Sunday, July 5, 2015

Majadiliano na Profesa Joseph Mbele

MAJADILIANO HAYA YAFENYIKA KATI YA MANDELA PALLANGYO. NA PROFESA JOSEPH MBELE WA CHUO KIKUU CHA OLAF CHA MAREKANI.
PROFESA JOSEPH MBELE

Safari yako ya uandishi ilianza muda mrefu. Je ni kipi kinakutia moyo na kuzidi kufanya kazi hii ngumu?
PROF: JOSEPH MBELE
Mimi ni mwalimu na ninauona uandishi kama sehemu ya ufundishaji au aina ya ufundishaji. Ndio maana uandishi wangu unaelekea zaidi katika mambo yanayoelimisha. Kazi pekee niliyoitamani hata kabla sijaanza shule ilikuwa ni ualimu. Kwa hivyo, ninapenda kuandika kama ninavyopenda kufundisha darasani.

Uliwahi kukutana na maneno mabaya kama kukatishwa tamaa au kukashifiwa wakati ulipokuwa unaanza fani?
PROF: JOSEPH MBELE
Sikuwahi kukutana na maneno ya aina hiyo tangu mwanzo. Uandishi wangu umekuwa zaidi wa kitaaluma, ambao unatokana na utafiti. Hakuna wakati ambapo uandishi wangu huo umeleta maneno mabaya au ya kukatisha tamaa. Lakini kwa kuwa ninaandika pia magazetini na mitandaoni kuhusu masuala ya kawaida ya maisha, wakati mwingine nakutana na maneno mabaya. Hapa ninamaanisha maneno yasiyozingatia hoja, bali yananilenga mimi. Ninawaona wanaofanya hivyo kuwa ni wajinga, wasiojiamini, kwani hata hawajitambulishi. Ninawaheshimu watu wanaopinga hoja kwa hoja. Wanatajirisha mijadala na wanatupanua mawazo.

Umeandika vitabu vingi. Licha ya kuwa ni Profesa mwenye kazi nyingi. Je unawezaje kutenga muda wa kuandika na kutekeleza majukumu mengine kwa ufasaha? Na je vitabu vyako vinapatikanaje?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema, uandishi wangu kwa ujumla ni mwendelezo tu wa ufundishaji. Uandishi unanisaidia kufafanua mambo akilini mwangu. Ninapoandika kuhusu masuala ya kawaida ya jamii, najiona ninaburudisha akili yangu. Mara kwa mara naandika kwa mizaha, na hiyo inaburudisha. Baada ya burudani hiyo, akili inakuwa tayari kufanya kazi ngumu. Uandishi wa masuala ya kawaida, pamoja na usomaji wa vitabu, ni burudani ya kutosha.
Vitabu vyangu vinapatikana mtandaoni, http://www.lulu.com/spotlight/mbele na Amazon.com. Vinapatikana kama vitabu halisi, lakini vingine pia kama vitabu pepe. Ninapenda vipatikane Tanzania pia. Kwa sasa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kinapatikana kwenye kituo cha utalii cha Burunge, mkoani Manyara: imborutours@gmail.com
kitabu 1

Fani hii ya uandishi, unadhani vijana tumeivamia? Au basi unaridhishwa na kiwango cha uandishi wa vijana hasa tunaochipukia?
PROF: JOSEPH MBELE
Ninadhani yeyote mwenye hamu ya kuandika awe huru kufanya hivyo. Kinachotakiwa ni uvumilivu, kwani haiwezekani kuwa mwandishi bora haraka bila uzoefu. Pia, ni lazima vijana na waandishi kwa ujumla wawe wasomaji makini. Kutegemea na aina ya uandishi ambayo kijana anataka kuandika, awasome waandishi wa mataifa mbali mbali waliotukuka katika aina ile ya uandishi.

Watu wengi wanadhani kazi ya uandishi inalipa na kutajirisha haraka-haraka. Wakati mwaandishi uambulia mrahaba wa asilimia kumi (10%) katika mauzo ya kazi yake ama asilipwe kabisa.
PROF: JOSEPH MBELE
Mwandishi aandike pale anapoona ana jambo la kusema. Msukumo utoke ndani mwake, na akisha andika ajisikie ametua mzigo. Asihamakie mambo ya nje, kama vile pesa. Mategemeo ya pesa hayaleti uandishi bora. Fundisho hili tumepewa na waandishi maarufu, kama vile Ernest Hemingway wa Marekani na Mario Vargas Llosa wa Peru. Jambo la msingi ni mwandishi kuiridhisha nafsi yake, na kuikubali kazi yake, kwamba imewasilisha kwa uaminifu na ukweli yale aliyokuwa nayo moyoni. Akiridhika kabisa, hiyo ni tunu bora kuliko pesa. Fedha ni matokeo. Vile vile, ni waandishi wachache sana duniani wanaopata fedha ya kuwawezesha kumudu maisha kutokana na uandishi. Waandishi chipukizi watambue hilo, na wale ambao hawana nia ya dhati ya kuwa waandishi wakumbuke hilo, wasije wakajisumbua na ndoto za bure.
Ninavyofahamu, mrahaba wa 10% au zaidi kidogo ni wa kawaida duniani kote, isipokuwa kwa waandishi maarufu.

Je wewe unadhani ni sahihi mtu kuandika kitabu mwaka ama zaidi na kulipwa ujira wa kipuuzi namna hii?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema, msukumo wa mwandishi uwe kusema yaliyomo moyoni mwake, kwa uaminifu na ukweli kadiri inavyowezekana. Kutokana na hilo, waandishi makini hutumia muda mwingi kurekebisha maandishi yao. Ukisoma habari za waandishi maarufu, kama Hemingway, utashangaa jinsi walivyokuwa wanarekebisha maandishi yao mara nyingi sana, na pengine kuishia kutoridhika na kuyaweka kando. Haraka haraka haina baraka. Kitabu kinaweza kuhitaji miaka mingi kukifikisha katika hali ya kumridhisha mwandishi makini. Mimi mwenyewe nilitumia miaka yapata 23 kukiandaa kitabu cha Matengo Folktales.
kitabu 2

Wachapishaji wengi duniani walikuwa kama miungu watu. Na hata basi hao watunzi waliokuwa na vipaji vikubwa kama akina Shaaban Robert, bado awakuwa na sauti mbele yao. Walikiwa ni watu wa kunyenyekewa sana na hata watu kujipendekeza. Ili tu kazi zao zichapishwe.
Lakini sasa naona kiburi hiki kinaanza kufyekwa-fyekwa na utandawazi. Mimi ninaomba utufafanulie ni namna gani waandishi wanaoteseka miaka na miaka wanaweza kufanya kusudi kuchapisha kazi zao kwa kutumia mtandao
PROF: JOSEPH MBELE
Ni kweli, wachapishaji wamekuwa kama miungu watu. Hata Shaaban Robert alilalamika kuhusu wachapishaji. Ni kweli kuwa siku hizi kuna tekinolojia za uchapishaji mtandaoni ambazo zinamwezesha mwandishi yeyote kuchapisha kitabu chake. Kinachotakiwa ni kwa mwandishi kujibidisha kusoma kuhusu tekinolojia hizi na akiamua, azitumie. Kuna aina tofauti za uchapishaji wa mtandaoni, na ni juu ya mwandishi kuamua anaipenda zaidi ipi.

Je kuna madhara gani yanaweza kujitokeza katika mfumo wa kujichapishia katika hiyo mitandao?
PROF: JOSEPH MBELE
Sidhani kama kuna madhara. Badala yake, naona uchapishaji wa mtandaoni umeleta demokrasia zaidi katika uwanja wa uchapishaji, tofauti na jadi tuliyozoea ya wachapishaji kuhodhi mamlaka.
Kuna watu ambao wanalalamika kuwa uhuru huu umesababisha machapisho ya viwango duni kuchapishwa kiholela. Hilo ni suala tata. Tukiangalia kwa upande wa wasomaji ambao tunaweza kuwaita wateja, nafikiri tunapaswa kutambua kuwa wao ndio waamuzi. Ninaamini kuwa wataweza kupambanua kati ya kilicho bora na kilicho duni.

Mtu anapochapisha katika mtandao labda. Labda mwingine anataka tu achapishe haraka-haraka ili aonekane na kupata pesa, bila hata kazi yake kuhaririwa uoni ni tatizo pia?
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema hapa juu, ninawategemea wateja. Kama mwandishi atachapisha kitabu duni, anaweza kuwadanganya wanunuaji wa mwanzo, lakini wateja huambiana kuhusu kitu walichonunua. Kama ni kibovu, kitakosa wanunuaji. Isipokuwa, labda niongezee kuwa mtazamo wangu huu umejengeka katika imani kwamba wateja ni watu wenye akili, kwani kama akili yao ni duni, hoja yangu itadhoofika.

Kuingia kwa teknolojia kwa kasi. Je unahisi ipo siku haya makampuni ya kuchapisha yatageuka na kuwa maghala?
PROF: JOSEPH MBELE
Suala hili linajadiliwa sana katika ulimwengu wa leo. Jambo moja linalojitokeza ni kwamba makampuni kama yale ya Marekani yameshaanza kujihami kwa kuingia katika matumizi ya hizi tekinolojia mpya za uchapishaji, sambamba na uchapishaji wa jadi. Hakuna anayejua kama uchapishaji wa jadi utakufa kabisa. Nikitoa mfano wa kuwepo kwa vitabu pepe, jambo moja ambalo ni wazi ni kuwa watu wengi wanataka kushika kitabu mkononi kama zamani, pamoja na kwamba siku hizi kuna vitabu pepe.

Licha ya mfumo wa kujichapishia mtandaoni kwa mrahisi kidogo. Uoni kama ni ishara ya kukubali na kukaribisha ukoloni mpya kwa mikono miwili? Au kusema shikamoo ukoloni?
PROF: JOSEPH MBELE
Tekinolojia ya kujichapishia mtandaoni, kama nilivyosema, imeboresha demokrasia katika uchapishaji. Kwa msingi huo, hata waandishi ambao hawakuwa na fursa ya kujieleza kwa walimwengu sasa wanayo fursa. Ukoloni wa fikra ambao ulisambazwa sana na vitabu, vitabu vilivyochapishwa kwa mtindo wa kibabe kama tulivyosema hapa juu, unaweza kupigwa vita na wanyonge kwa kutumia tekinolojia hii ya uchapishaji mtandaoni.

Kuna watu wanaondika. Na wapo wengi wanaojifunza kuandika na wanapenda! Lakini wanakatishwa tamaa kutokana na mifumo iliyopo kama kupuuzwa na kuachwa.
Naomba uwape neno na kuwatia nguvu.
PROF: JOSEPH MBELE
Kama nilivyosema hapa juu, mtu mwenye nia ya dhati ya kuandika hawezi kuyumbishwa. Anafuata msukumo wa moyoni mwake hadi mwisho. Anayekatishwa tamaa ni yule ambaye hakuwa thabiti katika nia na msukumo wa ndani. Mimi mwenyewe, naandika vitabu kwa sababu siridhiki na vile ninavyovisoma. Ninaandika vitabu ambavyo ningependa viwepo bali havipo, vitabu ambavyo ningependa kuvisoma, bali sivioni. Kwa hivi, kwa kiasi kikubwa ninajiandikia mwenyewe. Siyumbishwi na yeyote.
Ustahimilivu ni muhimu katika uandishi. Waandishi maarufu wa kimataifa wanaongelea jambo hilo. Wanakumbana na vipingamizi, lakini hawakati tamaa. Kipingamizi kimoja ni kuwa kuna nyakati ambapo mwandishi anashindwa kuandika. Akili haifanyi kazi. Mwandishi wa kweli hakati tamaa. Anajua kuna wakati utakuja ambapo ataweza kuendelea kuandika.
Vile vile wako waandishi ambao kazi zao zilikataliwa mara nyingi na wachapishaji. Hawakukata tamaa. Baada ya kuchapishwa, kazi hizo hizo zilizokataliwa zilikuja kuwa maarufu. Mwandishi mwenye msukumo wa
kutoka ndani, ana kiu ya kuandika. Akisha andika anakuwa na faraja au furaha. Hawezi kuacha kuandika, wala hawezi kukatishwa tamaa.

Picha zote kwa hisani ya http://www.josephmbele.blogspot.com
CHANZO: Mandelapallangyo.com

2 comments:

kitoi said...

Huyu kijana mandela siku hizi ameaznisha mtandao. unaitwa pallachat hata vitabu vyako uwa anaviweka sana huko. ila masikini ajapata msaada katika kuboresha na kuoneza mtandao huo. wa pallachat www.pallachat.com

http://pallachat.com/index.php?tab1=timeline&id=MANDELA

Mbele said...

Ndugu kitoi

Shukrani kwa taarifa. Ninaona huyu kijana ana bidii katika masuala haya ya kusaka na kusambaza elimu. Kila la heri.