Sunday, June 14, 2009
Binadamu Amnyonyesha Mnyama
Picha hii, iliyotokea tarehe 8 Juni, 2009, kwa Mjengwa, ya mama anayemnyonyesha mwanawe upande mmoja na mnyama yatima upande mwingine imenivutia na inanifikirisha.
Wengi wetu labda tutashangaa na kujiuliza kama huyu mama ana akili timamu. Lakini nadhani huyu mama anatufundisha au kutukumbusha mengi. Ni mama mwenye upendo na huruma. Habari hiyo hapa juu inasema kuwa huyu mama alikuwa anawalea watoto wake sambamba na huyu mnyama. Watoto na mnyama walikuwa wanacheza pamoja bila shida, na wakati wa kunyonyesha, mama anawanyonyesha wote kama inavyoonekana katika picha. Laiti nasi tungevipenda viumbe vyote namna hiyo hiyo. Lakini kwa wengi wetu, hata kuwapenda binadamu wenzetu tu ni shida. Uhasama, vita na magomvi hayaishi.
Huko tulikotoka, binadamu na wanyama tulikuwa pamoja, bila utengano. Pole pole kiumbe kinachoitwa binadamu kilibadilika na kuwa hivyo kilivyo leo. Lakini msingi wa maumbile yetu na wanyama wengine ni ule ule. Kama sisi wanadamu tunaweza kunywa maziwa ya ng'ombe na kustawi, kwa nini wanyama nao wasinyonye maziwa ya binadamu kama inavyoonekana katika picha hii? Huyu mama anathibitisha kuwa inawezekana, na hakuna madhara. Badala yake, anathibitisha kuwa ni faida pande zote.
Kuna hadithi nyingi na masimulizi mengine kuhusu binadamu waliolelewa na wanyama, labda kwa sababu ya kupotelea porini walipozaliwa, au kutelekezwa huko. Hadithi za aina hii zimekuwepo tangu zamani sana, sehemu mbali mbali za dunia. Warumi wa kale, kwa mfano, walikuwa na masimulizi kuwa waasisi wa mji wa Roma walikuwa Remus na Romulus, mapacha ambao walilelewa na wanyama porini. Hata miaka ya karibuni, zimeshatokea habari Uganda na sehemu zingine za kugunduliwa kwa binadamu ambao walilelewa na nyani porini.
Katika fasihi, tangu zamani za kale, habari hizi zimekuwepo. Katika hadithi ya Gilgamesh, iliyoanzia miaka elfu nyingi zilizopita katika nchi iitwayo Iraq leo, kulikuwa na mhusika aitwaye Enkiddu, ambaye aliishi porini na wanyama, kama ndugu wa damu. Ingawa kimwili alikuwa ni binadamu, hakuwa na tabia wala silika ya binadamu. Naye David Maluf, mwandishi maarufu wa Australia, ameelezea katika riwaya yake, Remembering Babylon, habari ya mtu aliyeanza kupoteza tabia na vipawa vya binadamu, kama vile lugha, kwa kuishi sana na wanyama.
Pamoja na mambo mengine, hadithi hizi zinatupa chemshabongo ya kutafakari nini maana ya kuwa binadamu.
Nafurahi jinsi huyu mtoto katika picha anavyomchungulia huyu mnyama. Haogopi. Na mnyama nae hawaogopi wanadamu. Laiti tungeendeleza jadi hii ya binadamu na wanyama kuishi pamoja bila uhasama. Leo hii, tuna uhasama mkubwa baina yetu na wanyama wa porini. Wakristu wanasimulia habari za Mtakatifu Francis wa Assisi, kwamba alikuwa anawapenda sana wanyama na ndege, nao walimpenda, wala hawakumwogopa, na walikuwa wanamkimbilia wakati wa shida. Ndege wa angani walikuwa wanakuja na kutua mikononi mwake, naye akiwalisha. Mtakatifu huyu aliwaita hao wanyama ndugu zake, kaka na dada.
Huyu mama katika picha anafanya vizuri kumlea mwanae katika tabia ya kuwa karibu na wanyama na kuwapenda na kuwajali. Tabia hii ingetufaidia wanadamu katika maisha yetu.
Mwandishi wetu maaarufu, Shaaban Robert, ni mmoja kati ya watu waliotuhamasisha kuwaheshimu na kuwapenda wanyama, ndege, na viumbe vingine. Katika maandishi yake alisisitiza muungano uliopo baina ya viumbe mbali mbali. Laiti kama tungezingatia mafunzo na falsafa yake; labda leo tungekuwa watunzaji wazuri wa wanyama na mazingira kwa ujumla.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
Mkuu hapa mimi naona kama kidogo kuna walakini nikweli inabidi tuwapende wanyama, kwa mtazamo wangu mimi kama mumyhery, labda kwa kutaka kumsaidia mnyama labda ningekamua na kuweka maziwa kwenye chombo kuliko kumnyonyesha moja kwa moja toka kifuani kwangu, hivi samahani tuchukue mfano mimi kama binti yako au mke wako nayoonyesha mtoto wako halafu nanyonyesha mbwa tukichukulia ile habari iliyo tangazwa toka BBc Swahili ambayo kuna baba mmoja alikuwa anamlazimisha mkewe awanyonyeshe mbwa wake ambao walikuwa wanamsaidia kuwinda, kwani alikuwa na ngo'mbe amabao walikuwa wanampatia maziwa ambao alitoa mahari wakati anataka kumuoa, hivyo mbwa wakawana pa kupata maziwa ndipo akawa anamuamrisha mkewe awe anayonyesha hao watoto wa mbwa amabo mama yao alikufa, matokeo yake mtoto mmoja akapata kichaa cha mbwa na kufa na mwengine nae alianza kukohoa kama mbwa, na mama pia chuchu zilikuwa na madonda kwani akinyonyesha mbwa huwa wana muuma, hili unalionaje, kama na watoto wako au wajukuu wanyonya ziwa moja nambwa? kwa kawaida sisi kwetu mkinyonya ziwa pamoja ni ndugu, hivyo yule mbwa pia anakuwa ndugu, kweli nawapenda wanyama lakini kwa mtazamo wangu kidogo naona kuna mushkeli kidogo
Naona umeuliza masuali magumu sana. Ikiwa kuna kulazimishana, nakubali ni kitu kibaya sana. Lakini nahisi huyu mama kwenye picha anafanya hivyo kwa utashi na mapenzi yake. Na nahisi kuwa anaona yote ni salama, kwa mtoto na huyu mnyama.
Isipokuwa, nawajibika kukubaliana nawe kwamba ingekuwa ni jambo linatokea miongoni mwa ndugu zangu, nadhani ningetishika, na labda hata mawazo yangu yangetikisika pia.
Hapo tunaona kuwa nadharia na vitendo wakati mwingine haviendani. Ni rahisi zaidi kuwa na nawazo na kuyatetea, kuliko kuyatekeleza.
Post a Comment