania wanaposema kubeba boksi, wanamaanisha kazi za aina hiyo. Na jina hilo linatokana na huu kweli kuwa wengi wa wahusika wanabeba na kupanga maboksi.

Wabeba boksi wanataniwa sana katika jamii ya kiTanzania. Wabeba boksi wengi nao wanajitania. Watanzania wengi wanaziona kazi za boksi kuwa ni kazi duni. Napenda kubadili mtazamo huo kwa kuelezea umuhimu wa boksi. Natumia hilo neno boksi kwa sababu linatumika pia kumaanisha kazi ya kubeba boksi.

Jambo moja la msingi ni kuwa wabeba boksi wanatumia nguvu zao kujipatia kipato. Wao ni tofauti na wezi au mafisadi, ambao wanakula jasho la wenzao. Kwa msingi huu, mbeba boksi anastahili heshima.

Kila kazi halali ina umuhimu wake katika jamii, iwe ni kilimo, uvuvi, usafishaji vyoo, ualimu, udaktari, au upigaji muziki. Kila kazi ya aina hiyo inastahili heshima. Mpiga boksi anafanya kazi muhimu. Bila yeye, jamii itakwama. Anastahili heshima.

Wabeba boksi, kama vile walivyo waTanzania wengine wanaoishi ughabuni, wanatoa mchango mkubwa katika kipato cha Taifa, kwa hela wanazotuma nyumbani, iwe ni kwa ndugu, jamaa, marafiki, au taasisi. Nimesoma taarifa kuwa mwaka 2008, kwa mfano, watu hao waliliingizia Taifa dola zaidi ya 100 millioni. Wenzetu waKenya wanaoishi nje waliingiza nchini mwao dola zaidi ya 400 millioni. Ni wazi kuwa mbeba boksi, akiwa ni mmoja wa watu hao, ni mtu muhimu kwa uchumi wa Taifa.

Je, lipi bora zaidi: kukaa vijiweni nchini bila ajira, au kubeba boksi? Hili ni suali la kutafakariwa.

Kuna wabeba boksi ambao, baada ya kukusanya hela, wanaanzisha miradi nyumbani wakiwa bado ughaibuni, na wengine wanarudi nyumbani na kuanzisha hiyo miradi. Kwa njia hiyo, wanatoa ajira kwa wananchi wenzao.

Mpiga boksi, kwa kukaa ughaibuni, anajifunza mengi. Anarudi nchini akiwa na upana wa mawazo kuhusu dunia na uzoefu wa nidhamu ya kazi, vitu ambavyo vinaweza kutoa changamoto kwa wananchi wengine.

Kwa ufupi, boksi lina umuhimu na heshima yake.

5 comments:

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

aiseeeeeee

na mimi nimesoma kwa kulipiwa na wabeba maboksi. tatizo ni pale wabeba maboksi walipokuja nyumbani na kujifanya wabebesha maboksi, kuwa wako juu.

kazi ni kazi na kila kazi ni njeama na ni bora pia kwani ni kazi.

Mzee wa Changamoto said...

Heshima kwako Prof Mbele.
Ukweli ni kwamba watu wengi wanashindwa kuwa na mtazamo chanya na mpangilio mwema wa kile wafanyacho. Nashukuru kwa maelezo haya ambayo licha ya kuwa na ufahamu wa heshima kwa BOKSI ninalobeba hapa, nimepata kingine cha ziada. Mtazamo wa akiba na kurutubisha mipango ya baadae nikirejea nyumbani. Napenda wabeba boksi wenzangu nao watambue ka undani yaliyonenwa na hasa waweke umakini katika aya yako uliyoandika "Mpiga boksi, kwa kukaa ughaibuni, anajifunza mengi. Anarudi nchini akiwa na upana wa mawazo kuhusu dunia na uzoefu wa nidhamu ya kazi, vitu ambavyo vinaweza kutoa changamoto kwa wananchi wengine."
Basi tutambua kuwa kujifunza ni kutaka. Kwa hiyo kukaa ughaibuni pekee hakutakufunza kama hutaki kujifunza. Na tuangalie nafasi tuliyonayo, tuitumie kwa umakini na mafanikio yatafuata.
Heshima kwenu

Mbele said...

Mimi nilikulia kijijini, nikiwa mtoto wa wakulima. Nilikuwa nachunga mbuzi na ng'ombe, nashiriki kulima, kuchuma kahawa, na kadhalika. Hadi leo, pamoja na kufundisha vyuo vikuu Tanzania na Marekani, sijasahau asili yangu. Nawaheshimu wakulima, wafugaji, wafagiaji, na kadhalika.

Kwa hivi, boksi ninaliangalia kwa heshima kama nilivyoeleza. Watu wasionifahamu hawajui hayo. Niliwahi kuhojiwa na Bongo Celebrity. Mdau mmoja alivyoona picha ya sura yangu aliandika kuwa boksi linanimaliza. Nilicheka kuona jinsi anavyolichukulia boksi. Soma maoni yake ya tarehe 19 Machi hapa.

Bennet said...

Kazi ni kazi madhali una malengo yako na unataka kuyatimiza, kitu cha muhimu ni kipato kama huna uwezo wa kufanya kazi nyingine za juu kwa sababu ya elimu unaanza na hizi kazi za chini, unakwenda shule na unatafuta kazi nzuri.

Sophie B. said...

Wote tukiwa na mtizamo wa kutodharau kazi kama hizi na wazifanyao tutafika mbali.Article nzuri Prof. nimeipenda nika iblog.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...