Leo Ijumaa tumemaliza wiki ya kwanza ya muhula wa kiangazi. Tumesoma tamthilia mbili za Ama Ata Aidoo wa Ghana: The Dilemma of a Ghost na Anowa, ambazo ni miongoni mwa tamthilia maarufu za Afrika. Hata hivi, kama ilivyo kawaida yangu, nimewatahadharisha wanafunzi kuwa dhana ya kumaliza kusoma kazi ya fasihi ni dhana potofu. Haiwezekani kumaliza, kwa maana ya kuielewa kikamilifu hadi kikomo, hata tukiisoma tena na tena
Ninapenda kufundisha The Dilemma of a Ghost sio tu kwa kuwa ni kazi nzuri kisanaa, bali pia kwa namna inavyoyaanika masuala ya maisha. Mfano muhimu ni suala la mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Msingi wa mahusiano hayo katika tamthilia hii ni ndoa baina ya kijana aitwaye Ato, kutoka Ghana, na Eulalie, mwanamke m-Marekani Mweusi.
Hao wawili wanakutana na kuoana wakiwa Marekani, ambako Ato alikuja kusoma. Eulalie, kama walivyo wa-Marekani Weusi wengi, anafurahi sana kwamba atakwenda Afrika, ambako ni asili ya watu wake. Ana imani kuwa atapokelewa kama mtoto wa nyumbani na atakuwa na maisha ya raha. Ato anachangia matumaini hayo kwa kumwelezea Eulalie mambo mazuri ya Afrika, pamoja na kutia chumvi.
Hali inakuwa tofauti baada ya wawili hao kufika nyumbani kwa Ato. Eulalie anakumbana na madharau kutoka kwa ndugu za Ato kwa kuwa ni kizalia cha watumwa. Tofauti za tamaduni zinachangia matatizo baina yake na ndugu hao. Hali inaendelea kuwa mbaya na kumkosesha raha Eulalie hadi hatimaye mama mkwe wake anapoamua kurekebisha hali na kuufanya ukoo umkubali.
The Dilemma of a Ghost imesheheni matumizi ya fani ya fasihi simulizi, kama vile nyimbo na hadithi za mapokeo. Dhamira ya kijana kujifanyia uamuzi wake wa kuoa bila kuwashirikisha wanafamilia ni dhamira inayojitokeza katika hadithi nyingi za mapokeo za Afrika. Katika riwaya yake, The Palm Wine Drinkard, Amos Tutuola aliweka hadithi ya "The Complete Gentleman" yenye muundo huo.
Matumizi ya fani ya fasihi simulizi yanajitokeza zaidi katika tamthilia ya Anowa. Humo tunashuhudia mambo yanayompata Anowa, msichana mzuri kuliko wote ambaye alikuwa anawakataa vijana wote waliokuwa wanamchumbia. Hatimaye anajichagulia mwenyewe kijana ambaye wazazi wake hawaridhiki naye. Yeye na mume wake wanahama nyumbani na kwenda mbali ambako wanajitafutia maisha. Hata hivi mwisho wao si mzuri.
Muundo wa hadithi ni ule unaofahamika katika hadithi za ki-Afrika na zinginezo ulimwenguni. Majivuno na ukaidi kwa wazee, wahenga, au miungu, hayana mwisho mwema. Wagriki wa kale walikuwa na dhana ya "hubris," kuielezea tabia hii. Waandishi kadhaa wa Afrika wametunga hadithi zenye dhamira hiyo. Mifano ni riwaya ya Things Fall Apart ya Chinua Achebe na riwaya ya Chaka ya Thomas Mofolo.
Kumalizia wiki hii ya kwanza, na ili kuwapa wanafunzi fursa ya kutafakari masuala muhimu, nimewapa jukumu la kuandika insha fupi moja kufuatana na maelekezo haya:
1) Discuss a female character in The Dilemma of a Ghost or Anowa.
2) Write about children in The Dilemma of a Ghost and Anowa.
3) Discuss the relationship between one couple--a man and a woman--in The Dilemma of a Ghost or Anowa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment