Tuesday, July 7, 2015

Ukiwa na Siri Iweke Kitabuni

Wengi wetu tumesikia kwamba ukiwa na siri iweke kitabuni; mw-Afrika hataiona. Kwetu wa-Tanzania, hali ni hiyo hiyo. Mwaka hadi mwaka, tumekuwa tukisikia jinsi utamaduni wa kusoma vitabu unavyokosekana Tanzania. Si jambo la kujivunia.

Nimekuwa nikiandika mara kwa mara hali ninayoiona hapa Marekani, katika matamasha ya vitabu, maduka ya vitabu, na maktaba. Wa-Marekani kama inavyoonekana katika picha nilizoweka hapa, wana tabia tofauti.

Picha ya katikati niliipiga katika tamasha la vitabu Minneapolis. Ya chini niliipiga katika tamasha la vitabu Mankato. Picha ya juu kabisa sikumbuki niliipata wapi. Zote zinaonyesha jinsi watu wanavyosaka vitabu na kuchungulia yaliyomo. Sijui kama kuna siri iliyofichwa kitabuni ambayo hawataigundua.

Ninaweza kuleta mfano moja mdogo kutokana na kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambamo nimeweka taarifa kuhusu wa-Marekani na wa-Afrika. Tangu kichapishwe, mwaka 2005, maelfu ya wa-Marekani wamekisoma. Wanazijua siri zilizomo.

Mama mmoja m-Tanzania aliyeanzisha na anaendesha taasisi fulani alikuja hapa Marekani kuonana na washirika wake. Kwenye jimbo la Colorado aliulizwa kama amesoma kitabu hiki. Alikiri kuwa hakuwa amekisoma. Baada ya kurudi Tanzania, aliwasiliana nami akanielezea tukio hili. Tulifanya mpango, nikampelekea nakala.

Hiyo si hali ya kujivunia. Wenzetu wa-Marekani wanazoeshwa kuvipenda vitabu tangu utotoni. Wanakulia katika utamaduni huo. Kutokana na kulelewa katika utamaduni huo, hata wazee wananunua na kusoma vitabu, kama vilivyowahi kuandika katika blogu hii.

2 comments:

Abias Laurian said...

Nimesoma ujumbe huu nimejifunza mengi... Kwa mwaka huu jukumu langu kubwa ni kusoma vitabu vingi iwezekanavyo, natamani sana nitimize jukumu hili.

Mbele said...

Ndugu abias laurian, umefanya uamuzi mzuri. Mimi nimekuwa mpenda vitabu tangu nilipokuwa kijana kule kijijini. Nina mazoea ya kununua vitabu. Usomaji wa vitabu umenifikisha hapa nilipo. Dunia inazidi kuwa ya "knowledge economy" ambamo "knowledge" ni mtaji wa thamani kuliko mingine yote.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...