
Mwanzoni mwa wiki hii, tarehe 19, nilipata ombi la urafiki katika Facebook. Nilivyoona jina la mhusika, Sandy, nilihisi kuwa si jina geni. Nilipoangali picha yake, nilikumbuka kuwa ni mama aliyewahi kunitembelea hapa Chuoni St. Olaf akiwa na rafiki yake, Desemba 2011. Niliandika habari za ujio wao katika blogu hii. Bila kuchelewa, nilikubali mwaliko wa urafiki.
Jana nimepata ujumbe wa mama huyu katika Facebook. Wakati tulipoonana, huyu mama na mwenzake walinunua vitabu vyangu, na aliniambia kuwa nakala ya Africans and Americans: Embracing Cultural Differences alikuwa anamnunulia rafiki yake ambaye alikuwa anapanga safari ya kwenda Afrika.
Kwa bahati mbaya tulipoteana kwa miezi mingi. Hatukuwa na mawasiliano. Baada ya kuungana tena katika Facebook, jana huyu mama ameniandikia ujumbe mfupi: My friend loved your book about the African culture. She had a wonderful experience.
Nimefurahi. Ni jambo la kushukuru kukumbukwa na mdau namna hii. Inaonyesha kuwa tulivyokutana mara ya kwanza tulikutana kwa uzuri na kumbukumbu zikabaki. Nashukuru pia kusikia kuwa rafiki ya huyu mama amekifurahia kitabu changu na safari yake ya Afrika.
Taarifa za aina hii kutoka kwa wadau wangu nazipata muda wote. Zinanipa raha maishani na hamasa ya kuendelea kufanya ninayofanya kama mwandishi na mtoa ushauri. Kuridhika na kufurahi kwa wadau ni tunu kubwa kwangu kuliko malipo ya fedha. Ninamshukuru Mungu kwa yote. Ninamwomba aendelee kunipa uzima siku hadi siku, na akili timamu, niweze kuendelea na majukumu.
2 comments:
Kaka Mbele hakuna kitu chenye kufurahisha na kuliwaza kama kupokea ujumbe juu ya kazi yako tena wenye taathira chanya. Hata hivyo, kwa msomaji makini kitabu chako si haba. Huwa nikiona masuala ya ubaguzi na maswali ya kijinga kuhusu Afrika huwa narejea na kujichotea maarifa.
Ndugu Mhango
Shukrani kwa ujumbe wako. Kwa kweli, kuweza kuwagusa watu kwa namna ya kujenga fikra njema na mahusiano mema, kuwapa matumaini na hamasa ya kuishi na kufanikiwa katika mema, ni faraja na tunu kubwa kwa waandishi wa aina yetu.
Kwa ujumla, jamii yetu ya Tanzania haijali hayo. Ukiwaambia kuwa hayo ya kuwagusa watu ni mafanikio makubwa, wanakushangaa, kwa sababu kigezo chao cha mafanikio ni fedha. Jamii yetu imepotea njia, tofauti na enzi za akina Shaaban Robert na Mwalimu Nyerere.
Post a Comment