Sunday, September 27, 2015

Tumechangia Kanisa la Venezuela

Leo kanisani kwetu hapa mjini Northfield, kanisa Katoliki, tulikuwa na padri ambaye anatumikia kanisa fulani nchini Venezuela. Huyu padri ni m-Marekani, na kwa miaka yapata arobaini, mapadri wa-Marekani wamekuwa wamisionari katika kanisa hilo la Venezuela. Hata paroko wetu aliwahi kutumikia kanisa hilo kwa miaka mitano. Ananivutia kwa jinsi anavyoijua lugha ya ki-Hispania, na anawahudumia waumini hapa Northfield wanaotumia lugha hiyo.

Huyu padri mgeni alitoa mafundisho mazuri, na katika kuelezea utume wake Venezuela alituhimiza kwa maneno matatu: "Pray, say, pay." Alifafanua kwamba tusali kuwaombea waumini wa kanisa lile la Venezuela, tuwaeleze wengine kuhusu hali halisi na mahitaji ya kanisa lile, na tutoe mchango kulisaidia kanisa lile.

Niliguswa na maelezo yake, nikangojea muda wa kutoa mchango. Kilipopitishwa kijikapu cha mchango, nilikuwa tayari nimekwangua vijihela vilivyokuwemo katika pochi yangu nikavitumbukiza humo. Nilijisikia faraja na furaha kwamba vijihela hivyo vitakuwa na manufaa kwa kanisa lile la Venezuela, hasa kwa kuzingatia kuwa dola, hata zikawa chache, zinakuwa ni hela nyingi kwenye nchi kama Venezuela au Tanzania.

Mimi kama muumini wa dini, naiheshimu dini yangu, na dini zote. Ninafahamu kwamba zote ni njia wanazotumia wanadamu kuelekea kwa Mungu. Ni safari, kama safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro. Kuna njia kadhaa za kufikia kileleni Kilimanjaro. Na itakuwa ni wendawazimu kwa watu wanaochukua njia tofauti kuanza kugombana na kupigana hadi kuuana kwa msingi wa tofauti za njia wanazochukua. Kwa mtazamo wangu, ni wendawazimu kwa watu wa dini mbali mbali kubezana au kugombana.

Ninaziheshimu nyumba za ibada za kila dini. Niliwahi kuelezea katika blogu hii nilivyozuru nyumba za ibada za wa-Hindu, nchini India. Leo nimechangia kanisa lililoko Venezuela. Lakini sibagui. Kuna wakati niliona taarifa kuwa wa-Islam wa sehemu fulani Tanzania walikuwa wanachangisha fedha za kukarabatia msikiti wao. Nilipeleka mchango wangu, kwa moyo mkunjufu, ingawa mimi si mu-Islam bali m-Katoliki. Nitaendelea kufanya hivyo.

Ninachojali ni kuwa wanadamu wote wameumbwa na Mungu, na Mungu hana ubaguzi, kama nilivyoandika katika blogu hii. Ninafurahi kumiliki blogu, kitu ambacho kinaniwezesha kueneza mawazo yangu na kupambana na mawazo ambayo nayaona ni sumu, hata kama yanaenezwa kwa jina la dini.

No comments: