Wednesday, October 19, 2016

Nimepata Vitabu Vipya vya Uislam

Leo nimepata vitabu kadhaa vya u-Islam kutoka kwa profesa Nadia Mohamed wa Minneapolis Community and Technical College. Huyu profesa, mzaliwa wa Misri, tulifahamiana mwaka jana. Muhula uliopita nilimwalika kutoa mhadhara katika darasa langu, Muslim Women Writers. Nilimwalika tena, na amekuja leo.


Katika vitabu alivyonipa leo, kuna nakala za Quran, yaani tafsiri tofauti. Kabla, nilikuwa na tafsiri mbili: moja ya Abdallah Yusuf Ali, yenye maelezo ya kina, ambayo nimekuwa nayo kwa miaka mingi, na ya pili aliyonipa Profesa Nadia Mohamed alipotembelea darasa langu muhula uliopita, kama nilivyoripoti katika blogu hii.

Lakini leo, amenipa The Message of the Quran, iliyotafsiriwa na kufafanuliwa na Muhammad Asad. Humo kuna Quran kwa hati ya ki-Arabu, na hicho ki-Arabu kipo pia kwa hati ya ki-Rumi. Na kuna tafsiri ya ki-Ingereza, pamoja na maelezo ya kina. Nakala ya Abdallah Yusuf Ali ina sura mbili: hati ya ki-Arabu na tafsiri ya ki-Ingereza.

Profesa Nadia Mohammed amenipa nakala zingine mbili za Quran, tafsiri ya Abdallah Yusuf Ali, ila ni tofauti na ile niliyokuwa nayo tangu zamani, kwa kuwa hii ni tafsiri tu bila yale maelezo. Hizi nakala ni vitabu vidogo kwa ukubwa, na kwa hivi ni rahisi kubebwa popote. Zinaonekana pichani hapa kushoto, zikiwa na majalada tofauti.

Kuna uzuri wa kuwa na tafsiri mbali mbali za Quran. Tunaambiwa kwamba ki-Arabu cha Quran ni cha pekee, sio rahisi kukitafsiri kwa lugha yoyote. Maneno yake mengi yana utajiri wa maana na ladha ambao ni mtihani mkavu kwa yeyote anayejaribu kutafsiri. Kutokana na ukweli huo, ambao unahusika pia katika tafsiri ya lugha yoyote, ni bora kusoma tafsiri mbali mbali. Nilimwambia hivyo Profesa Nadia Mohamed, ambaye ni mtaalamu, akaafiki.

Vitabu vingine alivyonipa ni viwili vidogo vidogo. Kimoja kinaitwa A Brief Illustrated Guide to Understanding Islam na mtunzi ni I.A. Ibrahim. Cha pili ni Wisdom for Life & The Afterlife: A Selection of Prophet Muhammad's Sayings, ambacho ni mkusanyiko wa mafundisho ya Mtume Muhammad, yaliyotafsiriwa na Samir Saikali kwa ki-Ingereza, kutoka ki-Arabu, na kuchapishwa na Islamic Literacy Project.
No comments: