Wednesday, October 26, 2016

Miaka 80 ya "The Snows of Kilimanjaro"

Kwa mara nyingine tena, ninaandika ujumbe kuhusu kutimia kwa miaka 80 tangu hadithi ya Ernest Hemingway, 'The Snows of Kilimanjaro" ilipochapishwa kwa mara ya kwanza. Niliandika ujumbe wa aina hiyo katika blogu hii. Leo nimesoma tena ujumbe wangu, nikajiridhisha kwamba niliyosema ndiyo ninayoamini hadi sasa.

Jambo moja kubwa kabisa ni kuwa wa-Tanzania tunajipotezea fursa za wazi za kutumia hazina kama hii hadithi ya Hemingway kuitangaza nchi yetu. Niliandika katika ujumbe wangu baadhi ya mambo ambayo tungeyafanya mwaka huu wa kumbukumbu. Lakini mwaka unaelekea ukingoni, na hakuna tulichofanya. Hii ni hasara ya kukosa utamaduni wa kusoma vitabu. Tunashindwa hata kutumia fursa zilizo wazi.

Nimeona niandike ujumbe huu leo kwa sababu wiki hii, hapa katika Chuo cha St. Olaf ninapofundisha, litatokea jambo la pekee linalohusiana na Ernest Hemingway. Keshokutwa, tarehe 28, pataonyeshwa kwa mara ya kwanza filamu ya "Papa's Shadow," ambayo niliwahi kuielezea katika blogu hii.

Hiyo ni filamu iliyotokana na kozi niliyofundisha Tanzania mwaka 2013 iitwayo Hemingway in East Africa. Nilisafiri na wanafunzi 29 wa Chuo cha St. Olaf, tukazunguka maeneo kadhaa ya Tanzania kaskazini, ambamo alipita Ernest Hemingway mwaka 1933-34. Katika safari hiyo, tulikuwa tunasoma maandishi ya Hemingway kuhusu maeneo hayo na maeneo mengine ambayo alipitia mwaka 1953-54.

Maandishi hayo ni pamoja na Green Hills of Africa na Under Kilimanjaro, ambavyo ni vitabu, kadhalika hadithi fupi mbili: "The Short Happy Life of Francis Macomber" na "The Snows of Kilimanjaro." Pia aliandika makala katika magazeti na barua nyingi akielezea aliyoyaona na kufanya katika safari zake. Kwa ujumla wake, maandishi haya ya Ernest Hemingway yanaitangaza nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa namna ambayo sisi wenyewe hatujaweza kujitangaza.

Hiyo filamu ya "Papa's Shadow" inawasilisha vizuri mambo muhimu ya uhusiano wa Ernest Hemingway na Afrika Mashariki. Sehemu kubwa ya filamu hii ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway. Tunajadili kwa kina na mapana fikra za Ernest Hemingway kuhusu Afrika, uandishi, na maisha kwa ujumla.

Kwa kuwa hiyo filamu inaonyesha sehemu mbali mbali za Tanzania na maelezo kuhusu mambo yanayoifanya Tanzania kivutio kwa watalii, kama vile Mlima Kilimanjaro, na kwa kuwa filamu hii imejengeka katika maandishi ya Ernest Hemingway, mwandishi maarufu sana ulimwenguni, ni wazi kuwa filamu hii itakuwa chachu ya kuitangaza Tanzania kwa namna ya pekee. Taarifa zaidi Kuhusu "Papa's Shadow," zinapatikana kwenye tovuti ya Ramble Pictures.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...