Monday, October 31, 2016

Black African Voices: Tungo za Afrika

Pamoja na kwamba fasihi ya Afrika, kama ilivyo ulimwenguni kote, inastawi kwa kasi kadiri miaka inavyopita, na waandishi wapya hujijokeza na kujipambanua, ni lazima pia kukumbuka na kusoma uandishi wa zamani. Kwa yeyote anayependa fasihi, awe ni mwanafunzi, mwalimu au msomaji wa kawaida, usomaji wa aina hii ni jambo lisilohitaji mjadala. Fasihi inahitaji usomaji usio na kikomo, sio tu kwa kuwa ina historia ndefu, bali pia kwa kuwa inastawi ulimwenguni kote na daima inaendelea kuchanua kama maua.

Mimi, mwalimu wa fasihi, ninazingatia umuhimu wa kufundisha kazi za tangu zamani hadi leo. Fasihi ya kila taifa au sehemu yoyote ya dunia ina historia, na fasihi inayoandikwa leo ni mwendelezo wa mkondo ulioanza zamani.

Katika siku hizi chache, nimekuwa ninasoma Black African Voices, kitabu kilichohaririwa na James E. Miller na wenzake. Sikumbuki ni lini nilikinunua kitabu hiki, lakini mara kwa mara katika kuangalia vitabu vyangu, nilikuwa ninakichungulia kitabu hiki, nikawa ninakumbuka kwa furaha enzi za ujana wangu, kuanzia miaka ya sitini na kitu, nilipokuwa ninasoma badhi ya tungo zilizomo. Kuna hadithi kadhaa na nyimbo za fasihi simulizi, mashairi, hadithi fupi na maandishi mengine ya waandishi mbali mbali.

Baadhi ya waandishi ambao tungo zao zimo katika kitabu hiki ni Ezekiel Mphahlele, Raphael Armatoe, Peter Abrahams, Birago Diop, David Diop, Cyprian Ekwensi, Richard Rive, Wole Soyinka, John Pepper Clark, James D. Rubadiri, na Grace Ogot. Ni furaha isiyoelezeka kuzisoma tena hadithi zilizonisisimua tangu miaka ile ya sitini na kitu, nilipokuwa mwanafunzi katika seminari ya Likonde, 1967-70 na Mkwawa High School, 1971-72.

Baadhi ya hadithi hizo ni "No Room at Solitaire," ya Richard Rive; "The Dignity of Begging," ya Bloke Modisane, "The Rain Came," ya Grace Ogot. Baadhi ya mashairi yaliyonisisimua miaka ile ni "Stanley Meets Mutesa" (James D. Rubadiri), "Africa" na "Listen Comrades" (David Diop), na "Prayer to Masks" (Leopold Sedar Senghor). Kuna pia tamthilia ya Edufa ya Efua Sutherland.

Katika Black African Voices kuna pia tungo za waandishi ambao sikuwafahamu miaka ile ya ujana wangu, kama vile J, Benibengor Blay (Ghana), Tshakatumba (Congo), Rui Nogar (Mozambique). Siwezi kuwataja waandishi wote ambao kazi zao zimo katika kitabu hiki, bali ninapenda tu kusisitiza kuwa ninaguswa sana na uandishi huu wa kuanzia miaka ya kabla ya kuzaliwa kwangu hadi ujana wangu. Wahariri walifanya kazi nzuri kuzikusanya tungo hizi katika kitabu kimoja.

1 comment:

Goodluck Ndunguru said...

Nimeipenda hii, kweli fasihi inaishi.Ubarikiwe Prof.