Friday, July 3, 2015

Mungu (Allah) Hana Ubaguzi

Blogu yangu hii ni uwanja huru kwa fikra na mijadala, ikiwemo mijadala kuhusu dini. Leo, kwa kifupi na lugha rahisi, napenda kuibua suala la dini na ubaguzi.

Laiti sisi tunaosema tuna dini tungetambua kuwa Mungu hana ubaguzi. Mungu, ambaye kulingana na tofauti za lugha, huitwa kwa majina mbali mbali, anathibitisha jinsi anavyowapenda wanadamu, wa dini zote, na wasio na dini.

Mungu anateremsha baraka zake bila ubaguzi. Anawapa uzazi watu wenye dini, sawa na wasio na dini. Wa-Islam wanazaa, wa-Kristu wanazaa, wa-Hindu wanazaa, na wa dini zingine kadhalika. Wasio na dini wanazaa.

Mungu anateremsha mvua kuotesha mbegu katika mashamba ya wa-Islamu, ya wa-Hindu, ya wa-Kristu, na ya wengine, hata wasio na dini. Kuku wa mu-Islam anataga mayai na kuangua vifaranga, sawa na kuku wa m-Kristu, sawa na kuku wa asiye na dini. Mungu hana ubaguzi katika kuteremsha neema zake.

Sasa basi, kwa nini wanadamu wengi wanaosema wana dini ni wabaguzi? Kwa nini wanatumia kigezo cha dini kujifanya wao ni bora kuliko wengine? Wanapobaguana namna hii, wanafuata njia ya Mungu au ya shetani?

11 comments:

NN Mhango said...

Mungu ni mbaguzi by nature. jiulize kwanini aliwaumba wanadamu akawapa akili wakati akiwanyima wanyama wengine? Pia naomba nikukosoe hapa. Allah si Mungu sawa na Jehovah kulingana na wanaowaabudia miungu hawa. Maana ukienda kwa wakristo wana utatu wakati waislam wana tawheed yaani upekee wa Allah. Nakubaliana nawe kuwa wenye dini ni wabaguzi sawa na miungu yao. Kwa mfano kwa imani ya kiislamu muislam ni bora kuliko asiye muislam. Surat 41:141, 3:28 ziko wazi. Kimsingi Biblia na Quran ni vitabu vya kibaguzi. Ndiyo maana vilipoletwa Afrika vilitukana na kudhalilisha mila zetu hata kutusingizia. Hivyo, ubaguzi ni asili ya dini hasa hizi za kimamboleo. Mfano Biblia Matayo 15:24, pia zipo sura zinazowataja wayahudi na wasiotahiriwa. Ujanja au tuseme utata wa hivi vitabu ni kwamba baadaye vinahubiri upendo na usawa huku vikipulizia vita na maangamizi. Kwa ufupi hakuna taasisi baguzi duniani kama dini. Ndiyo maana zina sheria (canons) za ajabu ajabu tofauti na taasisi nyingine. Mimi huwa napenda dini za kiasili ambazo hazina makuu wala makundi zaidi ya kutoa mwongozo simple.

Mbele said...

Ndugu Mhango,

Shukrani kwa mchango wako ambao nauona unafikirisha na kusisimua. Nimependa ulivyowasha moto. Kazi kwa waumini na wasio waumini.

Mbele said...

Ndugu Mhango,

Ngoja niseme neno, wakati nikiendelea kuzisubiri kauli za waumini na wasio waumini wa dini. Kwa mtazamo wangu, ambao ni imani yangu, wala siwasilishi au kuwakilisha imani ya wengine, ni kuwa Mungu ni mmoja, ila wanadamu wanamweleza kwa namna tofauti. Akili ya mwanadamu ni ndogo na hafifu mno kuweza kumfahamu Mungu na kumwelezea kikamilifu. Tunababaisha, ndio maana waumini wa dini mbali mbali wana maelezo tofauti. Kwangu hili si tatizo, ili mradi nisisitize kwamba Mungu si mjinga kama wanadamu wanavyodhani.

Ninamaanisha nini? Ninamaanisha kama nilivyotamka katika ujumbe wangu wa mwanzo, kwamba Mungu ameumba na anaumba vyote, na ameumba na anaumba wanadamu wa kila aina, na wote anawateremshia neema zake, kama vile nilivyoelezea. Waumini wangekuwa na akili nzuri wangezingatia hilo.

Badala yake, wamezua hizi dini na ndio tatizo lilipo. Tatizo si Mungu, ni wanadamu na dini zao. Dini ndio shule wanamofundishana mawazo na fikra hasi za kiburi, majivuno na ubaguzi. Ninamaanisha hizo fikra za waumini wa dini hii kujiona ni bora kuliko waumini wa dini ile pale, fikra za kudharauliana, kugombana, kuuana, kwa msingi wa dini, au kwa kutumia dini kama kichocheo cha tabia hizo mbovu.

Sisemi kwamba moja kwa moja dini ni sumu. Kuna mfano hai uliotoa wa dini za jadi za wahenga wetu. Zilikuwa safi, na hazikuwahi kutumiwa kama msingi au kichocheo cha ubaguzi, uhasama, na mauaji. Kwa mtazamo wangu, kama dini zote zingefuata njia hii, hatungekuwa na matatizo haya yanayoletwa au kuchochewa na dini.

Kwa kuwa tunautaja u-Islamu na u-Kristu, na ningependa kuongezea u-Hindu, waumini wa leo wanayo fursa ya kuamua namna ya kuitafsiri misahafu ya dini zao. Wanayo fursa na wajibu wa kutambua kuwa wanaishi katika dunia tofauti na ile ya kale, wana upeo wa fikra na fursa tofauti na zile walizokuwa nazo watu wa kale, na kwa hivi sherti waamue namna ya kuitafsiri misahafu. Wasiichukulie kikasuku. Ukasuku ndio unachangia matatizo. Inabidi waumini waweze kupambanua baina vitu viwili ambavyo kwa ki-Ingereza huitwa "the letter and the spirit of the Scriptures."

Watu wenye roho mbaya wanaweza kabisa kutafuta vifungu katika misahafu na kuvitumia kuhalalisha uovu. Kuna mhusika, Antonio, katika tamthilia ya Shakespeare, "The Merchant of Venice," ambaye anasema, "The devil can cite Scripture for his own purpose." Yaani shetani anaweza kunukuu msahafu kwa malengo yake mwenyewe.

Hili ndilo tatizo ninaloliona. Lakini mtu mwema mwenye nia njema anaweza kunukuu vifungu vya msahafu kuhalalisha na kuhimiza matendo mema. Ni uchaguzi wa mtu. Ni uchaguzi wa waumini. Lakini, kwa hali ilivyo, tatizo la ukasuku ni kubwa, na tatizo la roho mbaya ni kubwa.

Narudia kauli yangu: Nawasubiri waumini na wasio waumini wajitokeze wachangie mjadala. Blogu hii ni uwanja huru.

NN Mhango said...

Kaka nakubaliana nawe katika baadhi ya mambo na kupingana nawe katika baadhi. Ni kweli kuwa binadamu kwa uwezo wake mdogo kiakili hawezi kumjua Mungu vilivyo. Si kweli kuwa Mungu ni mmoja. Mamlaka husika zinadai hivyo. Wakristo na Waislamu wanasema miungu yao haifananishwi na yeyote. Hivyo, unaposema Mungu ni mmoja wakati ana sifa tofauti tokana na makundi tofauti unazidisha utata. Kwangu mimi ni kwamba Mungu hajulikani kwa wanadamu- kama ulivyosema-wanadamu wanababaisha kutokana na ufinyu wao wa uoni. Kuhusu ubaguzi nasema wazi kuwa dini -hasa za kimamboleo au tuseme pandikizi au nyemelezi - hata miunga yake ni wabaguzi. Jaribu kuchungua dini yako uone kwa mfano nafasi ya mwanamke na mwanamme uone kama ni sawa. Kwangu tatizo ni vyote vitatu yaani Mungu, dini na wanadamu au waumini wa dini husika. Ukirejea yaliyotokea zama za kale wakati wa inquisition na ugaidi unaoendelea kwa sasa utagundua tatizo la vyote vitatu. Leo sitaki niseme mengi. Nawaachia wengine nafasi nao waeleze yao. Hata hiyo concept ya shetani ni utata mtupu. Kimsingi, ni uumbaji wa wanadamu uliomzua shetani wengine wakisema kuwa alikuwa malaika mkuu akaasi jambo ambalo kwa malaika haliwezekani. Ni sawa na kusema robots au druids zinaweza kuasi wakati hazina uwezo huo. Hata kusema shetani alikuwa malaika mkuu ni uongo mtupu tena wa kitoto. Kwanini aasi hadi kumchukiza Mungu kana kwamba Mungu hakujua angefanya hivy. Maana kama Mungu anajua yaliyopo na yajayo alipaswa kujua kuwa malaika wake angeasi. Hivyo asingechukia wala kumuadhibu kwa vile alimuumba afanye hivyo ili kukamilisha mpango (project) ya Mungu. Kimsingi, uzushi, ubaguzi na uongo upo mwingi tu kwenye dini ambazo kinga au kichaka chake kikubwa ni imani na si welewa.

Mbele said...


Ndugu Mhango

Kwa maoni yangu, mjadala unaendelea kuwa mtamu, kwa maana ya kuchemsha bongo. Napenda tu niongelee kipengele kimoja, yaani iwapo Mungu ni mmoja au la. Ninaongea kama mu-umini wa dini yangu ya Katoliki, ingawa si mwakilishi au msemaji wa msimamo wa Kanisa langu.

Ninakubaliana nawe kuwa wa-Kristu wanalelewa katika imani kuwa kuna Mungu mmoja, na Mungu huyu ni yule wanaomwamini wao. Wanaamini kuwa Mungu wao ndio Mungu wa kweli. Kwa upande wa wa-Islam, ni hivyo hivyo. Wanalelewa katika imani kuwa kuna Mungu mmoja tu, ambaye kwa ki-Arabu huitwa Allah, ingawa sioni kama ni lazima wa-Swahili watumie jina hilo hilo. Wa-Islam wanaamini kuwa Allah ndiye Mungu wa kweli.

Hii ni kusema kwamba wa-Kristu wanatambua kuwa Mungu wao ni tofauti na Allah. Na wa-Islam wanatambua kuwa Allah ni tofauti na Mungu wa wa-Kristu.

Sasa hapo tayari kuna tatizo. Imetamkwa wazi katika Qur'an kwamba kuna Mungu mmoja tu. Sasa iweje wa-Islam wapambanue kati ya Mungu wao na Mungu wa wa-Kristu? Huku ni kukiri kuwa kuna Mungu zaidi ya mmoja. Ni kufuru. Vile vile kwa wa-Kristu, imetamkwa wazi katika amri kumi za Mungu kuwa kuna Mungu mmoja tu. Sasa iweje wa-Kristu waone kuwa Mungu wao ni tofauti na Allah. Yaani huku ni kukiri kuwa kuna Mungu mwingine tofauti na huyu wanayemwabudu wao. Ni kufuru dhidi ya amri kumi za Mungu.

Sasa mimi naona msimamo wangu ndio msimamo sahihi katika suala hili. Ninachosema ni kuwa kuna Mungu mmoja tu, ambaye huitwa kwa majina mbali mbali na watu wa dini mbali mbali, ambaye huelezwa namna mbali mbali na dini mbali mbali. Sifanyi kufuru hii ya kusema au kuamini kuna Mungu zaidi ya mmoja.

Wenye mawazo ya ziada au ya kupinga hayo tuliyosema nawakaribisha kwa mikono miwili.

NN Mhango said...

Kaka Mbele,
Shukrani kwa kurejea tena ingawa bado hitimisho lako limenichokoza pale uliposemaSasa mimi naona msimamo wangu ndio msimamo sahihi katika suala hili. "Ninachosema ni kuwa kuna Mungu mmoja tu, ambaye huitwa kwa majina mbali mbali na watu wa dini mbali mbali, ambaye huelezwa namna mbali mbali na dini mbali mbali. Sifanyi kufuru hii ya kusema au kuamini kuna Mungu zaidi ya mmoja." Mungu hawezi kuwa mmoja wakati kila mtu anakuja na vigezo vyake juu ya Mungu huyo huyo. Wakristo wakimueleza Jehova na waislam wakamueleza Allah unapata miungu miwili tofauti. Leo nitatumia kazi za wawili hawa ambao hawajawahi kuonekana na hawawezi kuonekana, nitatumia kiduchu toka kwenye kazi yao kubwa ambayo ni uumbaji. Wakristo wanasema Mungu alinyanga udongo akamtengeneza mwanaume aitwaye Adam na baadaye akatoa ubavu wake mmoja na kutengeneza mkewe aitwaye Eva jambo ambalo ukiliweka kwenye fikra yakinifu unaona ni kama utoto tu wa kawaida sawa na ambavyo watoto hufinyanga vinyago vyao vya kuchezea. Waislam nao japo ni kwa mchezo ule ule wa kukopi toka kwa wakrsito wanasema Allah alisema kila kitu kiwe kikawa. Hawa wanajitahidi kukwepa kutakiwa watoe maelezo ya mlolongo wa maelfu na mamilioni ya viumbe. Kinachochekesha ni pale waislam wanapomuita Allah muumbaji wakati si muumbaji kwa ajili ya maelezo yao, Nadhani walipaswa kumwita muhuuishaji badala ya muumbaji. Maana muumbaji lazima afanye kitendo cha kuumba ambacho wakristo wanakionyesha kama kufinyanga.
Hivyo, kwa kudurusu hayo machache, nategemea tutakuwa tumesogea mbele kidogo wakati tukingoja michango ya wenzetu hasa wakati huu wa mfungo wa Ramadhani ambapo michango yao hasa waislamu inawapa nafasi ya kupata twawab nyingi za kuweza kuwapeleka kwenye Jannah.

Anonymous said...

Huu mjadala ni mtamu, natamani tungekuwa tunachambua mambo hivi kuliko kishabiki na hisia. Nawapongeza sana Mhango na Mbele. Nikitulia nitachangia kwa undani zaidi.

Khalfan Abdallah Salim said...

Nashukuru kwa Prof. Mbele kwa kuiweka mada vizuri sana katika utangulizi wake na utetezi wake. Namshukuru Mhango kwa kuja na fikra tofauti. Hapo ndipo mjadala unapopata ladha na kusisimua watu wengine wafunguke.

Kimsingi, Mola hana ubaguzi na anao ubaguzi. Ifahamike ubaguzi si fikra hasi japo mara nyingi imekuwa ikitumiwa hivyo, ubaguzi kama dhana inancha mbili hasi na chanya. Ikiwa mtu hataki kutoa haki kwa mwingine au kumpa haki yake kwa sababu tu ni dini fulani tu, huu ni ubaguzi mbaya. Iwapo mtu hataki kuamiliana na mtu fulani ili asiathiriwe na fikra zake ambazo yeye hazimfurahishi mathalani mlevi au mgoni, hivyo akajitenga na yeye, huu ni ubaguzi mzuri. Mola hana ubaguzi katika kuwapa viumbe vyake vile alivyoahidi kuwapa kama alivyoeleza Mbele vizuri kabisa, kwa kuwa kufanya hivyo ni ubaguzi mbaya lakini iwapo imani yako au vitendo vyako haviendani na yale yenye kumridhisha na kustawisha jamii, ataendelea kupewa vile vile lakini malipo yake hayatokuwa sawa na wengine wanaotii na kuamini ipasavyo. Huu ni ubaguzi mzuri, hivi wema na waovu walipwe sawa eti kwa kuwa kutofanya hivyo ni ubaguzi!

Si sahihi kwa maoni yangu, kufikiri kuwa ubaguzi maana yake ni kuwepo kwa usawa na si vinginevyo. Hivi mtu angetaraji mwanaume azae kama anavyozaa mwanamke? Au mtu awe na mkia kama mbwa? Hivi wanawake wavae sawa na wanaume n.k? Bila shaka yapo maeneo ambayo ubaguzi maana yake ni kukosekana kwa usawa. Mfano, ajira inapokuwa ni kwa watu fulani tu n.k.

Kwa bahati mbaya, wafuasi wa dini zetu wamekuwa wakifanya mengi japo Mungu hajaagiza hivyo na si utashi wa Mungu mathalani katika utoaji wa haki na fursa kwa wote. Iwapo vijana wa kiislamu au kikristo waliofaulu watakatwa majina yao na wasipangiwe shule, huu ni ubaguzi mbaya. Sijui kama kuna dini yeyote inayoagiza hivyo, kuwa mtu wa imani tofauti na yako asipewe haki yake. Lakini haya yapo, tatizo nini? Pengine ni ule ugonjwa "Chuki Kubwa."

Itaendelea..

Khalfan Abdallah Salim said...

Baada ya kusema hayo, natofautiana na mawazo ya Mhango katika post yake ya mwanzo aliposema kuwa "Kwa mfano kwa imani ya kiislamu muislam ni bora kuliko asiye muislam. Surat 41:141, 3:28 ziko wazi." Kwanza sura 41:141 hiyo aya 141 haipo Je ni taypo? ama sura 3:28 inasema hivi "Waumini wasiwafanye makafiri kuwa wapenzi wao badala ya Waumini. Na anaye fanya hivyo, basi hatakuwa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Ila ikiwa kwa ajili ya kujilinda na shari zao. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni naye. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu." Hakuna ktk aya hii hicho alichosema Mhango, Uislam unahimiza uchamungu kuwa ndiyo sifa ya ubora wa mtu " Hakika aliyebora mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemuogopa." Aya hii ni maarufu na natumai Mhango anaijua vizuri. Kwa nini anapotosha na kudai kuwa huo upotoshaji wake ndio imani ya Kiislamu?

Kama mpenzi wa dini asili, je hivyo ndivyo dini asili inavyofunza? Tatizo la Mhango ni kama la J.Mihagwa (mwandishi wa Raia Mwema), wanapojaribu kusoma maandiko ya dini zetu fikra zao zinakuwa si huru hivyo, wao tayari washaegemea upande wao kinachofuata ni kutafuta kile alichosema Antonio ktk 'The Merchant of Venice'.

Mhango anasema " Waislam nao japo ni kwa mchezo ule ule wa kukopi toka kwa wakrsito wanasema Allah alisema kila kitu kiwe kikawa. Hawa wanajitahidi kukwepa kutakiwa watoe maelezo ya mlolongo wa maelfu na mamilioni ya viumbe. Kinachochekesha ni pale waislam wanapomuita Allah muumbaji wakati si muumbaji kwa ajili ya maelezo yao, Nadhani walipaswa kumwita muhuuishaji badala ya muumbaji." Inasikitisha sana kusoma sentensi yako ya mwanzo, eti waislamu wanakopi! (ama kweli akutukanaye hakuchagulii tusi) hili dai lako nilishajibu katika post za zilizopita, ila naona Mhango kafanya kuwa ni mtaji wa maandishi yake. Sihitaji kurudia jawabu.

Kuhusu uumbaji wa Allah , Qur'an inasema hivi "Yeye ndiye aliye kuumbieni vyote vilivyomo katika ardhi." 2:29, "Na hakika tulikuumbeni, kisha tukakutieni sura, kisha tukawaambia Malaika: Msujudieni Adam.." 7: 11. Hizo ni baadhi tu ya aya nyingi juu ya uumbaji wa Mungu kwa mujibu wa Uislamu, hivyo tufuate ya hao 'waislamu wako' au maneno ya Mungu mwenyewe? Kama unaswali juu ya mlolongo wa viumbe uliza ujibiwe, hamna anayekwepa. Waislamu wanaamini kuwa kwa Mola hufanya atakavyo, akitaka ataumba kwa mikono yako kama alivyofanya kwa Adamu au kwa tamko tu 'Kun fayakun (Kuwa-kikawa)'

Ni vyema kufanya tafiti na kuangalia mambo katika sura itakayoleta uwelewano na utangamano wa kijamii kama afanyavyo Pro.Mbele na sio kukuza tofauti za dini hadi kuleta maafa. Sisi waislamu na wengine, wajibu wetu ni kufikisha kwa wengine, na kutenda kwa uadilifu bila chuki wala dharau, na kutambua kuwa 'angelitaka Muumba angefanya watu wote wawe kitu kimoja (fikra zao, dini zao n.k)' si kwa faida wala wajibu wa Muislamu kudharau dini nyingine, au kujiona bora, bali kufanya yale yote ya uchamungu.

NN Mhango said...

Kwanza namshukuru ndugu yangu shehe Khalfan japo huwa hapendi kuitwa shehe. Kwa maana ya neno shehe na mchango wake, naamini yeye ni shehe mwenzetu. Japo Khalfan kajibu hoja bila jazba, nashukuru kuwa ameunga mkono baadhi ya hoja zangu huku akizichanachana nyingine. Naona kama nimemkwaza kwa kusema "Waislam nao japo ni kwa mchezo ule ule wa kukopi toka kwa wakrsito wanasema Allah alisema kila kitu kiwe kikawa." Hii ndiyo kun fayakun ambayo nadhani ndiyo namna alivyoumba Allah. Hivyo anapokuja na aya 2:29 anathibitisha ukweli wa hoja zangu kuwa kilichofanyika ni kukwepa kufanya kile alichofanya Jehova ambaye aliumba kitoto kwa kufinyanga udongo. Ninaposema kukopi namaanisha Quran kutokuwa na jipya zaidi ya kukariri yale yaliyokwisha bainishwa na wakristo lakini ikasema ni mapya na yameshushwa. Yangeshushwaje wakati yalishashwa na kujulikana hata kabla ya Sayyidina Muhammad (SAW)hazaliwa wala kutumishwa? Nadhani hii ndiyo hoja yenye mashiko na ya msingi isiyopaswa kufinywa wala kufinyangwa. Uumbaji kwa aliyesema kun fayakun kila kitu kikawa ni neno tata na halina mantiki. Ima kuhusu ubaguzi nadhani ubaguzi halina ubishi hata livishwe joho. Kwa nijuavyo mimi ubaguzi ni kitu hasi sawa na uuaji, ufirauni, uasherati n.k. Hivyo, kutaka kuuhalalisha kwa namna yoyote ni kupotoka na kupotosha wengine. Sioni ubaguzi mzuri. Nadhani alichotaka kueleza Khalfan akaishia kukichanganya na ubaguzi ni kuepuka baadhi ya watu au mambo lakini si kuwabagua.
Kitu kingine ambacho ni tata ni hadithi ya malaika kumsujudia Adam. Apaswaye kusujudiwa ni mmoja. Hivyo, pamoja na kuwa ni hoja inayosemekana kuwa ya Quran, kuruhusu kiumbe tena kilichoumbwa na aliyeumbwa kisujudiwe na viumbe wengine ni kufuru isiyosameheka kama tutakuwa makini na uchambuzi huria wa yale tunayosoma. Si kweli kuwa mimi ni sawa na Joseph Mihangwa. Mihangwa ni Mihangwa na Mhango ni Mhango na tuna maoni na elimu tofauti. Hivyo, mjumlisho wa aina hii unaweza kutafsirika kama kupindisha hoja au kutaka kuwapa watu majina mabaya. Wakati unaniacha Insh'Allah siku nyingine. Wabillahi tawfiq

Mbele said...


Ndugu Mhango

Napenda kuendeleza hoja yangu kuwa Mungu ni mmoja tu, pamoja na kwamba dini mbali mbali zinamweleza kwa namna tofauti. Umeandika:

"Mungu hawezi kuwa mmoja wakati kila mtu anakuja na vigezo vyake juu ya Mungu huyo huyo. Wakristo wakimueleza Jehova na waislam wakamueleza Allah unapata miungu miwili tofauti."

Napenda kurudia kauli yangu kwamba wanadamu hawana akili ya kuweza kumfahamu Mungu alivyo. Pamoja na juhudi yao yote, na nia njema, wanababaisha. Huo ubabaishaji wao unajidhihirisha kwa jinsi wanavyomwelezea Mungu kwa namna mbali.

Kuna hadithi ya vipofu saba na tembo. Vipofu saba walipata fursa ya kumshika tembo ili wafahamu tembo yukoje. Kipofu mmoja alishika mkia, akaelewa kuwa tembo ana umbo la kamba nene. Kipofu mwingine alishika mguu, akaelewa kwamba tembo ana umbo la mti mnene uliosimama. Kipofu mwingine alishika pembe, mwingine alishika sikio, na mwingine alishika tumbo, na kadhalika. Wote wakaja na tafsiri yao ya tembo alivyo. Zikawa tafsiri saba tofauti.

Kwamba vipofu hao walimwelewa tembo kwa namna mbali mbali haimaanishi kuwa tembo hakuwa mmoja. Na Mungu ni hivyo hivyo. Waumini wanajitahidi, lakini hawana upeo wa kuweza kumwelezea Mungu alivyo kikamilifu. Huu ndio msimamo wangu.